Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwanza kukushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangoia Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapochangia Bajeti ya Serikali, kwanza kabisa huwa tunafanya mapitio ya Bajeti. Vile vile, ukizingatia mwaka wa fedha uliopita tulipitisha Mradi maarufu sana kama Mradi wa TACTIC kwa ajili ya kujenga miradi mbalimbali kwenye miji 12 ambapo Jiji la Arusha ni mji mmojawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikubaliana kwamba tutaanza kujenga Stendi ya Kisasa, eneo la Bondeni City kuanzia Mwezi wa Saba wa mwaka uliopita. Umepita wa saba tumekwenda mpaka Desemba imepita leo tuko mwezi wa Sita tunakaribia kuumaliza, mpaka leo hata tenda haijatangazwa na bado tunazungumzia bajeti ya mwaka unaofuata. Kwa hiyo, ningefurahi kuona majibu ya Serikali kuhusiana na mpango wa ujenzi wa Stendi ya Jiji la Arusha, kitu ambacho Wanaarusha wanakitamani sana kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kuishulkuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye mpango wa kujenga viwanja vya michezo vya Kimataifa kwenye Mikoa miwili, Mkoa wa Dodoma lakini pia na Mkoa wa Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Arusha ni mahali sahihi kwa sababu hii ni sehemu ya kuunga mkono Royal tour lakini pia ni sehemu ya kuchangia kwenye masuala ya Sports tourism. Hii pia ni kazi nzuri ambayo imefanywa na wenzetu wa Wizara ya michezo kupitia Waziri wetu Dkt. Pindi Chana pamoja na Naibu Waziri, Katibu wetu Mkuu Ndugu yangu Yakubu ambao wanafanya kazi kwa ubunifu mkubwa na wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumepokea mpango huu katika hali nzuri zaidi na tumekwishatenga ardhi ya kutosha kwenye Kata ya Olmoti, Diwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa Kata ya Olmoti wako tayari kabisa kwa ajili ya kuupokea mradi huu kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Arusha tuna hoteli nyingi, tuna mazingira mazuri zaidi, hali ya hewa nzuri na nimeambiwa viwanja hivi vitakwenda kujengwa pia maeneo ya basketball, riadha na hasa ukizingatia kwamba Arusha na hasa maeneo ya Karatu ndio wakimbiaji wengi zaidi wanapatikana katika nchi yetu. Kwa hiyo tunaunga mkono jambo hili na ni imani yangu kwamba consultant ambaye nimeambiwa kwamba atapatikana wakati wowote kuanzia mwezi wa Saba kwa maana ya mwaka wa fedha unaoanza mwezi wa Saba, basi kazi hiyo itakwenda kuanza vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kwenye mapitio upande wa madini, tunaishukuru sana Serikali kwa sababu imekubali kurudisha madini ya tanzanite kwenye masoko yote. Tumeambiwa kwamba mpango huo utaanza kuanzia mwaka wa fedha unaokuja mwezi Julai na kuendelea. Vile vile, kuna mawazo hapa ya kuondoa kodi kwenye minada katika maeneo mbalimbali ambayo itafanyika, tunaunga mkono pia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya salamu hizo za awali, napenda nichangie kwenye masuala yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, wakati Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya ziara Mkoa wa Kagera ilikuwa ni tarehe 9/6/2022, alitoa maelekezo kwa TRA kuhakikisha kwamba hawarudi tena kufukunyua masuala ya kodi zaidi ya mwaka mmoja. Tunaona hapa Waziri wa Fedha amekuja na mapendekezo kwenye Finance Bill, lakini suala hili hajalileta kuliingiza kwenye mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba, ili kumlindia heshima Rais wetu na ili kuendelea kuyatunza maelezo ambayo Mheshimiwa Rais ameyatoa kwenye hadhara, ni vizuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha akatuletea hapa kwenye Finance Bill maelekezo haya yakaingia kwenye Sheria ili TRA wasiingie kwenye mtihani wa kuacha kusimamia sheria. Kama ni vizuri zaidi wakaweka utaratibu mzuri zaidi wa kuhakikisha kwamba wanaingiza kwenye sheria hasa kwenye Muswada wa Fedha wa mwaka huu na Wabunge tutawaunga mkono, kwa sababu ni lazima tumuunge mkono Rais wetu anapoonekana kuwajali wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nimefurahi sana kuona Mheshimiwa Waziri amezungumzia kwamba maeneo ya biashara yasifungwe. Nadhani tamko hilo lingeenda mbali zaidi, sio tu maeneo ya wafanyabiashara, lakini pia wanapoacha kufunga biashara wasifunge pia akaunti za wafanyabiashara. Wanapoacha pia kufunga akaunti za wafanyabiashara, waache pia kwenda kuchukua computer za watu, kuchukua simu za watu kwa wafanyabiashara wa maeneo mbalimbali. Watafute mbinu za kisasa za kuweza kukadiria kodi, kukusanya kodi lakini sio kwenda kuwavamia wafanyabiashara kuchukua vifaa vyao kwa kutumia kigezo cha investigation. Kwa hiyo, nadhani hilo nalo Mheshimiwa Waziri wa Fedha atusaidie kulipa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tumeona pia hapa yamekuja mapendekezo ya kuongeza shilingi 100 kwenye mafuta ya petrol na diesel. Hili wazo mimi binafsi sikubaliani nalo, kwa sababu kwanza ukiangalia kwenye mafuta peke yake kuna kodi kama 22. Kuna kodi ya Wharfage, Railway Development levy 1.5 percent ya CIF, Custom Association Fees, Weight and Measure, TBS, TASAC, EWURA, wako wengi na ziko kodi 22.