Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Natumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kutoa mawazo yangu katika siku ya leo tunapochangia Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza napenda kabisa kwanza kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake. Pongezi hizi nazitoa kwa niaba ya wananchi ya Mafinga, kwa niaba ya wananchi wa Mufindi Kusini ambao wewe umekalia hicho kiti na kwa niaba ya wananchi wa Mufindi Kaskazini kwa kaka yetu Exaud Kigahe ambaye ni Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini natoa pongezi hizi? Nampongeza Mheshishimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwanza kwa ule mpango wa EPC+F, watu wengi walikuwa na mashaka kwamba unaweza mpango ule usije ukawa ni kitu cha kikweli kweli, lakini wiki iliyopita tumeshuhudia kusainiwa kwa Mikataba na ujenzi wa Barabara ya Mafinga Mgololo kilomita 81 unaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa sababu pia jana wameweka saini mkataba wa Barabara ya kutoka Mtiri kwenda Ifwagi mpaka maeneo ya Mkuta kilomita 14 ambako ni Jimbo la Mufindi Kaskazini, lakini wakati huo huo Nyororo–Mtwango ambako ni kwako wewe Mwenyekiti wameshaanza. Hapa naomba niweke na kaombi kidogo pamoja na kuwa umesema tuki–address kiti hapa naki–address kiti na naomba pia nim–address na Waziri wa Fedha. Tunaomba pale Nyororo – Mtwango tumeshaanza, lakini kwa sababu tunafanya kwa fedha za ndani, tunaomba Serikali itupie jicho, ipeleke fedha ili ujenzi wa ile barabara uende kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi, katika hiyo Wilaya ya Mufindi ambao ni tajiri wa mazao ya misitu, maana tumezungumza hapa kuhusu vitongoji 15 kila jimbo kupatiwa umeme, nguzo zitatoka kule. Kwa hiyo itaimarisha miundombinu kutoka Sawala – Iyegeya mpaka Lulanda, jumla kilomita 40.7. Nafahamu ziko zile thelathini na ngapi na zile kumi ambazo tumeongezewa. Kwa hiyo haya yote mimi binafsi kama nimetoka Mafinga na Mufindi ambako Mheshimiwa Mwenyekiti wewe ni shahidi, sisi kama Wabunge watatu tumesimangwa sana, tumesemwa sana, lakini wananchi walikuwa hawajui, yako mengine tunaweza tukayasema hadharani lakini mengine tunayaficha chini ya meza, hatimaye yamekuwa, barabara zinaanza kujengwa. Kwa hiyo naipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi specific kwa Wanamufindi, nakuja na pongezi kama mbili, maana pongezi ni nyingi. La kwanza, ni hili la kuondoa ada kwa watoto wetu watakaokwenda kwenye Vyuo vya Ufundi, DIT, Dar Tech na ile zamani tulikuwa tunaita Mbeya Tech siku hizi inaitwa MUST.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mikubwa ya umeme, tuna Mradi wa SGR yote hii itahitaji mafundi wa kuihudumia kama sehemu ya maintenance. Kwa hiyo wazo hili ambalo Mheshimiwa Rais amelileta ni jambo jema, kwa sababu tutapata watoto wetu ambao watakuwa na ujuzi, watahudumia miundombinu ya reli yetu, lakini pia na miundombinu itakayotokana na umeme tutakaozalisha kwenye bwawa wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwasilishe ombi na ushauri kwa Serikali kwa maana ya Waziri wa Fedha. Naomba sisi tunaotoka kwenye mazao ya misitu, ukienda kwenye msamaha wa VAT sana sana unapata kwenye vitendea kazi kama vile matrekta ya kuvuta magogo kutoka shambani kupeleka site au kupeleka barabarani. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, ili tuwe na connectivity, baada ya kuwa tumetoa ada kwenye hivi Vyuo vya Ufundi, tutoe pia VAT kwenye equipment hasa hasa za mazao ya misitu ili hawa watoto tukishawasomesha wawe na mahali pa kuanzia. Kwa hiyo hili ni jambo muhimu sana katika ku–add value. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napongeza ni ambalo linaenda moja kwa moja kwenye Wizara ya Mheshimiwa Nape. Mara nyingi tunalalamika kuhusu mambo haya ya bundle na kadhalika, napongeza kwa sababu Mheshimiwa Waziri Nape na Serikali kwa ujumla wamekuwa wasikivu na wananchi wengi wanaweza wakawa hawajui, ile kupitisha miundombinu kwa ajili ya masuala ya mawasiliano ilikuwa kwa kilomita moja ukipitisha labda kwenye barabara za TARURA au za TANROAD kwa kilomita moja walikuwa wanatozwa dola 1,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limesemwa sana na mimi nilichangia kwenye Mpango na Serikali imekuwa Sikivu, sasa imepungua kutoka dola 1,000 ile kupata leeway mpaka dola 200 na ile annual fee imetoka 1,000 mpaka 100. Kwa hiyo matarajio yetu kwamba punguzo hili linaenda kuchochea uchumi wa kidigitali. Kwa hiyo, hili hapa napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zinaweza zikawa nyingi, lingine ni hili la kuwa na dirisha la kutoa