Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru nami kwa kunipatia wasaa niweze kutoa mchango wangu kwenye Bajeti Kuu ya Serikali ya 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la sekta ya uzalishaji na nitaomba nianze na Sekta ya Kilimo; kwenye Sekta ya Kilimo nitazungumuzia uzalishaji wa zao la mafuta ya kula ya alizeti. Mwaka 2021 Serikali ilikuja na mpango mkakati mzuri sana wa kwenda kupunguza ama kuondoa kabisa gharama kubwa tunayoitumia kama nchi ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje. Ikatuletea wananchi mpango wa kwenda kuzalisha zao la alizeti na ikateua mikoa mitatu ya kimkakati ili wananchi wa mikoa hiyo waweze kuzalisha kwa wingi ili tuweze kuona ni namna gani tunakwenda kuondokana na wimbi kubwa la upungufu wa mafuta ya kula ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia iliingia gharama ya kuhakikisha inawapatia wakulima mbegu ambazo zitakwenda kuwasaidia kuzalisha zao hili. Hata hivyo, pamoja na dhamira hii njema ambayo awali ilioneshwa na Serikali, lakini kwa sasa naanza kuiona Serikali ikirudi nyuma kwenye dhamira hii njema waliyokuwa nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamesema mwaka 2022, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa mafuta ya kula aliweka tozo ya asilimia 35, leo anakwenda kupunguza unaweka asilimia 25. Mheshimiwa Waziri, anachokitaka kukipata hapa ni nini? Leo wakulima wa alizeti wa Mkoa wa Singida, Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Simiyu tuna alizeti ya tangu mwaka 2022 ipo, mwaka 2023 tumeanza kuvuna, alizeti iko majumbani mwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali wameamua kupunguza kodi kwenye mafuta ya kula, wazalishaji ama wachakataji wa zao la alizeti wamefunga viwanda, wameamua kuagiza mafuta, wanauza mafuta ambayo yanatoka nje na yana gharama nafuu, ambayo hawatumii umeme na wameondoa wafanyakazi kwenye viwanda. Mwisho wa siku, changamoto tuliyokuwa tunataka kuondokana nayo ya kupunguza wimbi la uingizaji wa mafuta ndani ya nchi tunakwenda kurudi kule kule tulikotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mwananchi waliyempa imani kwamba alime zao la alizeti inayojenga uchumi wa kwake binafsi…

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunti, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cosato Chumi.

TAARIFA

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Kunti kwamba, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 50, katika kuhakikisha kwamba tutakuwa hatupungukiwi na dola, mojawapo ya mikakati ni kuongeza uzalishaji ili kuongeza mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi. Sasa, kwa hili analolisema Mheshimiwa Kunti, maana yake badala ya kuuza nje sisi sasa tunataka tuagize nje zaidi kitu ambacho kama Serikali tutaji–contradict. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Kunti, unapokea taarifa?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono 36. Serikali wakati mwingine wanatuchanganya Watanzania. Leo ninavyozungumza hapa mwaka 2022 gunia la alizeti ni shilingi 27,000 na mwaka 2023 wananiambia ni shilingi 20,000 mpaka shilingi 25,000. Hivi ni mkulima gani tena atalala aote ndoto mwakani aende akalime alizeti? Hivi ni kweli Serikali ndio dhamira yao kwamba tunakwenda kuondokana na hilo wimbi kubwa la uagizaji wa mafuta ndani ya nchi? Mbona tunarudi kule kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri ili tuweze kufikia hilo lengo hii asilimia 25 aliyoiweka tunaomba aiondoe, tena hata hiyo asilimia 35 aliyokuwa ameiweka, safari hii nilikuwa nimekuja aweke asilimia 50 ili wawekezaji wa viwanda vyetu vya hapa ndani waweze kuchukua malighafi zilizoko ndani hapa ili waone akiagiza nje na akichukua za ndani ni heri achukue ndani kuliko nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sio zao la alizeti peke yake, tuna zao la mchikichi ambalo Serikali pia walifanya mkakati, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda Kigoma kuzindua zao la chikichi, wakulima wa Kigoma leo wamelima michikichi, Serikali inaendelea kuondoa kodi kwenye mafuta, wanachotaka ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, achana na mchikichi, tuna pamba. Mimi nimeishi Mwanza, tulikuwa tunatumia mafuta ya pamba, leo mafuta ya pamba hayajulikani yalikofia ni wapi, wakati mbegu za pamba zipo na wakulima Mwanza wanalima pamba? Kwa hiyo, niishauri Serikali Wizara ya Fedha na Wizara za kisekta kwa maana ya Wizara ya Kilimo, waende wakutane wazungumze pamoja wawe kitu kimoja ili wanapokuja hapa wawe wanazungumza lugha moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waziri wa Kilimo anahamasisha watu huko kulima mazao ya kuzalisha mafuta, Waziri wa Fedha anakwenda kuondoa tozo kwenye mafuta. Sasa ni kitu gani hiki wanachofanya? Wanatuchanganya, hatuwaelewi shida yao ni nini? Wazungumze, waje wakiwa na kauli moja ili tuweze kuokoa Taifa letu kwenye suala zima la uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala zima la mbolea kwenye Sekta hiyo ya Kilimo. Msimu uliopita mbolea ya kupandia ilichelewa sana katika maeneo mengi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, tunaomba mwaka huu fedha itolewe mapema, mbolea ya kupandia ifike mapema ili wakulima wetu waweze kuondokana na adha kubwa ya kuchelewa kulima bila mbolea. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunti kuna taarifa kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mwigulu.

