Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru umenipa nafasi ili nichangie hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema niweze kusimama kwenye Bunge hili niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii vile vile kumpongeza Waziri wa Fedha kwa hotuba nzuri aliyowasilisha hapa Bungeni, imeleta matumaini kwa Watanzania na ina mambo mengi. Kabla sijaanza kuchangia hotuba hii ya bajeti ya mwaka ujao, ninaomba nichangie bajeti ambayo inaelekea kuisha tarehe 30 Juni, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa kwa bajeti hii ambayo inaendelea sasa hivi. Pamoja na misukosuko ya kiuchumi ya kidunia ameweza kufanya kazi nzuri na miradi yote ya kimkakati imeweza kupata fedha. Ukienda kwenye Mradi wa Bwawa la Nyerere kazi inaendelea, ukifika kwenye Reli ya Kati kazi inaendelea, ukifika Daraja la Magufuli kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni machache nimeona niyaseme kwamba, kazi nzuri wanafanya pamoja na misukosuko ya kiuchumi pia kuna masuala ya kulipa mishahara kwa watumishi hawajakopa, tukiangalia nchi zingine jirani wanakopa mishahara ya watumishi lakini Serikali yetu haijakopa inalipa mshahara ndani ya wakati, nawapongeza sana. Pia fedha za elimu bila malipo kila mwezi wanapeleka fedha bila kuchelewa, hiyo nayo inasaidia watoto wetu wapate elimu sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio ya Kitaifa pia Jimbo la Kwimba tumekuwa na miradi mingi sana imetekelezwa nitaomba niseme machache. Kwanza ni kwenye suala la afya, kwenye masuala ya afya sisi tumepata Hospitali ya Wilaya mpya imejengwa sasa hivi inatoa huduma, tumejengewa vituo vya afya viwili ambavyo vyote vinaelekea kuisha mwezi huu, tumepata zahanati nne zimekamilika, tukienda kwenye elimu madarasa yamejengwa sasa hivi watoto wakiingia shuleni hawakai chini kuna madarasa kuna madawati ya kutosha, tuna Chuo cha VETA kimekamilika kinaanza kutoa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye masuala ya maji kuna mradi wa Hungumalwa ambao unaelekea kuisha kukamilika mwezi wa Desemba mwaka huu, tukienda kwenye maji tena tuna mradi wa Nyamilama nao unaelekea kukamilika ndani ya mwezi wa Desemba, tuna mradi wa Jojilo Maleve imekamilika maji yanatoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme taarifa ya maji ni kwamba Jimbo la Kwimba tuna Kata 15 kwa sasa hivi miradi hii ikikamilika tutakuwa tumeshapata maji ya Ziwa Victoria, maji safi na salama kwenye Kata 14. Mwakani kuna mradi wa maji wa kupeleka Malampaka - Malya itapeleka kwenye Kata moja inaitwa Mwankulwe. Maana yake Jimbo la Kwimba hadi kufika mwakani tutakuwa tuna maji salama safi Kata zote. Ahsante sana Serikali kwa kazi nzuri ambayo mnatufanyia wananchi wa Jimbo la Kwimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nielekeze kutoa mchango wangu kwenye bajeti ijayo, nianze na suala la Kilimo. Mheshimiwa Waziri kama unavyofahamu Jimbo la Kwimba ni Jimbo la Wakulima na Wafugaji. Sisi wananchi wa Jimbo la Kwimba wote ni wakulima, tuna zao la Pamba limekuwa na changamoto mwaka jana, wakati wa msimu mbegu zilichelewa kupatikana, mbolea yule mzabuni aliyechaguliwa na Serikali hakuonekana kabisa kwenye Wilaya yetu, ilibidi tuende Halmashauri, ilibidi ikodoshwe gari kwenda kuchukua mbegu, kuchukua mbolea Mwanza Mjini, tumepata shida sana kwenye mbolea haikufika dani ya muda, wakulima pia ilibidi waende kufuata mbolea Mjini. Kwa hiyo, mimi naomba mwaka huu Serikali itusaidie angalau mbegu na mbolea zifike ndani ya wakati ili wananchi wa Kwimba weweze kulima vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kama Mheshimiwa Waziri umependekeza kwenye hotuba yako kwamba unataka kupunguza ushuru wa forodha, unataka kufanya asilimia 35 ifike asilimia 10 na kwenye mafuta ya kula unataka kufanya kutoka asilimia 35 ifike asilimia 25. Mheshimiwa Waziri kwa kweli mimi sikubaliani na hiyo hoja, ningeomba hilo suala ungeliacha kama lilivyo kwa sababu inaenda tofauti