Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza nami nachangia bajeti ya Serikali, lakini siyo kwa mara ya kwanza kabisa, bajeti hii Kuu ya Serikali siku ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, natamani nisome kipande kidogo cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kabla sijaanza kuchangia kwa sababu lengo langu leo nataka nichangie zaidi kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 12 Waziri wa Fedha alituambia; “Mheshimiwa Spika, kwa kutambua ukweli kuwa asilimia kubwa ya wananchi wetu wanaishi vijijini ambapo kilimo ndiyo msingi wa ustawi wa maisha, Serikali ya CCM chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea na dhamira yake ya kuboresha maisha ya wananchi kwa kuongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294.0 mwaka wa fedha 2021/22 hadi shilingi bilioni 954.0 mwaka wa fedha 2022/23 na kufikia shilingi bilioni 970.8 mwaka huo ambao tunauanza. Kuongezeka kwa bajeti ya kilimo kumewezesha kuongezeka kwa upatikanaji wa pembejeo za kilimo; kuanzishwa kwa kilimo cha mashamba makubwa ya pamoja; kuimarisha tafiti na huduma za ugani; kutolewa kwa ruzuku ya mbolea kwa wakulima; kuanza kwa miradi ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji na miundombinu…” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesoma kipande hiki ili kukumbusha tu maelezo mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, dhamira njema ya Serikali kuhusu kilimo chetu.

Mheshimiwa Spika, sisi wananchi wa Mikoa ya Singida, Simiyu na Dodoma tulipewa kazi ya kuzalisha alizeti kwa wingi ili kupunguza pengo la mafuta katika nchi yetu. Lakini leo ni majuto makubwa sana kwa wakulima wetu. Majuto yanakujaje? Badala ya kuongeza kodi ya mafuta yanayoingizwa nchini sasa inakwenda kupungua.

Mheshimiwa Spika, lakini leo tunapozungumza kilo ya alizeti sasa ni shilingi 500. Hapa Mjini Dodoma tulipo ukitaka kununua galoni ya mafuta ya kula ya alizeti ni shilingi 18,000, ikizidi 20,000. Hivi leo tunazungumza nini juu ya mkulima wetu wa Tanzania? Ananufaikaje na kilimo hiki ambacho Serikali ilitoa mbegu, ikatoa ushaiwishi mkubwa kwa wananchi ili walime alizeti, leo imeshuka sana.

Mheshimiwa Spika, tunapokwenda kupunguza kodi za mafuta ghafi yanayotoka nje, tunakwenda kuwaua wakulima wetu. Ninaomba Serikali iache uthubutu huo inaotaka kufanya. Tusaidie wananchi wa Tanzania, wakulima wetu ambao walitumia nguvu kubwa na ushawishi wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda Singida akafanya mkutano kushawishi wananchi walime sana alizeti. Wizara ya Kilimo ikaleta mbegu, wananchi wakachukua na wamelima, leo alizeti imeshuka sana, wananchi wana majonzi.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Serikali, namwomba Waziri wa Fedha, mwana-Singida mwenzangu, awaangalie wananchi wa Mkoa wa Singida. Wasipunguze kodi za mafuta ghafi yanayotoka nje ya nchi ili angalau alizeti ipande kidogo, ili Watanzania waliolima mwaka huu kwa ushawishi wa Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi waweze kunufaika na mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi hii ya Tanzania ili tutoke katika umaskini na kama alivyosema hapo Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba uti wa mgongo wa nchi hii ni kilimo, na wakulima ndiyo asilimia kubwa ya Watanzania, kilimo cha umwagiliaji ndiyo suluhisho. Leo tunapozungumza hatujafikia asilimia kumi ya ardhi ambayo inafaa kwa kilimo kulimwa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna eka zinazopungua milioni moja za umwagiliaji. Tumeona bajeti ilivyoongezeka kwa asilimia 300 ya bajeti iliyokwisha, lakini hatujaona mafanikio kwa asilimia 50 ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yetu. Mimi ninapozungumza hapa sina skimu hata moja iliyo kwenye mpango kwa bajeti iliyopita. Kama Mbunge wa Jimbo, Halmashauri yangu ya Itigi katika Halmashauri 184 haimo katika mipango ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, kama tuna nia ya kuisaidia nchi hii tutokane na umaskini na watu wetu, tutoke katika kilimo cha kutegemea mvua. Hatuwezi kutoka moja kwa moja, lakini tusaidie wananchi wetu, tuongeze skimu za umwagiliaji katika maeneo yetu. Ardhi inayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mujibu wa maelezo ya kitaalam ni ekari milioni 22. Leo ekari milioni moja hatuna Tanzania.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti iliyokwisha Wizara ya Kilimo ukiondoa kule kwenu Mbeya, ile Madibila maeneo mengine bado tunahangaika tu. Ninaomba sasa Serikali itie mkazo katika kilimo cha umwagiliaji, kitakuwa na tija na ni mkombozi wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwenye ruzuku za mbolea kuna jambo ambalo tunashangaa ni kwa nini linatokea. Mmegawa wakulima kwa madaraja, wakulima wa pamba, wakulima wa tumbaku mbolea yao haina ruzuku. Maana yake ni nini; hawana faida, hawafai, hawatakiwi? Kwa nini mbolea isiwe na ruzuku kwa wakulima wote, uchague zao la kulima ili iwe tija kwa mwananchi.

