Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami naomba nichangie hii Bajeti ya Wizara ya Fedha. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika hii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Segerea Kata ya Kipunguni kwa Mheshimiwa Waziri kuiweka Bajeti ya Malipo ya Fidia ya Kipunguni Kata ya Kipawa kwenye hii Bajeti, tunashukuru sana sana kwa sababu hawa wananchi wamekaa muda mrefu bila kupata malipo yao takribani miaka 30. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunakushukuru lakini tunaomba ulisema utapeleka wakaguzi ambao wanatoka Wizara ya Fedha tulikuwa tunaomba uwapeleke kwa haraka ili hawa wananchi waweze kupata fedha zao na ikiwezekana mwezi wa, huu tuko mwezi wa sita basi mwezi wa saba waweze kuanza kulipwa Mheshimiwa Waziri tutashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na barabara. Barabara za DMDP ambazo nimekusikia Mheshimiwa Waziri umeziingiza kwenye Bajeti ya mwaka huu tunashukuru sana. Nimekuwa nikichangia hapa kwa muda wa miaka karibuni mitano kuhusiana na Barabara za DMDP. Mkoa wetu wa Dar es Salaam Mheshimiwa Waziri unategemea sana miundombinu na tunapata wawekezaji wengi kuja kuwekeza kwenye nchi yetu lakini lango kubwa ambalo wanatumia ni kwanza wanaingia Dar es Salaam na wanapitia katika Airport yetu, Airport ya Dar es Salaam International Airport. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia mazingira ya Mkoa wa Dar es Salaam kuhusiana na miundombinu kwa kweli imekuwa hairidhishi. Kwa hiyo, kitu ambacho tunaomba pamoja na kwamba umeweka barabara kwenye hii Bajeti basi tunaomba ianze haraka kwa sababu kumekuwa kuna ucheleweshaji sana. Mfano kama mkitangaza hizi miundombinu au mkitangaza Bajeti kwamba kuna barabara zitajengwa hazianzi wakati huo huo zinakuwa zinachukua hata miezi sita Mheshimiwa Waziri au hata mwaka. Kwa hiyo, kwa sababu sasa hivi wananchi wetu wengi wamesikia kwamba kuna barabara sasa zinaenda kutengenezwa, barabara za DMDP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba kwa kuwa Mheshimiwa Waziri mmetangaza na mmesaini, na kupongeze sana pia nimpongeze Waziri wa TAMISEMI. Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Angellah Kairuki alikuja kufanya ziara katika Jimbo langu la Segerea. Unaweza ukaona Mheshimiwa Waziri kwamba Jimbo la Segerea lipo mjini lakini ukitembelea maeneo yake mengi ni barabara kama ziko vijijini. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ameziona na ameona jinsi gani wananchi wanahangaika kutokana na barabara kuwa mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri hii bajeti ambayo ameisoma na ameweka miundombinu tunaomba hiyo miundombinu iende ikatengenezwe kwenye Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni kuhusiana na wakandarasi wetu. Mkoa wetu wa Dar es Salaam miundombinu yake au jiografia yake ni kama unavyoiona. Inakuwaje barabara inatengenezwa na inakuwa mpya lakini mvua ikinyesha masaa mawili unashangaa maji yamejaa Dar es Saalam nzima na inaweza ikasababisha masaa matatu hakuna kitu chochote kinachofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo tunaomba hata hawa wakandarasi ambao wanaenda kututengenezea sasa hizi barabara wazingatie jiografia ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa sababu kuna sehemu nyingine kwa mfano Jimbo la Segerea kuna miinuko na milima mingi. Sasa tunaomba wakandarasi wawe wanaangalia sehemu ambazo wanaenda kutengeneza barabara ili sasa kuondoa yale matatizo, kwamba barabara ikishatengenezwa basi hayo maji yasijae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni kuhusiana na taasisi hizi mbili ambazo zote ni za Serikali; maji pamoja na miundombinu. Unaweza ukashangaa barabara imejengwa haina hata miezi miwili nao watu wa DAWASA wanakuja wanchimba kwenye ile ile barabara ambayo imejengwa haina hata miezi miwili. Kwa hiyo mimi napendekeza; hizi taasisi zote mbili ni taasisi za Serikali, kwa hiyo kwa nini zisiwe zina mawasiliano ya karibu? Kwamba sisi sasa hivi tunataka kujenga