Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niwe miongoni mwa wachangiaji wa leo. Naomba kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na timu ya wataalam wake; na wewe Mheshimiwa Mwenyekiti ni shuhuda; kwa jinsi ambavyo wamekuwa wasikivu wakisikiliza maoni ya Kamati ya Bajeti lakini pia maoni ambayo yaliletwa na wadau, Mheshimiwa Waziri hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usio pingika kwamba sheria ikitungwa Bungeni, pale inapoenda kutekelezwa vizuri mafanikio yake yanakuwa ya kwetu sisi sote. Hivi karibuni imezuka tabia kwa wafanyakazi wa Serikali hasa wa TRA pale ambapo wanapokwenda kutekeleza Sheria ambayo sisi tumeitunga vizuri, wanapoenda kufata kanuni katika kutoza kodi likija baya inakuja upande wa Kamati ya Bajeti lakini pia na Bunge kwamba ni Bunge ndilo ambalo limetunga Sheria hii. Si vizuri na inakatisha tamaa, likiwa zuri la kwetu na likiharibika lote liwe la kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza kipekee Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na ubunifu mkubwa ambao ameufanya, kwa kuja na ubunifu mkubwa sana wa kuja na filamu ya Royal Tour. Filamu hii inaleta watalii wengi sana na tumeambiwa wataendelea kumiminika kwa kadri siku zinavyokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba sisi kama Taifa, tukilinganisha na majirani zetu tunaupungufu wa mahoteli na vitanda. Lakini katika bajeti ambayo imeenda kusomwa na Mheshimiwa Waziri sijaona hatua za makusudi ambazo zinatakwenda kuchochea ujenzi wa hoteli kwa ajili ya watalii ambao tunatarajia watakuja. Ni vizuri wakati mnaenda kuhitimisha muje na vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shuhuda, kuna kipindi ambacho tulikutana na benki, inaonekana katika sekta hii pamoja na kuonesha kwamba kuna appetite lakini benki haziko tayari kukopesha watu wanaokwenda kuwekeza katika industry hii. Ni vizuri Serikali mkajiuliza, kwamba, pamoja na fursa iliyopo ya kwenda kutengeneza fedha kwa nini benki haziko tayari kupeleka kwenye maeneo hayo? Inawezekana ni sheria zetu, sheria za ardhi. Je, mtu anapokuja kutoka nje anapotaka kuleta mtaji wake, sheria zetu za ardhi zinasemaje? Atakuwa tayari kuwekeza? Kwa hiyo ni vizuri mkalitazama kwa mapana yake ili hao watalii ambao Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ya kuwaleta iende kuwa na manufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie eneo lingine la pili, kwenye kilimo. Ipo taarifa ambayo na mimi naiunga mkono, Serikali imetangaza kwamba lazima kuwe na control kuhakikisha kwamba chakula hakiuzwi kiholela, ni jambo jema. Lakini ni vizuri Serikali mkafanya tathmini; bei ambayo mwananchi wa Kalambo, bei ambayo mwananchi wa Namtumbo alikuwa akiipata kabla ya tangazo hili gunia lilikuwa limefika elfu sabini, leo hii tunavyoongea gunia liko shilingi elfu arobaini, shilingi elfu thelathini na tano. Je, kwa haya yanayofanywa na Serikali yanatoa motisha kwa mwananchi mwaka unaofata kwenda shambani kwenda kulima ilhali anajua kwamba kitu anachoenda kulima hakina maslahi kwake yeye.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI:Mheshimiwa Kandege kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Getere.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa hali halisi ya nchi yetu kuna maeneo bei ya gunia inafika laki na ishirini mpaka laki moja kwa hiyo pale wanapouza elfu arobaini wapeleke Mkoa wa Mara hasa kwenye Jimbo langu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kandege taarifa hiyo unaipokea?

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea wananchi wa Jimbo la Kalambo ambao alikuwa anapata gunia kwa shilingi elfu sabini leo ukimwambia apate elfu thelathini hatakuwa motivated kulima mwaka mwingine. Kwa hiyo ni vizuri Serikali wakajiuliza na kujibu maswali yafuatayo;Pale ambapo wamesema kwamba mahindi yasipelekwe nje, Je, wanafedha ya kutosha kununua mahindi katika vijiji vyote? Je, wananunua kwa bei gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alishawahi kusema, ni vizuri ukiyasema uyakumbuke. Ulisema kwamba si kazi ya mwananchi kutunza mahindi kwa ajili ya Serikali. Kwa hiyo lile jambo lilokuwa zuri kwa ajili ya mwananchi naamini bado haijabadilika. Serikali mjipange…

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kandege kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo.

