Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia bajeti kuu ya Serikali. Kwanza kabisa napenda nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba Watanzania tunaishi katika maisha mazuri. Ni ukweli usipingika kwamba katika kipindi chake cha uongozi hakuna hata jimbo moja katika nchi hii ya Tanzania ambalo limekosa mradi mkubwa wa maendfeleo kutoka kwa Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu za pili, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa wanayoifanya, na hasa hii ya kutuandalia bajeti, ambayo itakuwa mkombozi kwa wananchi wetu wa hali ya chini katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa vipaumbele vyake vya bajeti ya mwaka 2023/2024. Kwanza kabisa nianzie katika miradi mikubwa ya maendeleo; Bwawa la Mwalimu Nyerere. Bwawa hili litakapo kamilika litakuwa mkombozi mkubwa sana kwa wananchi wa Tanzania na hasa kwa kutupatia umeme wa uhakikia na wenye unafuu. Ni matumaini yangu kabisa, litakapokwisha Bwawa hili, la Mwalimu Nyerere, Watanzania wengi watanufaika na kufaidika na umeme wa bei rahisi kama ilivyoelezwa na viongozi wetu hapo nyuma, kwamba Bwawa la Mwalimu Nyerere litakapokwisha basi hali ya umeme nchini itarudi katika ubora wake na wananchi watapata unafuu wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa Mradi wa SGR. Mradi huu utakapokamilika utaleta maendeleo makubwa sana katika nchi yetu. Pia nipongeze Wizara ya Fedha kwa kuongeza bajeti katika Wizara ya Kilimo hadi kufikia bilioni 170.8. Haya ni maendeleo makubwa sana ambayo tunakwenda kuyapitia katika nchi yetu. Pia nipongeze Wizara kwa kutenga fedha katika vipaumbele vyake kujenga mabwawa 100 kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji. Hii itasaidia sana katika sekta ya kilimo na wananchi wa Tanzania watapata manufaa makubwa kupitia mabwawa haya 100 ambayo yanakusudiwa kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu zingine nizitoe kwa Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa ujumla katika kipaumbele cha Mradi wa SEZ Bagamoyo. Mradi huu ni wa miaka mingi. Tangu wananchi walipofanyiwa tathmini yapata miaka kumi na nne. Lakini sasa Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi pamoja na viongozi wake wameamua sasa mradi huu waupe kipaumbele katika bajeti ya mwaka huu. Hii ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo ya Zinga Bagamoyo wanafaidika na wananufaika ili miradi ya maendeleo ya viwanda pale iweze kuanza na wananchi pamoja na nchi nzima iweze kufaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala moja, jana wachangiaji wengi sana walizungumza kuhusu suala la kodi ya ngano, na mimi nataka nilizungumzie kidogo suala hili. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba pamoja na Mawaziri wenzie wa Afrika Mashariki kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Wameona ni jinsi gani hizi nchi za Afrika Mashariki zinavyotaabika katika suala zima la chakula. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumza kabisa, mwaka 2019 uchumi katika kwa upande wa mfumuko wa bei ilikuwa 3.5 percent lakini mpaka kufika mwaka 2022, mfumuko wa bei umefikia asilimia 8.7 hii ni hatari sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii inasababishwa na Vita ya Ukraine pamoja na Ugonjwa wa Covid ambao ulitupitia. Sasa basi naomba kitu kimoja, tuiunge mkono bajeti hii na hasa katika suala zima la kupunguza kodi katika chakula. Mimi nikupongeze Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Mawaziri wenzio wa Afrika Mashariki kwa hatua mliyochukua. Leo hii kwa mfano suala la ngano, wafanyabiashara wa Tanzania, uzalishaji wao wa ngano ni tani milioni moja na laki moja mpaka tani milioni moja na laki mbili. Uzalishaji wetu katika nchi sidhani kama unazidi tani laki moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukisema kwamba unawapandishia kodi ya ushuru wa forodha asilimia 35, Mama Ntilie wetu, wapika chapati, wapika mandazi hivi watakuwa katika hali gani? Kwa sababu mfanyabiashara utakapompandishia kodi lazima na yeye atapandisha bei ya bidhaa, na atakapo pandisha bei ya bidhaa wanaokuja kuathirika ni wananchi wakawaida. Kwa hiyo nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa hatua hii, hakuna jambo baya ambalo limefanyika, jambo ni kunusuru maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kulizungumza. Naomba Mheshimiwa Waziri hili kidogo alitilie mkazo. Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake wametoza bidhaa za viwango vya asilimia 20 kwenye mashine za kamari zinazoagizwa nchini. Mimi kwa maoni yangu hizi mashine za kamari ni janga kubwa sana katika Taifa letu. Pamoja na kwamba tunapata mapato kwa kupitia mashine hizi za kamari lakini kipato tunachopata ni kidogo kuliko athari ambayo wanaipata wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii baba ana shilingi 15,000 yake baada ya kwenda kununua unga wa watoto wakale nyumbani anakwenda kucheza kamari, akifika kule fedha zote analiwa, akirudi nyumbani hana chakula cha watoto, fedha yote kaibwaga katika kamari. Halafu Je, tuna control gani ya hawa wanaochezesha kamari kama hizi fedha wanapeleka benki? Asilimia kubwa wakitoa fedha kwenye mashine zao wanapeleka majumbani mwao kuhifadhi, mzunguko wa mabenki unapungua.

