Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nami nichangie hoja hii ya hotuba ya Wizara ya Fedha na Mipango, lakini pia mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii yenye mapato na matumizi ya mwaka 2023/24 ni bajeti ya wananchi. Na hii tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, bajeti imebeba unafuu wa maeneo kadhaa muhimu kwa ajili ya wananchi. Mimi nampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan lakini pia kwa kuweka vipaumbekle vya sekta zifuatazo; elimu, maji, barabara, nishati na afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hizi ndiyo zinazongoza kwa maendeleo ya wananchi. Wananchi wakipata mafanikio katika haya mambo matano, ndiyo watakuwa wamesema tumepata maendeleo. Maeneo haya matano yanagusa wananchi wote Tanzania na ndiyo maana nasema kwa kweli bajeti ya mwaka huu ya mama Samia Suluhu Hassan na ndugu yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Wizara yake, ni ya wananchi. Hongereni sana Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wataalam wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa mliyoifanya kuandaa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitaje maeneo ambayo yametugusa sisi wananchi, na haya ni baadhi tu; moja, tozo ya SDL au ujuzi wa elimu. Tozo hii nilipoingia Bungeni hapa ilikuwa ni asilimia sita ya kila mfanyakazi wa sekta binafsi mshahara wake analipiwa na mwajiri asilimia sita. Na hii ilikuwa taabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya kuomba kazi katika Nchi za Afrika Mashariki, ile gharama ya ajira kwetu ilikuwa iko juu sana. Hii tozo haipo Uganda, haipo Rwanda wala Burundi, Kenya ipo asilimia ndogo tu kwenye sehemu ya utalii. Lakini Tanzania ilikuwa asilimia sita. Leo nasimama hapa – na ninaomba nitoe taarifa kwamba ni mwajiri imepunguzwa kutoka asilimia sita mpaka asilimia tatu; sisi waajiri tunampongeza sana mama. Na hili hakika hatutamsahau. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, kuondoa ada za vyuo vya kati. Nimesoma vyuo vya kati hivyo, vinaitwa elimu ya ufundi ama elimu ya amali, kutokea shule ya msingi na kwenda shule ya upili (sekondari) form one mpaka form four (kidato cha kwanza mpaka cha nne) unachagua masomo ya kiufundi, halafu unakwenda chuo cha ufundi. Wakati huo zilikuwa shule mbili tu, Shule ya Sekondari ya Ufundi Ifunda na Moshi Technical. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunalipwa hela na Serikali sisi kusoma pale. Sijui ilitokea nini wakaondoa ikalazimu wanafunzi walipe ada pale, wazazi wenye uwezo wa chini walishindwa kupata wataalamu wa ufundi kwa sababu hatukuweza kulipa tena ada; tunamshukuru sana mama Samia na kwa hilo mama Samia hatuwezi kukusahau kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni Serikali kutofunga biashara kwa sababu ya migogoro ya kodi kati ya wafanyabiashara na Serikali. Suala la kufunga biashara ilikuwa inafunga mapato ya Serikali, ilikuwa inafunga kodI za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ndugu yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, umepiga ndipo. Kwa kuondoa hizo gharama za kuwafungia watu, wengine wamepoteza roho zao, wengine wamekufa, ilikuwa taabu sana. Hebu fikiria una biashara yako unakula na unaishi halafu imefungwa kwa sababu ulikosea kidogo mahesabu na siyo watu wote ni wataalamu; umefanya jambo zuri sana, Mungu akuongoze na hatutakusahau. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne; mapendekezo ya Serikali yanalenga kuendeleza miradi iliyopo. Nimepitia bajeti yote hii, inalenga matrilioni ya fedha ili kumaliza miradi inayoendelea kimkakati. Niitaje hapa; Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR, Daraja la Magufuli, ununuzi wa ndege, ujenzi wa meli, ujenzi wa barabara, kuendeleza REA (umeme), ujenzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa vituo vya afya, elimu bure, kuongeza bajeti ya kilimo. Haya siyo mambo madogo. Ndiyo maana nasema leo hii, na ninaweza kusema kifua mbele kwamba bajeti hii ni ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kulijali sana jimbo langu. Jimbo la Tabora Kaskazini ukifumba macho ukaangalia mambo yaliyopita lilikuwa la ajabu ajabu sana. Leo tumepata hela nyingi sana kupitia Halmashauri ya Uyui, tumepata fedha nyingi sana kutekeleza miradi ya elimu, maji, umeme, barabara, afya na utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Uyui ilikuwa hana majengo, tulikuwa chini ya mti tumejishikiza kwa DC. Tumepata majengo ya shilingi bilioni nne, majengo mazuri ya kisasa. Tena ndiyo ghorofa la kwanza kijijini kule lipo; tunamshukuru sana mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaka unda haneni, maana yake akinena kishapata, naogopa kuyasema mambo mazuri yanayokuja kwangu, lakini wacha niwatajieni machache, hamtayaondoa. Kwa ufupi, bajeti hii iliyomalizika imefanya mambo yafuatayo katika Jimbo langu, na nimesema niyataje; tumejenga kituo cha VETA, tumejenga madarasa mengi ya shule za sekondari na msingi, tumejenga mradi wa BOOST, tumepewa shule mpya ya msingi (milioni 500), mpya kabisa tujenge; tumepewa shule ya sekondari mpya tujenge (milioni 470). Na kuhusu afya tumepewa vituo vya afya vitatu tumejenga na vimekamilika. Lakini pia tumepewa zahanati mbili na zahanati nyingi tumekarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya siyo madogo ya kuacha kupongeza. Ni lazima tumpongeze mama huyu ambaye ana utu, ana mapenzi na wananchi wake, lakini ni mlezi wa wananchi wake, ametuona sisi Uyui. Nani kama mama? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hakuna.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji, nikwambie, ndiyo nimesema mtaka hunda haleni msione wivu kidogo. Jimbo la Tabora Kaskazini lina vijiji 68 tunafungua maji ya bomba chini ya miti kutoka Mwanza Ziwa Victoria na haya hayakuwepo kabisa. Leo tuna maji ya bomba ya Ziwa Victoria lakini pia mradi wa ile miji 28 katika vijiji vyangu 82 utaongeza vijiji vinavyopata maji mpaka vifike 72. Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Mwigulu na Wizara yako, mmetutendea mambo mazuri sana Jimbo la Tabora Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na umeme, umeme tulipoingia madarakani sisi hata Kijiji kimoja hapakuwa na umeme. Leo hii nasimama hapa nasema vijiji 58 tunawasha umeme, bado vijiji 24, na ambavyo mpaka mwezi wa nane unakamilika. Hii ni bajeti ambayo sisi wana Uyui tunaiona kama ni ndoto vile lakini ni bajeti ambayo tunafikiria kwamba imetubeba vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara, Jimbo langu ni jipya, Wilaya yangu ni mpya tulikuwa hatuwezi kutembeleana barabara hakuna tumejenga barabara. Mama ametupa ela nyingi karibu bilioni tatu tujenge barabara na barabara zimekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeitaja miradi hii ambayo ni alama za utu, upendo na ulezi wa Mama Samia Suluhu Hassan jimboni kwangu. Pongezi nyingi kutoka kwa wana Uyuwi Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge hoja mkono, Ahsante sana. (Makofi)