Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nina imani kwa sababu ni wa mwisho nitapata hata dakika 15. Cha kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa nafasi hii ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kutoa mchango wangu kwenye bajeti kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa niaba ya wakulima hapa nchini hasa wakulima wa tumbaku, wakulima ambao walifkia hatua ya kukata tamaa. Lakini kwa uwepo wa Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan; wanunuzi walikuwa wameshaondoka nchini; hivi tunavyoongea leo wanunuzi wa tumbaku Tanzania ni wengi. Bei ya tumbaku sasa imepanda kutoka dola 1.4 leo wastani wa bei ya tumbaku inayozunguka kwa wakulima wetu katika mikoa yote inayolima tumbaku ni wastani wa dola 2.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, niendelee kukuomba sana wakulima wa tumbaku wanahitaji waione dola 4 kwenye bei yao, wakulima wa tumbaku wanataka waone bei inazidi kuongezeka. Tunaomba uendelee kutupunguzia kodi ambazo zinabana wanunuzi wa tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kazi unayoifanya ni nzuri sana, bajeti yako imekaa vizuri, hotuba yako ilishiba vizuri sana. Ombi langu hili; mwaka jana kwenye bajeti nilikuomba sana tuondolee kodi kwenye Hanson cross ili wakulima wa tumbaku waweze kupata faida kubwa. Tuondolee kodi kwenye ushuru wa duty twine ili wakulima wa tumbaku waweze kupata faida kubwa. Waondolee wanunuzi ushuru wa mionzi wanapata shida kubwa sana. Tunahitaji ushuru uendelee kupungua kwa sababu Mheshimiwa Rais anahitaji wakulima waende kulima, wakulima waweze kupata faida kubwa sana. Kwa hiyo niendelee kukupongeza Mheshimiwa Waziri ulianya kazi kubwa sana bajeti yako imeshiba vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais. Kwenye Jimbo la Ushetu leo tunavyoongea tulikuwa na barabara zetu ambazo zilikuwa hazijafunguka. Mheshimiwa Rais wakati anaingia madarakani tulikuwa na mtandao wa barabara kilometa 400 tu lakini leo mtandao wa barabara katika Jimbo la Ushetu ni zaidi ya kilometa 1029 ni kazi kubwa imefanywa na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ilikuwa haifanyi kazi, leo tumewekewa x-ray tuna vifaa vyote vimejaa, watalamu wetu kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu inafanyika, operation zinafanyika pale pale. Wananchi wa Ushetu sasa hawaendi tena katika Manispaa ya Kahama kazi inafanyika vizuri katika Halmashauri yao ya Ushetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumwomba tu Mheshimiwa Waziri. Tuliahidiwa Kituo cha Afya Ulowa, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Kata ya Ulowa aliahidi ujenzi wa kituo cha afya tangu mwaka 2017, leo miaka zaidi ya mitano hakuna kituo cha afya hakijajengwa, Mheshimiwa Waziri tupelekee fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuiomba Serikali walituahidi kilometa 54 za lami, nashuhudia tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu wana-sign mikataba, mikataba inazinduliwa kwenye majimbo ya wenzangu. Mheshimiwa Waziri hebu nipelekee fedha na mimi kwenye kilometa 54, kwenye hii barabara ambayo iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Aliahidi marehemu Magufuli sasa barabara ile bado haijaanza kujengwa. Tuombe basi angalau kwenye bajeti hii tukazindue, tukasaini na wewe uwepo kwenye uzinduzi wa barabara inayotoka Kahama inapita Nyandekwa, inapita Ukune, inapita Kisuke, inapita Nyambilangano inaenda Uyogo inaunganisha mpaka kwenye Jimbo la Kaliua kwa ndugu yangu Mbunge wa Kaliua. Tuwekee na sisi historia kwenye Jimbo la Ushetu tupate angalau hata lami ya kipindi cha utawala wa Mheshimiwa Rais pamoja na wewe ukiwa Waziri wa Fedha ya kuweza kupigia picha wananchi wa Ushetu, tunakuomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais mwaka jana ametupa zaidi ya 2,080,000,000 madarasa yamejengwa vizuri; lakini ametupa shule mpya mbili zaidi ya milioni 800 shule zimejengwa na zimeshakamilika zinafanya kazi. Niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuomba, tuna kilio kwa wakulima wa pamba. Hali ya wakulima wa pamba bei inazidi