Mheshimiwa Waziri nikuombe sana hili suala mliangalie kwa kina either kama tunahitaji kupata kodi katika hizi mashine za kamari basi tuongeze kodi kubwa sana. Na kama hatupati kodi ya kutosha basi tuziache kwa sababu hazituletei faida, zinaumiza wananchi wetu. Wananchi kwa kweli wamekuwa mateja wamekuwa addicted na hizi kamari, uchumi wao unakuwa mbaya, maisha yao yanakuwa magumu kwa kwa sababu ya kucheza kamari kila siku. Mheshimiwa Waziri mimi naomba sana, kuna vitu vingi vya mapato vya kubuni lakini hiki sio chanzo ambacho ni afya kwa maendeleo ya wanajamii yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala taasisi zinazokopesha. Kuna taasisi ambazo zimezuka mitaani huko zinakopesha watu, hizi taasisi kwa kweli ni janga kwa wananchi wa Tanzania. Kuna taasisi ambazo wananchi wanafikia hatua mpaka wanakimbia majumbani kwao. Leo mwananchi wa kawaida mama wa Bagamoyo ambaye hakusoma unamwambia nitakukopesha kwa asilimia ya 45 riba, hajui maana ya asilimia 45 ni nini, anachukua mkopo baadaye anaambiwa katika laki moja uliyochukua unatakiwa ulipe shilingi 45,000, anashangaa. Yeye anafikiri kaambiwa kwamba alipe shilingi 45,000 ya kuchukua laki moja, sasa hii inaleta changamoto kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi taasisi mmezipa vibali nyingi sana, hazifanyi kazi yenye kutukuka kwa wananchi wetu. Watu wanaacha nyumba zao, wanakimbia kwa sababu ya kukimbia mikopo ambayo inakopeshwa na hizi taasisi. Naomba Wizara ichukue hatua kuhakikisha kwamba kunakuwa na taasisi maalum ambazo zitapewa vibali zenye kukopesha tena kwa masharti ya riba maalum ili wananchi waweze kupata hiyo mikopo na wasiathirike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa anayoifanya, kazi ya kuandaa bajeti sio kazi ya mchezo. Bajeti hii ni bajeti ya mfano wa kuigwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa anayoifanya. Kazi ya kuandaa bajeti sio kazi ya mchezo. Bajeti hii ni bajeti ya mfano wa kuigwa. Bajeti ambayo itakwenda kurejesha uhai wa wananchi wa Tanzania. Nimshauri Mheshimiwa Waziri, maneno yapo mengi, watu wanasema sana, lakini kazi wanayoifanya ni kubwa. Leo hii mmekaa katika hizo nafasi sio kwa nia mbaya ya kuwadhulumu au kuwanyanyasa Watanzania. Lengo na madhumuni yao ni kuwajenga Watanzania. Kwa hiyo, wajitahidi, pale ambapo wataona panafaa, basi wahakikishe kwamba bajeti wameitengeneza vizuri na wananchi wapate faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)