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye hizo kodi 22 bado kuna kodi kiasi cha shilingi 413 tunaita fuel levy. Hii 413 tayari kodi ya barabara imo humu ndani. Ukiangalia kuna 186 kwa ajili ya TANROADS, kuna shilingi 177 kwa ajili ya TARURA, kuna shilingi 50 kwa ajili ya maji. Kwa hiyo, unaona kabisa barabara zimezingatiwa TANROADS, TARURA wamo humu na maji pia yamo. Kuongeza shilingi 100 nyingine ni kuongeza mzigo kwa mwananchi na kumwongezea mzigo Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi, unapoongeza shilingi 100 mfanyabiashara hana shida, yeye anaongeza ule mzigo, halafu anampelekea mwananchi. Daladala zitataka kupanda bei, mabasi yatapandisha bei na gharama nyingine zitaongezeka kwa sababu itakuwa inagusa pia uzalishaji. Ushauri wangu ni kwamba, tutafute eneo lingine, lakini eneo hili ambalo linakwenda kumgusa moja kwa moja mwananchi kama Serikali tuliangalie vizuri zaidi na hasa ukizingatia tuna changamoto kwenye dola yetu, haijawa stable sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mwaka 2018 dola moja ilikuwa ni sawa na Sh.2,276 kwa wastani, leo dola moja ni sawa na Sh.2,398, maana yake ni nini? Mafuta duniani yanauzwa kwa dola na kama yanauzwa kwa dola yanapokuja Tanzania tukiweka kwa shilingi, peak yake kuna ongezeko la Sh.122. Unaona kabisa mzigo wote huu unaokuja anaubeba Mtanzania. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha zaidi akaongeza ubunifu zaidi kwenye vyanzo lakini sio vile ambavyo vinakwenda kumuumiza mwananchi na Mtanzania wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sambamba pia na kwenye upande wa kupanda kwa bei ya saruji na yenyewe ni vile vile. Tunataka Watanzania wawe na maisha mazuri, tunataka tuondoe nyumba za tembe, lakini mwisho wa siku gharama za ujenzi unaziongeza. Ukiongeza gharama ya cement maana yake umeongeza gharama ya ujenzi na umemnyima uwezo Mtanzania wa kuweza kununua cement nyingi zaidi ili aweze kujenga nyumba nzuri zaidi. Kwa hiyo, ni ushauri wangu kwamba na hili lenyewe kwa sababu linamgusa mwananchi moja kwa moja, Serikali ikalitafakari na itafute ubunifu mwingine kwenye upande wa kodi lakini siyo huu ambao unakwenda moja kwa moja kwa mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kumekuwa na changamoto nyingi sana, Wakandarasi wetu, wazabuni wetu hawalipwi kwa wakati. Leo ukifanya kazi ya Serikali, ukichelewa kumaliza mradi Serikali wanakupiga penalty, lakini Serikali inapompa kazi mzabuni au mkandarasi, ikichelewa kumlipa yenyewe haipigwi penalty. Nafikiri ni vizuri tuweke utaratibu hapa ikiwezekana Serikali pia inapochelewa kumlipa mkandarasi au mzabuni na yenyewe pia iweze kupigwa penalty.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mbaya zaidi kwa sababu watu wetu hawa wanakopa fedha benki na kule kwenye benki wanapewa riba. Kwa hiyo, kadri wanavyochelewa kulipwa na wao wanachelewa kufanya marejesho, mwisho wa siku wanapata hasara kubwa zaidi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri atoe tamko kwenye halmashauri zetu, lakini pia na kwenye taasisi zote za umma ambazo zina madeni walipe madeni kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alishasema jambo hili “Mtu yeyote asitangaze tenda kama hana fedha za kulipa”, lakini huko hali ni mbaya. Nenda karibu kila mahali, halmashauri hazilipi, taasisi za umma hazilipi, kuna madeni kila mahali. Tunaomba hili jambo Mheshimiwa Waziri aliweke vizuri kwa sababu tunajua yeye ni Mchumi mbobezi na tunajua kwenye masuala ya uchumi lazima pia uangalie circulation ya watu wako wale ambao wanafanya shughuli mbalimbali za biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye upande wa gharama za bando. Bahati nzuri nimesoma computer science undergraduate lakini hata degree yangu ya pili nilisoma masuala ya computer. Katika kitu ambacho tunatakiwa tukiangalie vizuri ni gharama za bando, zimepanda sana. Majibu tunayopewa hayaendani na hali halisi. Unaambiwa sijui zima App hii, unaambiwa fanya hivi, hicho ni kitu kimoja kitakupunguzia matumizi, lakini hapa tunachokisema ukiangalia data zetu sisi kwa wastani, kwa mfano mwaka 2020, ulikuwa ukinunua data za 15,000 kwa wiki, ulikuwa unapata wastani wa GB 10. Leo 15,000 hiyo hiyo kwa upande wa Vodacom unapata GB 7.38, ukienda Tigo unapata GB 7.2, ukienda Airtel unapata GB 7.