Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu. Kwanza nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea miradi mingi katika maeneo mengi sisi wananchi wa Wilaya ya Kakonko, tunamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nipongeze Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri. Nipongeze kwa bajeti nzuri ambayo inakwenda kuwagusa wananchi wetu wa kawaida hasa kwa kuweza kutoa mkopo kwa wanafunzi katika vyuo mbalimbali hasa vyuo vya kati. Tunaipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jicho sasa linapaswa lipelekwe kwenye vyuo vya kati hasa wale wanaosomea elimu amali ambao wanaweza wakawa ni wale wanaosomea useremala, wanaosomea ushoni, wanaosoma uuguzi na kadhalika; hawa wanasomea kazi. Tunategemea kwamba ndani ya muda mfupi wakikopeshwa watamaliza masomo yao na wataweza kujiajiri na hivi ni rahisi kwao kurudisha fedha ambazo Serikali imewakopesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi katika eneo la kuchangia kwenye bajeti. Ili bajeti iwe endelevu lazima kuwe na vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kui-support bajeti hii, na maeneo ambayo yanapaswa kusupotiwa (to be supported) ni pamoja na kuongeza vipato ambavyo vinatokana na wananchi wanaoingia na kutoka kwenye mipaka ya nchi yetu. Upo mpaka kama wa Mlongo katika Wilaya ya Kyerwa, upo mpaka wa Mabamba katika Wilaya ya Kibondo, upo mpaka wa Mnanila katika Wilaya ya Buhigwe lakini kwa Wilaya ya Kakonko tunao mpaka wa Mhange. Mpaka ule nilisha mwambia hata Mheshimiwa Waziri kwamba hebu tuwekeze katika mpaka wa Mhange, tupeleke wataalam tuweke forodha pale. Nina uhakika kupitia mpaka ule Serikali itaweza kupata fedha.

MHE. CONDESTER M. SCHWALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Aloyce Kamamba, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Condester Sichwale.

TAARIFA

MHE. CONDESTER M. SCHWALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nataka kumuongezea taarifa mzungumzaji anayeongea kwamba ni kweli mipaka mingi ambayo tumeona kuna mageti ya forodha ndiyo imekuwa ni chanzo kikubwa sana cha mapato. Mfano Boda ya Tunduma, Namanga, Holili, sehemu zote hizi na nchi yetu imebahatika kuwa na mipaka mingi sana, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge anachokiongea ni sahihi kama eneo lake kuna mpaka akiongezewa geti la forodha kitakuwa ni chanzo kingine kizuri sana cha mapato kwenye nchi yetu.

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Aloyce taarifa unaipokea?

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ninaipokea na ninaomba basi Mheshimiwa Waziri aweze kutuboreshea mpaka wetu wa Mhange kwa kupeleka wataalam, kwa kupeleka majengo pale na tupelekewe fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Kakonko kwenda Kinonko, kwenda Gwarama mpaka mpaka wa Mhange. Nina uhakika natumia maneno mengi kumwomba Mheshimiwa Waziri lakini akichukua ushauri huu iko siku atatumia muda mwingi kushukuru ushauri huu. Naomba sana ushauri huu uchukuliwe, waboreshe mipaka yetu nina hakika kwamba matunda yanaweza yakapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo ahadi za viongozi wetu, zikiwepo ahadi za Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakiuliza katika maswali ya msingi lakini muda mwingine katika kuchangia kwao. Ahadi ni deni. Zipo ahadi ambazo Serikali imeweka kwa wananchi wetu katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Kakonko. Katika mji wa Kakonko tuliahidiwa kilometa tatu na Hayati Rais Magufuli, tumejengewa kilometa 0.63, tuombe kilometa zilizobaki, kilometa mbili na ushee hivi zikamilishwe ili mji wetu wa Kakonko nao uweze kuwa na hali nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ambayo imewekwa mwaka huu kuna ujenzi wa Hospitali ya Kanda katika Mkoa wa Kigoma na vile vile kuna ujenzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Muhimbili. Nina uhakika fedha zikipelekwa na ujenzi ukafanyika, wananchi wa nchi jirani za Burundi, Congo, Zambia wataweza kupata matibabu katika hospitali hizo. Kwa hiyo pamoja na kwamba tutakuwa tunatoa huduma ya matibabu lakini itakuwa ni chanzo cha fedha kwa nchi yetu. Niombe sana fedha zitengwe, ardhi Kigoma tunayo ili ujenzi huo wa hospiatli ya rufaa pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki cha Muhimbili, ujenzi uweze kuanza katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma tuna Ziwa Tanganyika lakini katika ziwa letu ukiangalia maziwa mengine kuanzia Bahari ya Hindi meli zipo, Ziwa Victoria meli zipo, Ziwa Nyasa meli zipo lakini Ziwa Tanganyika ni tatizo. Usafiri katika Ziwa Tanganyika ni tatizo, meli hatuna. Tuna miaka mitatu fedha zinatengwa lakini fedha haziendi. Tuombe katika bajeti ya mwaka huu kama ni kuteseka Mkoa wa Rukwa, kama ni kuteseka Mkoa wa Katavi, tumeteseka kwa muda mrefu sana. Tuombe kwenye bajeti hii fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa mikoa hiyo mitatu katika ziwa Tanganyika, tuletewe fedha meli ambazo ni za kukarabatiwa zikarabatiwe lakini na meli mpya ziweze kupelekwa katika maeneo hayo ili miji yetu ichangamke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia panapaswa kuwa na boti za kusafirisha abiria kutoka mji wa Kigoma kwenda Katavi huku chini, kutoka Kigoma kwenda katika miji ya Congo, kutoka Kigoma kwenda Burundi. Tukiwa na mchanganyiko wa wananchi wanaotoka na kwenda jirani, wanaotoka jirani kuja katika miji yetu nina uhakika biashara itakuwepo na uchumi wa wananchi wetu utaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo barabara ambazo ni za kuunganisha Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine. Tunashukuru Serikali inaendelea kulifanyia kazi hilo; lakini bado kuna shida ya umaliziaji wa barabara inayounga Kigoma na Katavi pamoja na Kigoma na Rukwa. Kipo pia kipande ambacho kiko katikati ya Kibondo na Kasulu, pale bado pana tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi uliona kwamba kulikuwa na picha inazunguka kwenye mitandao, lakini ule sio udongo wa Kigoma na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amekwishazungumzia hilo. Yote hiyo inatokana na changamoto ambayo tunaipata kwenye barabara. Tuombe, zile fedha ambazo zinapungua na hazijapelekwa kwenye maeneo hayo, zipelekwe na ujenzi uweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma inatengenezwa kuwa ni eneo la uwekezaji katika Kanda ya Magharibi, lakini hatuna uwanja wa ndege ambao unaweza ukaruhusu ndege kuingia na kutoka muda wote. Tuombe Uwanja wetu wa Ndege wa Kigoma upelekewe fedha za kutosha, thamani ambayo inahitajika ikamilishwe ili ujenzi unapokamilika nina hakika tutakuwa na uwezo wa kuwapokea wasafiri kutoka Nchi jirani za Burundi, Congo, Zambia kwa sababu ni rahisi kutokea upande ule wa maeneo yale. Hivyo, Kigoma kama Mkoa utakuwa na nafasi ya kufanya biashara nzuri zaidi na hivyo kuongeza mapato ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru tena kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)