Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi leo niweze kuchangia katika hotuba hii ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Watanzania, kwa kweli tumeona miradi mingi sana katika Majimbo yetu. Haijawahi kutokea kuona fedha nyingi za miradi zinazokwenda katika Majimbo yetu na jinsi wananchi wanavyopokea miradi hiyo wanaipokea kwa furaha, wanaipokea kwa bashasha na naomba niseme tu kwamba mwaka 2025 Watanzania wengi watatoa pongezi hizo au watatoa ahsante kwa Mama kwa kumpa kura nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niipongeze sana Serikali kwa kujali Jimbo langu la Maswa Mashariki, tumepata fedha nyngi katika miradi, tumejenga vituo vya afya tumejenga barabara tumejenga barabara za Mjini Maswa tumeweka hadi mataa barabarani na sasa hivi kuna miradi mingi inaendelea ambayo kwa kweli wananchi wa Maswa wanashukuru na wanapongeza na watakwenda kumpa kura Mama mwaka 2025 bila kikwazo chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza Serikali juzi tumeshuhudia Serikali imeingia mikataba ya ujenzi wa barabara saba zenye jumla ya kilomita 2090 na zenye thamani ya zaidi ya trilioni 3.7. Mkataba huu tumesaini kwa mtindo ule wa EPC+F (Engineering Procurement Construction and Financing). Huu mtindo ni mpya tunaishukuru sana Serikali kwa kukubali kuingia katika mtindo huu mpya wa ujenzi wa barabara tunaona kabisa sasa barabara zinakwenda kujengwa maeneo ambayo tulikuwa hatutegemei barabara hizo kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Ilani za Chama cha Mapinduzi mara nne au mara tano Ilani zimeandikwa zinasema kwamba barabara ya Karatu -Mbulu – Haydom – Meatu - Lalago, Maswa inakwenda kujengwa. Ilani zimepita tatu, Ilani hii inakwenda kutekelezwa kwa vitendo chini ya Mama Samia Suluhu Hassan, kazi kubwa kwa kweli Serikali imefanya, tunaomba mtindo huu kwa sababu ni mpya Serikali iusimamie kwa karibu, tuone ujenzi huu unafanyika kwa haraka na hata ndani ya mikataba hiyo kama kuna interest kutokana kuchelewesha kulipa au namna ile yoyote ambayo iliwahi kutokea katika ujenzi wa barabara tunavyojenga miaka ya nyuma, basi kuepusha hilo ni kwamba Serikali itekeleze wajibu wake kwa upande wake na wale wajenzi watekeleze kwa upande wao kwa muda uliopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninakupongeza wewe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali yako pamoja na Watendaji wako wa Wizara yako kwa jinsi mlivyokaa na kukubaliana kwamba sasa MSD ipewe mtaji. Tunawapongeza sana, tunaomba MSD wafanye kazi kwa weledi, wafanye kazi kwa uhakika Watanzania wanategemea makubwa kutoka kwao. MSD walikuwa wanaomba sana wapewe mtaji tunashukuru Serikali imekubali na mtaji umetolewa, tunaomba sasa mtekeleze kwa kupeleka fedha na MSD ianze kununua dawa ili iweze ku-supply dawa kwa wakati. Vilevile kuna ujenzi wa vifaatiba vinavyotokana na Pamba niwaombe sana MSD, kiwanda kijengwe kwa haraka, tunatambua mnakwenda kujenga kiwanda hicho katika Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia hili kwa sababu gani? Zao la pamba tumekuwa na changamoto kubwa sana, wakulima wa Pamba tunapolima Pamba, tunapouza Pamba hii baada ya ku-gin inakwenda kuuzwa lint nje ya nchi tuna-export Pamba asilimia 70 mpaka 75, tunatumia asilimia 20 hadi 25 tu kwa ajili ya viwanda vya ndani, tukiendelea hivi Mkulima wa Pamba siku zote ataathirika na bei ya Soko la Dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi lint inauzwa kwa dola 0.73, ukisema mnunuzi wa Pamba anunue kwa faida inabidi anunue Pamba kwa shilingi 800 au 900 maximum shilingi 1000. Indicative price ya Pamba ni shilingi 1,060 ukisema huyu mnunuzi anunue siku zote atakwenda kutengeneza hasara, wakati siku za nyuma bei ya Pamba ilikuwa inaongezeka, siku za nyuma tulikuwa tunaona bei ya Pamba inaongezeka kutokana na soko la dunia linavyosema, lakini tukiendelea kutegemea soko la dunia ambalo linakuwa na direct impact kwa mkulima wa Simiyu, mkulima wa Mwanza hatutamkomboa mkulima. Serikali lazima ifanye intervention kuangalia namna ya kumuokoa Mkulima wa Pamba, anapolima Pamba basi alime kwa uhakika na auze kwa bei ya uhakika inayompa faida, bila hivyo hatuwezi kuliinua zao letu la Pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Wabunge wengi wamepiga kelele baada ya kusikia kwamba bajeti inakwenda kupunguza kodi ya mafuta ambayo yanaingizwa kutoka nje yaani kwa maana ya crude oil kwenye palm oil.

