Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kunipatia nafasi niweze kuchangia ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, nawapongeza kwa sababu ya usikivu, changamoto zipo kama binadamu lakini mkiendelea kusikiliza naamini hayo mengine ni ya kawaida katika shughuli zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa masikitiko makubwa sana kwamba ni namna gani tumeshindwa kuwekeza kwenye Ziwa Tanganyika. Nitaanza kwenye eneo moja tu. Ukiangalia mipango ya Waziri wa Kilimo ni mipango mizuri sana, leo tunapozungumzia mapinduzi ya uchumi yatakayotokana na kilimo lazima tuachane na kilimo cha mazoea tuende kwenye kilimo cha kisasa, unapozungumzia kilimo cha kisasa lazima uzungumzie umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo ameonesha ni namna gani anataka kuweka kipaumbele kwenye umwagiliaji. Changamoto inayojitokeza ni fedha. Kwa kuwa, Mawaziri wa kisekta wameshaonesha mipango yao leo tunachotaka ni kushauri Wizara ya Fedha, na jambo hili kama kweli tunategemea kilimo itakuwa ni mbadala wa ajira Tanzania, lazima tuwekeze kwenye kilimo, kwa sababu Waziri ameshaonesha mipango basi Wizara ya Fedha mpeni fedha, ili akija hapa tumlaumu yeye kwa suala la usimamizi. Fedha apewe kisha tuje tuangalie usimamizi wake ukoje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Ziwa Tanganyika tunapakana na nchi tatu. Tunapakana na Congo, Burundi na Rwanda. Ziwa Tanganyika pamoj ana kujenga bandari, bandari Kigoma, bandari Kabwe, bandari Kalema, Kipili na Kasanga, lakini cha ajabu kwamba Serikali tulikwenda kuweka fedha tulikuwa tunataka ku–achieve nini? Kama Ziwa Tanganyika halina usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo kama fedha itawekezwa kwenye kilimo, wakulima wale wa eneo la Ziwa Tanganyika hawatalima mpunga mara moja kwa mwaka, watalima zaidi ya mara moja. Wakilima zaidi ya mara moja bandari zipo, kinachotakiwa ni usafiri wapeleke nchi za jirani. Tunakwama wapi? Haya mambo yanasikitisha, yanahuzunisha sana na ndiyo maana anasema siyo kwamba wote tunakataa mikopo ya Serikali, tunakopa kuwekeza kwenye vitu gani? Vina manufaa gani kwa Watanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo kama tumeamua kuwekeza, hivi leo kweli hatujui faida ya kuwekeza kwenye Ziwa Tanganyika kuweka usafiri, tukateka biashara upande wa Congo, tunasubiri nini kwenye jambo hilo? Miaka mitatu Mheshimiwa Waziri, Waziri wa uchukuzi ameshaonesha nia, miaka mitatu anatenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa meli, miaka mitatu tunasoma tu hapa lakini hakuna fedha inakwenda. Kwa hiyo, changamoto siyo kutenga, changamoto ni kupeleka fedha. Niwaombe Waziri na Naibu wako, kwa kuwa kwenye Serikali kumekuwa na changamoto kubwa, yaani leo kusoma hapa kwamba tumetenga ni jambo moja, kupeleka jambo kubwa zaidi ambalo linahitaji msukumo ambao siyo wa kawaida, baada ya kupeleka kuna changamoto pia ya usimamizi wa huko mlikopeleka, mradi ukamilike kwa wakati lakini usimamiwe kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Ziwa Tanganyika hilo tunazungumzia suala la maji yaani ni kilio cha siku zote, miaka yote, shida ya maji wakati tuna Ziwa Kuu, Ziwa Tanganyika. Waziri wa Maji amesema anatamani na yeye kwa sababu suluhisho ni maji kutoa Ziwa Tanganyika, Mheshimiwa Waziri hiyo mikopo yako peleka huko sasa. Wakitoa maji Ziwa Tanganyika tunazungumzia sasa kwamba kutakuwa na manufaa kwa wakulima hawa. Hayo maji yatatumika kwenye matumizi ya binadamu, kwenye viwanda pamoja na kilimo. Mpe fedha Waziri wa Maji akamilishe mradi wa maji na sisi tukikaa sasa tuseme kwenye Ziwa Tanganyika tumetumia ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ndani ya Ziwa Tanganyika kuna samaki wa mapambo. Wale Samaki wanavyochukuliwa hata wananchi hawajui huko wanakokwenda wanatumiwaje hao samaki, ni kwa sababu hatujawekeza kikamilifu. Lakini shida siyo masikini kwa hiyo lazima tu–change mindset. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo nataka nizungumze changamoto kubwa ya tozo ambazo ni kero kwa Watanzania. Hizi tozo nataka nianze na kwenye simu. Kwenye suala la miamala ya simu nazungumzia Mtanzania wa kawaida kabisa, achana na data huyu tu anayefanya miamala ambaye yule mama ameuza mahindi shambani, anataka kumtumia mtoto wake fedha anasoma UDOM na yeye anataka mtoto wake asome Chuo Kikuu. Anapotuma na yeye changamoto, mtoto mwenyewe anayepokea changamoto, yule amefanya biashara gani? Tumeona hapa mmeonesha namna ambavyo mtakwenda kusaidia yule anayetuma asikatwe angalau yule anayepokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa umesema tutasimamia usajili, tunajua kabisa kwamba huyu ni mwanafunzi huyu siyo mwanafunzi, kwani tulisajili kwa ajili ya nini? si mnajua lakini ile miamala inavyofanyika tunajua kwamba huyu siyo mfanyabiashara. Yale makato mwongozo utolewe na Serikali, kwa sababu hili suala ni kutengeneza gharama kwa mtanzania wa kawaida kabisa ambayo haiana sababu. Na hili jambo tuangalie pia mpaka kwenye sim–banking. Hivi akatwe na benki lakini akatwe tena na kampuni ya simu, kwa nini msikae na haya makampuni angalau makato yawe ya aina moja? Kwa nini akatwe mara mbili huyu mtumiaji wa simu? Hata kama mnataka kukusanya lazima tujue tukusanye bila kumuachia alama mbaya huyu mtanzania ambaye tunatamani kesho tena aendelee kutumia simu na aendelee kuona umuhimu wa hiyo miamala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni vizuri Mheshimiwa Waziri na Kamati yako kaeni chini mpitie upya Sheria za Kodi pamoja na kanuni zake zina changamoto nyingi sana. Hakuna sababu ya kugombana na wafanyabiashara, kaeni nao wanafahamu umuhimu wa kodi lakini waone matokeo ya kodi wanazozilipa moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine nataka kuzungumzia hizi gari za abiria. Gari za abiria na wao wamekuwa na changamoto nyingi, hizi gari za abiria wanapokwenda stand lazima wasimaishwe. Hivi si zinajulikana trip kwamba wanavyoingia kwenye zile stand kwa siku wanaingia mara ngapi. Kwa nini isipigwe hesabu kwa mwaka wanaingia siku ngapi gharama yake ni kiasi gani ili wakajumulisha yale mahesabu, kuondoa ususmbufu wa abiria kila wakati kusimamishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie jambo lingine la kodi za forodha. Unajua inafikia mahali Halmasahuri nao wanatamani kwamba angalau wapate chochote, sasa yale matamanio yao wanatunga Sheria Ndogo ambazo zinaenda kunyume kabisa na Sheria Mama. Matokeo yake tunaenda kufifisha hayo maeneo ambayo tulitegemea itakuwa ni mwarobaini, kwa hiyo ni vizuri na huko mkaangalia hata kama Halmashauri wanakuwa na kanuni zao, zile Sheria Ndogo ambazo wanakuwa na matamanio ya kukusanya wapitie kwanza Sheria Mama pamoja na kusudio lao la kutaka kukusanya ili wasiondoe hili suala ambalo lipo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sana Mheshimiwa Waziri akiwa anakaa mara kwa mara na cabinet yake kupitia hizi changamoto ambazo hazina sababu ya kuleta hizi kelele kama ilivyotokea Kariakoo. Ile uliyoiona ni ya Karikaoo lakini ukiangalia nchi nzima kuna changamoto kubwa sana. Changamoto zinatokana na nini inawezekana sheria ikawa haina changamoto kubwa lakini zile kanuni zina changamoto nyingi sana. Pia shida inakuwepo kwenye usimamizi ambapo usimamizi huu uko chini yako lazima na wewe uliangalie Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine natamani kuzungumzia suala la sekta ya uzalishaji nimezungumzia upande wa kilimo lakini na upande wa maji. Nimeona hapa kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri mmetenga fedha kwa ajili ya Katiba mpya. Mmetenga bilioni tano, ni jambo jema nawashukuru mmetenga, lakini kwa sababu Serikali yetu kutenga ni jambo moja na kupeleka fedha ni jambo jingine. Tunaomba fedha hiyo iende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba mpya tunayoisema leo kuna mambo mengi tunarekebisha hapa ndani lakini kuna mengine ambayo tutarekebisha hii Katiba iliyopo mpaka lini? Hii Katiba ni ya manufaa yetu sisi sote. Hatusemi Katiba hii itaenda kuwasaidia Vyama vya Siasa peke yake, Hapana! Ndiyo maana Katiba tunasema ni ya nchi yetu, imekuwa ya muda mrefu lakini itaendana na mazingira ya sasa. Nikuombe Mheshimiwa Waziri upeleke fedha, mchakato uanze, utakaozingatia utaratibu na maoni watakayoyatoa Watanzania ili yale yatakayopitishwa yaweze kutekelezeka na Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho Waziri wa Maliasili na Utalii changamoto aliyonayo sasa hivi ni kuhusu hawa Wanyama, yaani ninapoamka asubuhi unasikia habari ya tembo. Leo tu asubuhi ninapokuja hapa Bungeni tembo wamekwenda mpaka kijijini. Mheshimiwa Waziri, tembo si tunawataka na wananchi tunawataka. Peleka fedha zijengwe fence kuzuia wale wanyama wakali ili waendelee kubaki na wanufaishe Taifa. Hayo ni maeneo muhimu kama tembo tunawapenda na binadamu tunawapenda. Upeleke fedha za kifuta jasho pamoja na kifuta machozi ili hawa wananchi ambao leo nimezungumza hapa alipokuwa anawasilisha Waziri. Haiwezekani mkulima ambaye amelima ekari zaidi ya tano, heka moja tembo wakila analipwa shilingi 25,000! Ni mambo ya kikoloni, ni mambo ya zamani, hayana maana yoyote tukitoa leo 25,000 huwezi kwenda kununua chochote. Ahsante sana. (Makofi)