Mheshimiwa Spika, inapoongezeka bajeti ya Wizara ya Kilimo kwani hawa wakulima wa pamba hawajachangia katika mapato ya nchi hii? Hawajachangia kodi ambazo zimesababisha wao kuongezewa? Wakulima wa tumbaku ambao kule kwangu Itigi nao wanalima mbolea yao haina ruzuku.

Ninaomba Serikali iondoe huo ubaguzi wa kubagua wakulima wa aina ya mazao fulani. Twende kama wakulima ruzuku inayopewa mbolea nchi nzima wapate ruzuku ya mbolea.

Mheshimiwa Spika, nina jambo lingine ambalo nataka kulichangia; mifumo ya TEHAMA. Mifumo ya TEHAMA katika Halmashauri zetu, Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Mawaziri wake hawa wamepeleka miradi mingi katika maeneo yetu, lakini mifumo haifunguki, miradi haitekelezeki. Wanachukua bidhaa za watu, wanachukua mafuta kwenye petrol stations, namna ya kuwalipa inakuwa mtihani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba mifumo ifunguke, lakini pia isomane. Mifumo ya Halmashauri haisomani na TRA. Mifumo ya Halmashauri haisomani na maeneo megine. Hata Bandari na TRA mifumo haisomani…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, tunatamani kuona mifumo hii iwe mifumo imara ambayo ili utekelezaji wa bajeti na hasa utekelezaji wa miradi hii kule vijijini kwenye Halmashauri zetu iweze kufanyika vizuri.

SPIKA: Mheshimiwa Yahaya Massare, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa msemaji kwamba sasa hivi leo ni siku karibu ya 25 Halmashauri zote zimesimama uendeshaji wake na mifumo imezimwa, na tunakwenda kumaliza bajeti, tunataka hili analolizungumza Mheshimiwa Yahaya ni la msingi shughuli za Serikali zimesimama, nini mustakabali wa hili jambo? Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Yahaya Massare, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, taarifa naipokea kwa sababu ni suala la ukweli. Mimi ninapozungumza hapa Halmashauri yangu ya Itigi vitu vimesimama. Serikali imetuletea, tunajenga Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya pale, lakini wale wanaotusaidia kuhudumia pale wamesimama na wamekwama kwa sababu mfumo umezima kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, hata Madiwani wangu kule Itigi hawajalipwa kutokana na mifumo imesimama, imezimika, haifanyi kazi. Kwa hiyo, ni mambo ya kweli na nataka twende sasa tuwe na mifumo imara ambayo itafanya kazi kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka nitumie fursa hii kuishukuru Serikali kwa namna ilivyofanya hasa katika miundombinu, tumeona barabara kilometa zikisainiwa, majuzi tu, kwangu kule Itigi tunajenga barabara kwa kiwango cha lami, kilometa 56.6, ninaomba sasa Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya ahsante sana.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: …zimebaki kilometa 356 kuja Mbeya kule kwako pale Makongorosi.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa basi Mheshimiwa Waziri aiweke katika mipango yake na mimi niingie katika utaratibu huo wa barabara ya lami. Ahsante sana kumalizia barabara ya Makongorosi – Mkiwa hadi Itigi, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja hizi za Bajeti Kuu ya Serikali. (Makofi)