Mheshimiwa Mwenyekiti, palm oil siku zote inajulikana duniani ni rahisi, ukiileta kwa bei ambayo umepunguzia kodi huyu muingizajiwa crude oil ya palm oil, muuzaji wa mafuta ya Pamba, mafuta ya Alizeti hawezi kuingia kwenye competition kwa sababu mafuta yake yatauzwa kwa bei ya juu. Crude oil bei yake ni chini na kibaya zaidi au kizuri zaidi kwa upande wa crude oil ukimpa huyo kodi ya asilimia 35 akiingiza atafanya refine aka-refine yale mafuta, by product yake anakwenda kutengenezea sabuni akitengeneza sabuni atapata faida huko. Mkulima wa Alizeti mafuta yake akikamua Alizeti by product yake ni mashudu, Pamba by product yake ni mashudu hayana thamani kubwa zaidi ya kuwa chakula cha Wanyama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukimshushia kodi mwenye crude oil ya palm oil, mimi niliona kwamba ina mantiki lakini baada ya Wabunge wengi kulalamika tumekuja kugundua kwamba ukiweka asilimia 35 ya crude oil ukamuwekea import duty, akiingiza mafuta akafanya refine atauza kwa bei ambayo inafaida kidogo sana lakini atatenengeza faida kwenye sabuni ambayo ni by product ya crude oil. Kwa hiyo, nadhani Mheshimiwa Waziri hebu tujaribu kukaa na ku-rethink, kuona ni namna gani ya kufanya ili kusudi Mtanzania asije akanunua mafuta kwa bei ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua crisis ya mafuta inakwenda mpaka kwa muuza chips, crisis ya mafuta inakwenda kwa Watanzania moja kwa moja. Kwa hiyo, tuiangalie mahitaji ya mafuta ni tani 680,000 kwa mwaka, Watanzania tunaweza kwa kutumia mbegu zote uwezo wetu ni ku-produce tani 300,000 tu. Sasa tani 380,000 inabidi tutoe nje sasa tuangalie ni namna gani ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye Ngano. Kuna Mbunge mmoja jana hapa amepiga kelele sana jana kuhusiana na suala la Ngano, lakini Ngano tunaambiwa kwamba mahitaji ya Ngano kwa mwaka ni metriki tani 1,000,000, production yetu Tanzania ni only 20 percent, sasa hatuwezi kuishi bila ku-import Ngano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lile sharti lililowekwa na Wizara ya Kilimo la kwamba mfanyabiashara anayetaka ku-import muwekeeni sharti, asilimia 20 mpaka asilimia 30 ya Ngano anayonunua anunue ndani, 70 percent anunue kutoka nje, liwe ni sharti ili kusudi aweze kununua Ngano ya ndani anunue na Ngano ya nje, kwa sababu yeye ni mfanyabiashara wa Ngano afanye hivyo ili kuipa soko Ngano yetu ya ndani vilevile na ngano ya nje iweze kuingia lakini mkipandisha sana kodi impact inakwenda kwa Mtanzania moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wengi sasa hivi asubuhi Mama Lishe anapika chapati, chapati ikibaki inalika mchana na ikibaki anaenda kuwapa wanae jioni wanakula. Kwa hiyo, ngano imekuwa ni chakula kikubwa sana. Vilevile hata ukiangalia kwenye mafuta chips imekuwa ni chakula kinachoshindana na wali, zamani tulikuwa tunakula wali jioni siku hizi watu wanakula chips jioni. Kwa hiyo, ni lazima tuwe makini tukicheza vibaya tukakuta kodi imepanda impact inakwenda kwa Watanzania moja kwa moja kwa hili Mheshimiwa Waziri lazima tuwe makini na tuweze kuishauri vizuri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)