Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa nami kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nimesoma Bajeti ya Serikali, nimeona kuna mambo mengi mazuri, hongera sana Mheshimiwa Waziri. Naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia tozo ya Shilingi 100/= kwenye mafuta. Nadhani tunapoweka tozo kwenye mafuta, ina madhara makubwa kwenye uchumi kwa sababu inakwenda kwenye usafirishaji na itasababisha mpasuko, kupanda gharama kwenye sekta nyingine za uchumi. Nashauri, tuna mitandao ya kijamii; Instagram au tuseme social media, tungeangalia huko tukaiepeleka kule kwa sababu unapoipeleka kwenye social media haina madhara makubwa kama ambavyo tumependekeza kuipeleka kwenye mafuta. Huo ni ushauri wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye kilimo. Wachangiaji wengi wamesema na ndivyo hali ilivyo, kilimo kinahusisha watu wengi Tanzania, hasa wenye kipato cha chini. Tunao Mradi wa BBT, lakini huku kwetu tunakotoka tunalima zao la kahawa, ndiyo zao kubwa sana, lakini ni zao ambalo linaiingizia kipato kikubwa nchi hii. Ukiangalia wakulima ambao wanachangia pato la Taifa kupitia zao la kahawa, ni wakulima wadogo wadogo wenye mashamba madogo madogo; ekari moja, nusa ekari na ndio hao wanaochangia uzalishaji wa kahawa hasa Mkoa wa Kagera. Mkoa wa Kagera tunazalisha zaidi ya tani 40,000 na ndiyo hizi tunakwenda kuuza nchi za nje na kutuletea fedha za kigeni, lakini ukiangalia mashamba ya wakulima, yanatia hofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwenye bajeti hii tuangalie jinsi ya kuongeza uzalishaji wa kahawa kwa kuyahudumia haya mashamba madogo madogo ya wakulima wadogo wadogo, ambao huwa wanawasomesha watoto wao na kutunza familia zao. Haya mashamba tukiyapatia kipaumbele, tukahakikisha kwamba wanapewa mbolea na ruzuku kuhakikisha kwamba haya mashamba yanahudumiwa; na ndiyo yanaweza kutoa kwenye mauzo ya kahawa ambapo mwaka 2022 tulipata shilingi bilioni 240 tukaenda mpaka shilingi bilioni labda 500 tukaanza kushindana na jirani zetu Uganda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Uganda na Tanzania, pamoja na kwamba Tanzania ni nchi kubwa, lakini bado mauzo yetu ya nje ni kidogo. Hili ni eneo ambalo tunaweza tukapata fedha nyingi kutokana na mauzo ya kahawa. Naomba tulifanyie kazi. Ila hatuwezi kulifanyia kazi hivi hivi, lazima tuangalie na kiwango gani cha kahawa tunauza nje ambacho bila kuongezea thamani. Tuna viwanda vidogo vidogo. Kwa mfano, kwenye wilaya yangu pale, vipo viwanda ambavyo vinaongeza thamani zao la kahawa, lakini hatuvipatii kipaumbele kuongeza kiwango cha kahawa ambacho wanakifanyia kazi na kuki-process ili tuuze nje zao ambalo tumeshaliongezea thamani. Kahawa nyingi tunaiuza kama raw material.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo, pale Kagera tuna kiwanda kikubwa cha TANICA. Pamoja na kwamba Mkoa wa Kagera tunazalisha zaidi ya tani 40,000, lakini kiwango ambacho kiwanda chetu cha TANICA kinaweza ku-process ni tani 1,500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, mwaka huu kupitia Bajeti ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri ameahidi kutupatia Shilingi bilioni 8.7 ili kukipatia kiwanda hiki mtaji wa uendeshaji, lakini kukipatia mtaji wa uendeshaji pekee yake, haiongezi lolote. Napendekeza kiwanda hiki tukipatie mtaji wa kuboresha mitambo yake, kwani kina mitambo ambayo imepitwa na wakati, teknolojia wanayoitumia inasababisha kupoteza kahawa nyingi. Ndiyo maana mauzo yetu ya nje kwa kahawa ambayo imeshakuwa processed ni madogo mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile pamoja na kwamba ni madogo, ukiangalia bei ya kilo moja ambayo inazalishwa na TANICA, kwenye soko inauzwa dola 8.5 wakati kahawa inayotoka nje kwa kilo moja hiyo hiyo inauzwa dola nne. Sasa ukiangalia uwiano wa bei, mazao ambayo yanatokana na kiwanda chetu hayawezi kushindana katika soko lolote, kwa sababu tunazalisha kwa gharama kubwa, kwa kuwa teknolojia tunayoitumia ni ya zamani. Kiwanda hiki kilijengwa tangu mwaka 1963 na tangu hapo hatujawahi kukipatia mtaji kuboresha teknolojia. Nadhani ni muda muafaka sasa kukipatia mtaji kiwanda hiki ili tuweze kubadilisha teknolojia kiweze kuzalisha na mazao yake yaweze kushindana na mazao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kahawa ambayo tunaizalisha hapa nchini, hasa ile inayotoka Bukoba ni kahawa nzuri, na ukiipeleka kwenye Soko la Dunia popote, itapata wanunuzi lakini tatizo tulilonalo ni kwamba hatuwezi kushindana kwa sababu hatuna teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiachana na suala la kahawa, wakati tunachangia Wizara ya Ustawi wa Jamii, tuliongelea masuala ya ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii. Tunalo tatizo kubwa sana nchi hii. Wizara yenyewe inaongelea zaidi masuala ya maendeleo ya jamii na masuala ya maendeleo ya jamii ni Wizara zote. Tumesahau Sekta ya Ustawi wa Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Mheshimiwa Waziri anapokuja kutoa hitimisho, tuangalie hili suala la ustawi wa jamii. Tumeongelea vijana wetu kuharibiwa, tumeongelea matatizo ya jamii yanayoendelea, ni kwa sababu tumesahau hii sekta muhimu ya ustawi wa jamii. Tunakimbizana na maendeleo, lakini tumeshindwa kuwekeza vya kutosha kwenye ustawi wa jamii. Napendekeza tuangalie kwenye bajeti yetu, tuone kwa jinsi gani tunaweza kuisaidia Wizara tukajenga rehabilitation centers kwenye majiji makubwa ambako kuna mmomonyoko mkubwa sana wa maadili na vijana wetu wameharibiwa, ili wale ambao wamebainika kwamba wamepata matatizo/wameharibiwa waweze kupelekwa kwenye rehabilitation center na kuwarududisha katika hali yao ya kawaida, waweze kubaki kwenye jamii na kuendelea na uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwenye jimbo langu, naishukuru sana Serikali, imefanya kazi kubwa sana, imetujengea shule, vituo vya afya na hospitali. Kama wachangiaji wengine walivyosema, sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha kwamba Serikali pale ambako imejenga vituo vya afya na hospitali tupatiwe watendaji ili tuweze kupata thamani ya fedha ambayo tumeiwekeza kwenye miundombinu ambayo imejengwa na Serikali kwa fedha nyingi za walipakodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Naishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kuifanya, namshukuru Rais wetu, Wizara na Watendaji wote wa Wizara husika kwa kutuletea bajeti ambayo nadhani itatuvusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)