Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii.
Kwanza kabisa napenda niwapongeze walioandaa hotuba hii, na sisi kuweza kutupatia nafasi kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze na viwanja vya ndege. Ni kweli Serikali imejitahidi kupanga bajeti kwa ajili ya viwanja vya ndege, na tunaomba basi, kwa namna ambavyo mmeweza kupanga, muweze kuvitekeleza, tumekuwa na mipango mingi ambayo hatuiwezi. Napenda kuishukuru Serikali kwa kuweza kutenga kiasi fulani cha fedha kwa kiwanja cha ndege cha Mpanda, mmetenga karibu shilingi milioni 700. Sasa hizi shilingi milioni 700 sijajua zinaenda kutengeneza visima vya mafuta, kuweka taa, ama extension ya zile kilometa mbili. Kwa hiyo, nilikuwa napenda Mheshimiwa Waziri, utakapo kuja uweze kunipatia majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niende kwenye suala moja la daraja langu la Kavuu kwenye Jimbo la Kavuu. Sipendi sana kulaumu napenda niseme litekelezwe. Daraja hili la Kavuu si chini ya miaka nane linapangiwa bajeti. Kila bajeti nikisoma ni shilingi bilioni mbili ambazo sijaziona, kila mwaka naona shilingi bilioni mbili ambazo sijui zinapelekwa wapi. Ninaomba Waziri uniambie daraja hili linakwisha lini? Na ningependa liishe mwaka huu na ninapenda pesa hizo zitakapotoka uniambie ili nizifuatilie daraja hilo niweze kulisimamia mwenyewe naona Serikali imeshindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba kabisa Waziri pesa hizo pindi zinapotoka uniambie ili niweze kuzifuatilia na wakandarasi wa nchini wapo wanaoweza kufanya kazi nzuri, tunaweza tukakuelekeza; wengine wako Mbeya na Sumbawanga, wanafanya kazi vizuri sana, hasa katika mkoa wa Katavi ambao wanaufahamu na udongo wa kule wanaufahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo napenda pia nijue kiwango cha lami kitajengwa lini kutoka barabara ya Kibaoni mpaka Kilamatumu kupitia Inyonga, kutoka Inyonga mpaka Ilunde. Ninaongea haya akina mama, watoto, wagonjwa wana teseka kweli kweli; hawafiki maeneo ya matibabu kutokana na ubovu wa barabara. Hakuna magari kwa sababu maeneo yale karibu eneo kubwa ni mbuga na ni hatari kwa kina mama kwa kupanda pikipiki na magari kwa sababu tu ya barabara.
Ninaomba barabara hizo zitengenezwe ili wananchi wa maeneo hayo nao waweze kupata ahueni hasa katika suala zima la kufuata matibabu; ukizingatia kwamba mkoa wetu bado ni mpya na hauna hospitali ya Mkoa wala ya Rufaa, ni lazima twende Bugando, Tabora ama Mbeya. Kwa hiyo lazima tupite hizo barabara na tunapita kwa shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba sana ili na sisi tuweze kupata matunda ya nchi yetu kwa sababu tunalipa kodi kama watu wengine wanavyoishi mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nije kwenye suala la bandari, naongelea gati la Karema. Gati hili limekuwa ni wimbo, meli ya MV Liemba imetoka kuongelewa hapa, katika bajeti iliyopita ukurasa wa 38 wa kitabu kile mmeongelea ile meli sasa inawekwa kwenye makumbusho, lakini leo humu ninasoma mnasema mmekubaliana na Ujerumani kwamba mnakuja kuitengeneza. Kipi ni kipi wananchi wale wachukue, kwamba meli ile ni nzima ama ni mbovu inafanyiwa marekebisho ama inawekwa makumbusho inaletwa meli nyingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini tuweke maisha ya Wananchi wa Ikola, Karema, Kala, Kirando, Kabwe mpaka Kigoma tuyaweke rehani kwa ajili ya meli hii? Kama ni mbovu meli hiyo wekeni, leteni meli mpya wananchi wanataka maendeleo. Ile ni corridor ya biashara, tunaenda Congo, Burundi, Zambia, kama mnaona tatizo kwamba meli kutoka Mpanda mpaka Karema inashindikana, tukarabati barabara/tutengeneze barabara ya kwenda Kasesha, Karema mpaka Kasanga Port ili tuweze kupata na kufanya biashara na wananchi wa mkoa wa Katavi na Rukwa waweze kuuza mazao yao kwa urahisi, ili waweze kujiongezea kipato na waweze kukuza uchumi wao kama Serikali inavyosema, kutoka kima cha chini kwenda kima cha kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyoMheshimiwa Waziri nafikiri unanisikia, unanielewa, umetoka Katavi juzi na umeona hali halisi ya kule naomba utekeleze hilo hasa daraja la Kavuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja barabara ya kutoka Kibaoni – Kasansa – Buze – Kiliamatundu na ya Majimoto – Inyonga mpaka Ilunde, ninaomba majibu ya barabara hizo. Tumekuwa tukisema kila siku, na ninapenda nirudie kama wenzangu waliokwishatangulia kusema kuwa hatuna sababu ya kusema tunasubiri barabara fulani ipandishwe daraja, tunapadisha daraja kutoka lipi kwenda lipi? Wananchi ni wale wale, wa level ile ile, haki yao ni sawa. Wote tuna haki ya kupata barabara bora, maji salama na huduma za msingi kwa wakati mmoja bila kujali huyu ni wa kijijini au wa mjini.