kabisa na malengo ya Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo ilikuja na bajeti yao wanasema mambo mengine ya kuboresha na sisi hapa tunakinzana. Mimi ningeshauri hili suala uliache kama lilivyo pia usaidie wale wanaotaka kuagiza mafuta ya kula na ngano wanunue kwanza mafuta yaliyoko ndani ya nchi na pia ngano wanunue ambayo iko ndani ya nchi inazalishwa ndiyo wapate kibali cha kuagiza nje. Wasipate kibali cha kuagiza bila kuwa na mchango wa kununua mazao yanayozalishwa ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kusema ni kwenye suala la umeme. Suala la umeme napongeza sana Serikali kwamba bajeti ya mwaka kesho tutakuwa tumepeleka umeme vijiji vyote, sasa tunaanza kupeleka umeme kwenye vitongoji. Nawapongeza sana Serikali kwa maamuzi haya, lakini tatizo tulilonalo ni kwamba wananchi wetu wana uwezo wa kulipa umeme? Mimi ningeshauri na kupendekeza kwa Serikali kwamba waangalie gharama za umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kwamba hzi gharama za umeme zilipokuwa zimepangwa na EWURA ilikuwa wakati ule tulikuwa tuna jenereta za Diesel kama mfano Kigoma ilikuwa inatumia majenereta ya diesel, kwa hiyo gharama ya uzalishaji ya umeme ilikuwa juu. Sasa hivi tunazalisha umeme kwa kutumia gesi na mabwawa kwa hiyo bei imeshuka mimi ningependa sana Serikali iangalie tunawapelekea wananchi umeme lakini wana uwezo wa kulipa umeme? Nashauri tupunguze bei ya umeme ili wananchi kwenye vitongoji waweze kuunganishwa na umeme, tusije tukafikisha nguzo lakini haziendi kwenye nyumba kwa sababu hakuna uwezo. Kwa hiyo, lazima tuandae uwezo wa wananchi kupata umeme na kutumia umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ningependa kulisemea ni la barabara. Siku chache zilizopita Mheshimiwa Waziri wa Fedha alitoa tamko hapa Bungeni wakati wa Wizara ya Ujenzi. Tunayo barabara yetu ya Hungumalwa - Ngudu kuelekea Magu tunataka ijengwe kwa lami. Miaka mingi tumeomba hiyo barabara tukaambiwa na Waziri wa Fedha kwamba kuna fedha za African Development Bank anazifuatilia, akizipata hiyo Barabara ya Hungumalwa-Ngudu kueleka Magu ataitangaza. Bajeti yake ambayo amewasilisha Mheshimiwa Waziri tumeona hiyo kwamba fedha za African Development Bank zipo zimekuja. Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri wakati unafanya wind up ya hotuba yako, tuambie lini unatangaza barabara yetu ya Hungumalwa inajengwa kwa lami, lini unatangaza, hilo tamko lako tunalisubiri siku una-wind up hotuba yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwamba Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza tumebaki peke yetu hatuna barabara inayotuunganisha kwenye Mkoa kwa lami. Tunayo barabara ya kutoka Ngudu kwenda Jojilo kwenda Mabuki iko ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kujengwa kwa lami. Tunaomba hiyo barabara pia ifanyiwe utaratibu wa kujengwa kwa sababu Wilaya haiwezi kuwa haina barabara ya lami kwenda kwenye Mkoa. Wilaya zote zinaunganishwa na lami lakini Wilaya ya Kwimba imebaki peke yake tunaomba angalau na hilo pia walifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la kimkoa, Mkoa wa Mwanza tumekuwa na kero ya jengo la abiria kwenye uwanja wa ndege, miaka mingi tumekuwa na kero, tumekuwa tukisemea. Kuna jengo la abiria limejengwa limekuwa na mapungufu, hilo jengo wameshakabidhiwa Tanzania Airport Authority kwamba waliboreshe, wakamilishe. Tunaomba sana uwanja wetu wa ndege uboreshwe na hilo jengo likamilike. Tunaomba Serikali ituambie lini TAA watakamilisha hilo jengo ili liweze kutoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na wageni wetu wanaokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu Airport ya Mwanza ndio sura ya Mwanza. Mgeni anapokuja anakutana na ile jengo ambalo limekaa pale halikamiliki, limekaa kaa tu pale, tunaomba hilo jengo nalo lipate kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu, nakushukuru sana kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)