TAARIFA

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri ambao Mheshimiwa Mbunge anachangia na Wabunge wengine wamechangia, nataka nitoe taarifa kwamba, tunapokea maoni yanayotuelekeza tupandishe kodi, lakini nilichotaka kutoa taarifa ni kwamba sio kwamba tumeshusha. Kwenye mafuta tumebakiza kodi iliyokuwepo mwaka 2022, kwa maana hiyo kwa kuwa maoni ya Wabunge tupandishe sisi tunalipokea hilo. Hata hivyo, tulibakiza kama ilivyokuwa mwaka 2022 kwa ajili ya kukabiliana na gharama za maisha. Kwa hiyo, kwa kuwa maoni ni kwamba tupandishe tumelipokea, lakini sio kwamba tumeshusha. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Kunti, unaipokea taarifa?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba azingatie hilo. Ni kweli apandishe ili viwanda vyetu nchini viweze kufanya kazi, kodi iweze kulipwa hapa ndani ya nchi ili vijana wetu na Watanzania wenzetu waweze kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia suala la mbolea. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri, fedha itoke mapema ili tuweze kuagiza mbolea, iletwe wakati wa msimu wa kupandia kwa ile mikoa inayopanda mapema, waweze kupata mbolea ya kupandia kuliko misimu hii ya nyuma iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie pia tozo ya shilingi 100 kwenye lita ya petrol panoja na diesel. Tuna kama miezi kadhaa huku nyuma ambapo Serikali iliamua kuweka ruzuku kwenye mafuta diesel pamoja na petrol kutokana na wimbi kubwa la Vita ya Ukraine. Mheshimiwa Waziri, sasa naona hapa ametuletea ongezeko la tozo ya shilingi 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa unapoongeza kodi kwenye mafuta ya diesel na petrol unapandisha nauli za usafiri, lakini gharama za vyakula pia zitapanda na kila kitu nchini kitapanda. Sasa namuuliza Mheshimiwa Waziri, hivi ni kweli tumekosa vyanzo vingine vyote vilivyopo mpaka twende tena kwenye mafuta ambayo miezi michache huko nyuma tumeweka zaidi ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya kwenda kupunguza makali ya maisha kwa wananchi wetu? Hiki kitu anachokifanya Waziri hapa kinakwenda kuleta maisha magumu zaidi kwa wananchi wetu kwa sababu kila kitu kitapanda kutokana na suala zima la ongezeko la mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa haraka haraka dakika zangu zinakwenda. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna kodi ya shilingi 1,000 kwenye mfuko wa cement. Ujenzi ni gharama kubwa sana, bati gharama, nondo gharama, mchanga gharama, leo tena na cement wanaendelea kuongeza. Mheshimiwa Mwigulu, hahitaji wananchi wake wa pale Iramba wenye nyumba za udongo full suit chini na juu waweze kuwa na nyumba zenye matofari mazuri ya block waweze kuishi kwenye maisha mazuri anakwenda kuongeza tena kodi kwenye cement, kwenye nondo huku hapakamatiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe kama alivyoridhia kwenye suala zima la tozo ya mafuta, halikadhalika kwenye hili suala la tozo ya cement ya shilingi 1,000 kwa kila mfuko aende akaiondoe ili cement iweze kushuka na tuweze kupata nyumba bora kwa Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunti, ahsante sana muda wako umekwisha, nakushukuru sana.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)