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa unaona kabisa imetoka kwenye 10, hawajaongeza bei lakini wamepunguza bando, kwa maana nyingine pia wameongeza bei. Kwa maana ya kwamba ukiangalia kipindi hicho GB moja ilikuwa ni wastani wa shilingi 1500 ambapo GB 10 ilikuwa ni shilingi 15,000. Leo hii GB moja kwa upande wa Vodacom peke yao unapata kwa shilingi 2,054 kwa hiyo hapa wameongeza shilingi 554. Ukienda Airtel wameongeza shilingi 583, ukienda Tigo wameongeza shilingi 583. Kwa hiyo, gharama za bando zimeongezeka na ndio maana watoto wetu wakipewa assignment kule mashuleni ukimwekea bundle la 5,000 akitumia kidogo tu limekwisha. Kwa hiyo, linaongeza gharama za maisha, inaongeza gharama za shule na inapunguza pia ubunifu wa watu wetu kuendelea kudadisi masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri na nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Nape Nauye, ni vizuri ili suala wakaliangalie vizuri. Nafahamu uzalendo wa Mheshimiwa Waziri, ni vizuri wakakae na wenzetu wa TCRA, mitandao ya simu waangalie namna ya ku–review data hizi na tusiambiwe kwamba mbona kule duniani gharama ni ndogo. Dunia ni dunia na Tanzania ni Tanzania, tuizungumzie Tanzania yetu ambayo ni bora na ya kipekee, haifanani na nchi nyingine yoyote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nadhani niliseme ni kwenye upande wa kodi ya majengo. Nimeona hapa Mheshimiwa Waziri amekuja na mapendekezo anataka kodi ya majengo turudi tulikotoka. Maana zamani ulikuwa unafanyiwa uthamini inajulikana value ya jengo halafu unalipa. Gharama zilikuwa ni kubwa, rushwa zilikuwa nyingi, Mthamini akija pale jengo la bilioni mbili ukiongea naye vizuri anakwambia milioni 800. Kwa hiyo wanaweka mianya ya rushwa. Baadaye Serikali hii hii ikaja na utaratibu kwamba, badala ya kwenda kwenye masuala ya uthamini, basi tuweke utaratibu wa kuangalia kama ni nyumba ya chini walisema shilingi 10,000. Kama ni ghorofa kila floor walisema ni shilingi 50,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wameona hizo fedha ni ndogo ni bora wakae chini waangalie badala ya shilingi 10,000 iwe angalau ni Sh.15,000 na badala ya shilingi 50,000 kwa kila floor ya ghorofa basi angalau iwe shilingi 80,0000 au shilingi 100,000, lakini wakianza masuala ya evaluation, maana wametuambia kwenye maelezo yao wataanza 2026. Sisi tunafahamu hii Serikali, leo wameanza wamechokoza kidogo, ukienda mbele unasema kuanzia Januari utekelezaji utaanza. Kwa hiyo unakuwa na statement ambazo mwisho wa siku unashindwa kujua uisimamie ipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, badala ya kuja na mambo ya uthamini, kwanza yatawapa gharama kubwa, wataalam walio nao ni wachache na wataongeza pia mianya ya rushwa. Tutafute namna nyingine kama wanaona hiki ni chanzo kizuri cha mapato, basi tuongeze pale kidogo, lakini tusiende kwenye uthamini kwa sababu watawakatisha Watanzania kujenga nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ana nyumba yake ya ghorofa 10 anamkopo wa kulipa miaka 30 au 40 halafu mkopo hajamaliza, bado Serikali inakuja kumwambia kwamba pengine tumefanya uthamini na kodi ya majengo utalipa asilimia fulani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kwa sababu namfahamu kuwa ni mchumi mbobezi, daktari na amefanya kazi pia BOT, ni mtu ambaye ana uzoefu wa kutosha pamoja na Naibu Waziri wake na Katibu Mkuu watakwenda kuliangalia, kwa sababu hili wameleta kama pendekezo sio sheria wala sio taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo hili kwa ushauri wangu ni kwamba ni pendekezo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa kina…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, muda wako umekwisha.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, uliahidi kuniongeza dakika mbili sijui bado zipo au umeghairi?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, muda wako umekwisha.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.