TAARIFA

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mkulima Kandege na wakulima wote wa nchi hii. Serikali imezuia kupeleka mazao ya kilimo nje ya nchi kinyume na utaratibu. Anayefuata utaratibu uliowekwa na Serikali atapata export permit, ilimradi awe na business license awe na tin, short of that hatutaruhusu mazao ya kilimo kutoka nje ya nchi kinyume na utaratibu.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Kandege unaipokea Taarifa?

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa na ni vizuri wananchi mkajua kwamba Serikali haijazuia mahindi kwenda nje na msubiri bei zitapanda muuze katika hali ambayo itakuwa na tija katika kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza eneo hilo, na bahati nzuri napata response nzuri kutoka Serikalini kwa hiyo wananchi wa Kalambo msubiri msiwe na haraka ya kuuza mahindi, mtauza mahindi katika bei ile ambayo inaleta tija ili na mwakani mrudi kwenda kulima mkijua kwamba kilimo ni tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende eneo jingine la pili. Teknolojia haiongopi na namba haziongopi. Ni ukweli usipingika kwamba Serikali kwa kutofanya maamuzi kwa wakati wakati mwingine wanajikosesha fedha wao wenyewe. Kuna utaratibu ambao ulikuwa umeanzishwa ambao ulikuwepo tangu zamani juu ya kuwepo kwa bahatinasibu ya Taifa. Jambo hili tangu mchakato wake umeanza ni muda mrefu Serikali inajikosesha mapato. Hebu mtuambie mchakato wa kuianzisha umefikia wapi? Kwa sababu tusipokuwa na bahatinasibu ya Taifa ni kwamba watu wetu wanakwenda kucheza off show hakuna chochote ambacho kinapatikana ndani ya Serikali na sisi tungetaka fedha zipatikane ili mwananchi wa Kalamba afaidike na kujengwa kwa madarasa na kupelekwa lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kama hiyo haitoshi kama ambavyo nimesema namba haziongopi; wakati walipokuja wenzetu wa Sport Betting waliiambia Serikali kwamba kwa kushusha kodi kwa mwananchi ambaye ana win tafsiri yake itaenda kuongeza watu wanaoshiriki na wananchi watajua kwamba wanapata fedha. Ni ukweli usiopingika kwamba hadi leo tunavyoongea kufika mwezi Mei Serikali imeweza kuvuka malengo kwa asilimia 12, na kufika mwezi Juni hakika inaweza kufika asilimia 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Serikali ni vizuri mkawasikiliza wadau wawape takwimu, kile wanachoahidi kwamba kinaweza kupatikana kikapatikane na Serikali mwe tayari kukubali matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee zao la pamba. Nilimsikia Mbunge anayetoka eneo ambalo pamba inalimwa, lakini ni ukweli usiopingika kwamba sisi kama Taifa tunategemea zao hili kwa ajili ya kuingiza fedha za kigeni. Ni ukweli usiopingika pia kwamba pamoja na kutegemea zao hili haina tija pale ambapo pamba inaenda kuuzwa nje ikiwa haijaongezwa thamani yoyote. Kama Serikali naomba mjiulize na mtoe majibu, kwa nini asilimia 75 ya pamba inakwenda ikiwa pamba ghafi lakini wakati huo tunaambiwa eti kuna viwanda ambavyo vinatengeneza nguo? Tupate majibu, je, nguo hizo ambazo zinatengenezwa ni zile ambazo ni za standard ya leo? Je, vinaanzia kuanzia pamba kuchambua na hadi kuja kutoa nguo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali mkaweka mazingira ya kuhakikisha kwamba Viwanda vinakuwepo vya karne ya 21 ambavyo hakika hata ukienda sehemu ambayo wafanyakazi wanafanya kazi unasema wako katika mazingira yaliyo bora. ni vizuri pia mkatafuta namna ya kuweza kutoa vivutio ambavyo vitasaidia watu waje wajenge viwanda na si kubabaisha kuna viwanda wakati hakuna viwanda kwenye uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Serikali wameliona hili. Watu wetu walikuwa wanataabika juu ya uingizaji wa vitenge, vinakuja vitenge ambavyo vinakuja Tanzania, vinaenda nje ya nchi halafu vinarudi Tanzania tunakuja kuuziwa tena Tanzania…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kandege muda wako umeisha.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)