Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijaanza kuchangia, naomba nitoe shukranI zangu mbele ya Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kufika hapa. Pia napenda kushukuru chama changu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kunifikisha hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Mpango huu kuna mambo mawili au matatu ambayo nahitaji kuchangia. Jambo la kwanza ni kuhusiana na uvuvi haramu pamoja na uwindaji haramu ambao unaendelea katika nchi yetu. Sasa katika Mpango huu ambao nimeupitia sijaona kama kuna mkakati wa kuweza kuzuia hao majangili ambao wanaendelea kuua watu wetu na kuiba wanyama. Pia kuna wawindaji ambao wanapewa vibali halali, ningeomba Serikali sasa kupitia huu Mpango iweke mkakati wa kuhakikisha kwamba pamoja na kupewa vibali lakini ijulikane ndani ya hizo National Park wanafanya shughuli gani. Nikitoa mfano kwenye Mkoa wangu wa Katavi kuna Wapakistan zaidi ya 40 ndani ya lile pori, lakini ukiulizia ni shughuli gani wanafanya siyo za kiuwekezaji. Nimewahi kutembelea pale, unakuta wengi wao ni madereva lakini wengine wanapika, ndiyo wanaohudumia kwenye hoteli pale ndani. Kama Serikali tuangalie hawa wawindaji ambao wana vibali kabisa vya kuwinda katika mbuga zetu wanafanya shughuli gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya mbuga pia kuna viwanja vya ndege, sasa hatuwezi kuelewa hawa wawindaji wanasafirisha vitu gani. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tusiendelee kulalamika kwamba ndovu wanaibiwa inabidi kuchukua hatua. Nitoe masikitiko yangu kwa rubani ambaye alitunguliwa na hawa majangili katika mbuga ya Meatu. Kama Serikali au TANAPA wameshindwa kuweka usalama kwa hawa mapolisi ambao wanalinda wanyama wetu pamoja na mbuga zetu basi ni bora tukajua ni jinsi gani tunawalinda hawa wanyama wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mchango wangu wa pili unajikita katika viwanda. Mapinduzi ya viwanda yanatakiwa yaendane na uzalishaji wa umeme yaani huwezi ukazungumzia viwanda bila kueleza unaongezaje nguvu ya umeme katika viwanda vyetu. Mpaka sasa Tanzania tunazalisha umeme megawatts 1,247 lakini Mpango Mkakati wa Miaka Mitano uliopita Serikali iliweka mpango wa kuongeza uzalishaji wa umeme wa megawatts zaidi ya 2,780 lakini hatukufikia malengo. Tunapozungumzia mapinduzi ya viwanda basi tuhakikishe kwamba nguvu kubwa tutaongeza kwenye uzalishaji wa umeme kwa sababu hatuwezi tukazungumzia viwanda bila umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme hatuzungumzii kwenye viwanda tu pia tunauzungumzia kwenye matumizi ya kawaida ya wananchi wetu nikitoa mfano wa Mkoa wangu wa Katavi. Mkoa wa Katavi mpaka sasa tunatumia umeme wa generator hata kama tuna viwanda vidogo vidogo kwenye mkoa wetu basi hatuwezi kuzalisha product ya aina yoyote kwa sababu umeme siyo wa uhakika. Kuna kipindi inafikia wiki nzima wananchi wa Mpanda au Mkoa wa Katavi wanakosa umeme. Kwa hiyo, mapendekezo yangu katika suala la umeme Serikali iangalie sasa ni jinsi gani tunakwenda kuweka mikakati mizuri katika kuweka nguvu ya kuzalisha umeme hasa kwenye kipimo cha megawatts. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa tatu unajikita zaidi kwenye afya. Kama Serikali tunahitaji kufikia malengo, maana nimesoma Mpango huu una mipango mizuri kabisa ambayo inatakiwa tuifikie kwa ajili ya ku-achieve hizo goals ambazo mmeziweka. Kitu ambacho nakiona kinafeli zaidi katika Mipango yote ni kwamba tuna mipango mizuri lakini lazima kuwe na implementation na monitoring lakini Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali tatizo hakuna ufuatiliaji. Kwa hiyo, naomba Serikali hata kama mnajikita kwenye sekta binafsi, sekta za afya, pamoja na elimu, inapopangiwa bajeti fulani basi implementation iongezwe kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilohilo la afya, Mkoa wangu wa Katavi ni almost kama miaka saba iliyopita mpaka leo tumepata Manispaa Serikali ilitoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa na kuna eneo kubwa karibuni heka mia tatu lilishanunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo lakini mpaka sasa hakuna dalili yoyote ambayo inaonesha hospitali itajengwa lini. Pia wale wananchi ambao walikuwa wanakaa kwenye eneo ambalo Serikali ililinunua mpaka sasa wengi wao hawajalipwa. Naomba Serikali katika mpango wenu mhakikishe ujenzi wa hospitali katika mikoa au manispaa mbalimbali unafanyika lakini pia bajeti yake ipangwe na kuonyeshwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nilitaka kuzungumzia kuhusiana na ukusanyaji wa mapato. Tunapozungumzia ukusanyaji wa mapato kama Serikali ya CCM miaka yote tunalalamika lakini mchawi ni nani? Kuna watu ambao hawalipi kodi lakini Serikali imekaa kimya, miradi inashindwa kutekelezwa, tuna mipango mizuri lakini kodi tunapata wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge katika Bunge lililopita 2010, kulikuwa kuna kashfa ya sukari, kuna watu ambao walihusika na kutoa vibali vya Serikali na wengine wakaenda kununua sukari nchini Brazil kuleta Tanzania. Hasara tuliyopata kwenye kashfa ile ya sukari ni zaidi ya shilingi bilioni 300. Wengi wao wengine tunawafahamu kwa majina akiwepo Mheshimiwa Mohamed Dewji. Kwa hiyo, naomba kabisa ile ripoti ya Kamati ya Bunge iletwe hawa watu washughulikiwe na walipe kodi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa kama hizi zinapotea kumbe tungeweza kufanya maendeleo kutokana na kodi hiyo. Kuna watu tunawaachia wanarandaranda na wanatumia pesa za wananchi. Kwa hiyo, naomba Serikali tuwe strict kuangalia ni mianya gani inayosababisha tunapoteza pato la Serilkali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaposema tunahitaji kuwekeza katika elimu basi tuwakumbuke Walimu wetu kwa kuwalipa mishahara yao lakini pia tutengeneze mazingira mazuri katika shule zetu. Ahsante. (Makofi)