Ninaomba sasa kama Sheria hiyo ya Bodi ya Barabara au ya kwenu, inaleta matatizo tunaomba muilete hapa, ile siyo msahafu wala biblia kwamba haibadiliki. Leteni hapa tutafanyia marekebisho watu waweze kuapata maendeleo sawa kwa sawa na mgawanyo uwe sawa kwa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja barabara ya kutoka Kawajense – Ugala – Kaliua mpaka Kahama. Barabara hii tumekuwa tukiiongelea sana sambamba na ujenzi wa daraja la Ugala, tumekuwa tukiiongelea sana, itamsaidia mwananchi kutoa mazao yake kutoka Mbeya, Sumbawanga, Katavi, Kahama na hatimaye kwenda Musoma na na hata kwenda Darfur wanakopigana kila siku hawana chakula. Tumekuwa tukiongelea umuhimu wa barabara hii; na barabara hii ilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2005 na haijatengewa hata hela ya upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli sipendi sana kuilaumu Serikali lakini tufike mahali tuwe realistic, kila siku tunaongea hapa haipendezi mtu kila siku ukalisema neon moja, ukisema neno moja kila siku unaumia. Sasa tusianze kupeana pressure humu maisha ni mazuri hata kama magumu. Lakini tunahitaji tunapoongea tunajua tunaongea na Serikali ni watu wazima, wenye akili timamu, tusikilize shida za wananchi na zitekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongelea suala la reli ya kati, reli ya kati imeongelewa sana, kwa kweli itakuwa ni aibu kama kila siku tutakuwa tunaongelea suala hili ifike mahali tuchukue maamuzi tufanye kwa vitendo sasa. Matokeo makubwa sasa si pesa, ni pale unapokuwa na tatizo na ukali-solve tatizo mara moja, hayo ndiyo matokeo makubwa na si pesa kutoka sehemu nyingine. Niwaombeni sana tatizo la reli tunalo, sasa ni wakati muafaka wa kulitatua. Tutakapo litatua ndipo tutakapokuwa tumefika kwenye matokeo makubwa sasa.
Kwa hiyo, niwaombe kabisa na Serikali inisikilize na standard gauge iwe ni kipaumbele, si suala la kung‟oa mataruma ya reli ya Tura mkayapeleka Katumba ama mkapeleka Mpanda hapana, tunataka reli sawa sawa na maendeleo ya sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongelea suala la kurudisha, vinaitwa nini vile?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Not viberenge, magenge. Tulisema yale magenge yatasaidia sana katika kulinda reli zetu na pia katika kuongeza ajira. Sasa mimi sielewi kwa nini yaliondolewa. Ndiyo maana mnaona kila wakati yale mataruma yanang‟olewa na wananchi kwenda kuuza chuma chakavu, tunaona kwenye tv magari yanavyobeba. Ni vyema sasa mkafikiria mahali na mkafika wakati wa kurudisha; sambamba na kwenye barabara tuliposema kwamba turudishe Public Work Department kwa ajili ya matengenezo ya kila mara ya barabara, kwa ajili ya kuhakikisha barabara zetu zinapitika wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niongelee suala la mitandao au suala la mawasiliano. Ninashukuru sana Serikali yangu kwa kutupatia mitandao hasa vijijini kupitia Halotel, hawa ndugu zetu wa Vietnam, wanafanya vizuri nashukuru. Tatizo langu kubwa na hawa watu ni namna wanavyotoza zile tozo…
Haiwezekani wakatoa kwenye mnara shilingi 30,000 kwa mwezi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kengele ya kwanza. Mimi hilo nalikataa ninaomba kabisa Serikali iangalie namna itakavyo toza hizo tozo tozo hizo…
Haiwezekani shilingi 30,000 kwa mwezi huo ni uonevu na ni wizi hata kama wanapewa huduma wanafanya biashara...
Wapewe hela kufuatana na huduma wanayotoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.