hapa barabara je, kuna bomba lolote la maji ambalo linaweza kupita, kwa sababu linaleta usumbufu mkubwa sana. Na yale mashimo ambayo wanachimba watu wa DAWASA yanakaa muda mrefu sana na yanasababisha watu wanapata ajali. Kwa hiyo tunaomba barabara kama inajengwa watu wa DAWASA wawe wameshapita na kuweka mabomba yao, tunaomba sana. Hilo pia litasaidia hata Serikali kutokupata hasara kwa sababu barabara inapojengwa halafu tena inaenda inabomolewa ina maana kuna hasara ambayo inaongezeka hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni kuhusiana na TARURA. Tunashukuru sana TARURA kwa kipindi kirefu imekuwa ikipata hela bajeti ambayo si kubwa lakini sasa hivi naona mmeongeza bajeti. Kwa hiyo tunaomba hiyo bajeti ambayo imewekwa kwenye TARURA iende ikafanye kazi kwa haraka. Jambo lingine ni kuhusiana na fedha ambazo zinakusanywa na halmashauri, zile asilimia 10, tulisema kwamba kuna fedha ambazo zinaenda kwenye barabara. Sasa kumekuwa katika kipindi hiki cha kama miezi sita kuna hela ambazo zimepelekwa kwa mkurugenzi kwa ajili ya kutengeneza barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hizi fedha ambazo zinapelekwa kwa Mkurugenzi, sasa hivi tangu imeanzishwa Taasisi ya TARURA mkurugenzi hana mainjinia, kwa hiyo kumekuwa kuna tatizo la ucheleweshaji wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Segerea kuna barabara ambazo tulikuwa tumezitembelea tangu mwaka jana ambazo zilikuwa zimewekwa ili zitengenezwe na halmashauri kutokana na ile asilimia, lakini mpaka sasa hivi ninavyoongea hizo barabara hazijatengenezwa kwa sababu kumekuwa kuna ucheleweshaji kati ya TARURA na halmashauri. Halmashauri sasa hivi hawana mainjinia, kwa hiyo tunaomba hizi fedha ziendelee kupelekwa TARURA. Kwa sababu jambo hili unafuatilia halmashauri halafu ukifika Mkurugenzi anakwambia mimi sina injinia, kwa iyo inabidi urudi TARURA. Kwa hiyo kumekuwa na ucheleweshwaji sana. Kama mlikuwa mnapeleka hizi fedha TARURA basi tunaomba tu muendelee kupeleka TARURA hizi fedha ili watu waweze kuendelea kupata barabara kwa haraka pia TARURA waweze kufanya kazi yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni mifumo ya halmashauri. Sasa hivi mwezi mzima hakuna kitu kinafanyika shughuli zimelala, mifumo yote haisomi. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba, sijui ni jambo gani Mheshimiwa Waziri, naomba ulishughulikie. Kwa sababu kama mwezi mzima mifumo ikiwa haisomi ina maana hata itakapofunguliwa unaweza ukakuta kuna mapato yamepotea au kuna wizi umetokea mpaka mje mgundue inakuwa ni imechukua muda. Kwa hiyo tunaomba ulishughulikie jambo hilo ili mifumo iweze kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na sheria za kodi. Nafikiri hizi sheria za kodi kama zingepitiwa upya hata kusingekuwa na migogoro ambayo inaenda kutokea, kwa mfano kama mgogoro uliotokea Kariakoo kuhusiana na wafanyabiashara, na Iringa. Napendekeza, kama inawezekana hizi sheria ziletwe Bungeni ili tuweze kuzipitia upya ili ziweze kuwa sheria rafiki. Hii ni kwa sababu hii migogoro itakuwa inaendelea kila siku. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenda kumaliza huu mgogoro ambao ulitokea Kariakoo. Kwa hiyo tunaomba sana sheria hizi uangalie Mheshimiwa Waziri ili ziweze kuwa ni sheria rafiki ili tuweze kuendelea na mambo mengine ambayo yanaweza yakatuingizia kipato kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu elimu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fedha ambazo zimekuja katika Jimbo letu la Segerea pia Mkoa wa Dar es Salaam mzima. Katika Jimbo langu la Segerea tumepata fedha nyingi sana kwa mwaka ambao umepita na tumejenga miundombinu mingi sana ya elimu. Na mpaka sasa hivi tunajenga maghorofa matatu kwa ajili ya sekondari. Pia tunajenga madarasa mengi kwa kutumia fedha ambazo zimekuja kwa ajili ya elimu. Kwa hiyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: …tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais pia tunakushukuru Mheshimiwa Waziri naunga mkono hoja.