huduma kwa wawekezaji. Napongeza kwamba kutakuwa na mfumo wa pamoja ambapo Taasisi kama NEMC, OSHA, BRELLA, TRA, TBS na kadhalika, zitakuwa zinapata kwa pamoja. Hapa napo nitoe angalizo, unakuta mfanyabiashara au mwekezaji amejaza kila kitu, litakapofika suala la control number, that’s a big problem, mara mtandao uko chini, mara njoo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yangu kwamba Serikali wakiongozwa na Wizara ya Mawasiliano ya Mheshimiwa Nape, hebu turahisishe maana yake yale ni mapato. Mtu ameshajaza kila kitu siku tatu kupata control number, anaambiwa mtandao sijui uko chini, mtandao uko taratibu, mtandao sijui umesimama. Naomba kama tunafanya huu muunganisho wa mifumo tuendane pia na kuimarisha na kuboresha miundombinu ya kuwezesha sasa huu uchumi wa kidijitali uende vizuri kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hili suala ambalo kwenye ukurasa nadhani wa 50 hadi 51, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na ningeomba Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, naona unazungumzishwa hapo hili unisikilize vizuri sana pamoja na kwamba Mwenyekiti umesema tuelekeze kwako. Kwenye suala hili la kukosekana au kuwa na upungufu wa dola, Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesema jitihada tunazofanya mojawapo ni kuhakikisha tunazalisha, tuuze nje kuliko kuagiza, sasa hapa nakuja wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuamue suala moja, tunaamua kuwa Taifa la wazalishaji au Taifa la wachuuzi, mimi Cosato Chumi na wanamafinga sisi tunataka tuwe Taifa la wazalishaji na hayo ndiyo maono ya Mheshimiwa Rais na ndiyo maana tukapewa ruzuku ya mbolea, ndiyo maana tunapewa ruzuku kwenye mbegu. Kwa hiyo, mimi ushauri wangu kwenye suala la mafuta na mimi hili nasema na sitoacha niliseme mpaka litokee, hebu Mheshimiwa Waziri tuende na mfumo wa kwenye sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari viwanda vilikata tamaa kuwekaza kwa sababu tulikuwa tunatoa vibali hovyo hovyo sukari inakuwa flooded hapa lakini baada ya kudhibiti na kuweka utaratibu mzuri tunaona uwekezaji na upanuzi kwenye viwanda vya sukari umeongozeka na sasa hivi deficit ni kama tani 15,000. Kwa hiyo, naomba kwenye ngano na mafuta ya kula na watu wa Serikali kuna mahali wanataka kutuchonganisha Wabunge na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikiliza juzi Mheshimiwa Waziri vizuri sana kwamba basi tutapandisha, kana kwamba huo ushuru wa asilimia 35 kana kwamba ukipandishwa bei itakuwa kubwa, hata ulipopungua, ulipokuwa zero rated Waheshimiwa Wabunge, bei ya mafuta ya kula haikupungua huo ndiyo ukweli, mlaji wa mwisho hakunufaika, yamenufaika ma–tycoon lazima tuseme ukweli. Bei ya mafuta imepata ahueni kidogo juzi baada ya kuanza kuvuna alizeti. Kwa hiyo, naomba na wataalam wake Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili la Kamati naunga mkono mapendekezo ya Kamati kwa ujumla imeenda vizuri, isipokuwa kwenye suala la cement ile shilingi 20 ambayo ni sawa na mfuko 1,000 Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais ameshiriki mikutano sasa mfululizo mara mbili, ule wa dunia wa mabadiliko ya tabianchi, kuna fedha nyingi kwenye mifuko ya mabadiliko ya tabianchi, na kuna mahali Kamati imempongeza Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, kuliko tutwishane mzigo Watanzania bado ziko fedha nyingi. Mheshimiwa Kakoso amesema hapa jana, hii biashara tu ya hewa ya ukaa kama sisi tunaotoka Mufindi, Iringa, Njombe Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inaweza ku subsidize kuliko kumtwisha mwananchi hii shilingi 20 sawa na 1,000 kwa mfuko wa cement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kutoka mwisho, nina barua umoja wa wastaafu Halmashauri ya Mji wa Mafinga wanaomba ile pensheni ya iongezwe. Mapendekezo yao wanasema lile dirisha kwamba wazee kwanza wanapokwenda kupata afya, hapana tuwe na dirisha lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo la mwisho kwa Mheshimiwa Bashe, nimekutumia meseji kuhusu mahindi. Mimi naomba niwatoe wasiwasi Serikali, mmesema tu – apply na asubuhi umesema watu wana – apply lakini mtandano uko chini. Hii dhana kwamba eti wakulima tutauza hadi tusahau kujiwekea chakula siyo kweli. Sisi tuna akili timamu kwa miaka yote. Kwa hiyo, ni mambo mawili, ama mrahisishe upatikanaji wa vibali kwenye huo mfumo wenu tuuze nje, pili kama hamuwezi NFRA nunueni kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Mungu Ibariki Mafinga, Mungu Ibariki Mufindi, Mungu bariki viongozi wetu, mmbariki sana Mama Samia Suluhu Hassan. Ahsanteni sana. (Makofi)