kuporomoka niendelee kukuomba kuwepo na mfuko wa pembejeo. Kuwepo na mfumo wa kinga ya mazao hasa mazao ya kimkakati kipindi bei ya masoko inapokuwa imetikisika. Leo hii wakulima wa pamba wametumia gharama kubwa kuzalisha zao lao, wamelima pamba nyingi, wamehamasika hasa baada ya kupelekewa mbegu za pamba kwa bei ya ruzuku. Tunaomba sasa, kama mtikisiko wa bei ya pamba inapokuwa mkubwa hivi kwenye mazao yetu ya kimkakati tuwe na maandalizi, tusisubiri mpaka tukio litukute halafu ndipo tuanze maandalizi. Leo hii bei ni 1,060 mpaka inaenda mpaka shilingi 1,000 lakini wakulima wanalia wanasikitika bei ya pamba imeporomoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe sasa, kama mwaka mmoja korosho ilishuka bei Serikali yetu iliweka mkakati wa kuzinunua korosho zote na bei iliongezeka na Serikali ikaja kuuza. Mafuta yalipanda bei Mheshimiwa Rais akaamua kuweka bilioni 100 kwa kila mwezi; lakini pembejeo pia mmeweka ruzuku kwa nini sasa mtikisiko huu wa bei msijifungie wataalamu ambao Mheshimiwa Rais akaamini mkaweka ruzuku ili wakulima wetu wa pamba waweze kupata bei nzuri? Kwa sababu wamehamasika kulima pamba vizuri. Sasa wanapopata beii ndogo imeshuka, tunawashusha tena wanashuka chini hawawezi kulima pamba mwakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niendelee kuomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa sababu uko hapa lichukue hili kwa ajili ya kuweka kinga ya mazao tuwe na mfuko wa kinga ya mazao ya kimkakati tunapoingia kwenye mtikisiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa tumbaku wanahitaji kulipwa fedha zao kwa dola. Tunapata taarifa kwamba wakulima wa tumbaku inawezekana wakalipwa shilingi kitu ambacho ni hatari sana. Wakulima kwenye mkataba wetu wa halmashauri ya tumbaku malipo yanafanyika kwa dola, makato ya bei yao wamekatwa kwa dola iweje sasa malipo yaende kwa shilingi? Na Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati anahutubia hapa kwenye mpango wa bajeti yake amesema Serikali ina akiba ya dola zaidi ya 1,177,000…
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu iweje leo dola…
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Emmanuel, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kakoso.
TAARIFA
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kunipa nafasi ya kumpongeza ndugu yangu Cherehani na kutoa taarifa juu ya anachokizungumzia. Zao la tumbaku limekuwa na uhimilivu wa kuuzwa kwa bei nzuri kwa sababu ya makubaliano yado la, pembejeo zinakopwa kwa dola, mauzo yote yanafanyika kwa dola. Sasa tunapofikia hatua ya kutaka kuuza kwa shilingi ni kuwaua wakulima naomba sana dola iendelee kuliko mapendekezo yalivyo kwa sasa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Cherehani, taarifa unaipokea?
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii kwa sababu wakulima wana matumaini, wana imani kubwa na Mheshimiwa Rais, wana imani kubwa na Waziri wa Kilimo lakini wana imani kubwa na Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hivyo tunaomba wakulima wetu wa Tumbaku waendelee kulipwa kwa dola kama utaratibu ambao tumejiwekea kwenye Halmashauri ya Tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukuomba, Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo hapa, kuhusu Kahama. Kahama ningeomba tuitenge kuwa lango la biashara kwa Kanda wa Ziwa pamoja na nchi za maziwa makuu kwa sababu ninavyoongea tu mawasiliano katika Manispaa ya Kahama ni makubwa. Nikikutajia tu hapa na wewe unaweza ukajua kwamba kweli Kahama inastahili kuwa lango la kibiashara kwa sababu wakulima wetu na viongozi wetu na wananchi wetu sio lazima waende Kariakoo kuhemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatakiwa sasa kanda ya ziwa na sisi tuwe na ukanda wetu tutengeneze Kariakoo katika ukanda wa maziwa makuu. Ukiangalia mwaka 2019 Manispaa ya Kahama ilikusanya bilioni saba, mwaka 2021 walikusanya mapato katika Manispaa ya Kahama bilioni 9.6, mwaka 2022 walikusanya bilioni 9.6 na mwaka 2023 Kahama wamekusanya zaidi ya bilioni 10 kwa miaka mitatu Kahama imekusanya zaidi ya bilioni 35. Iweje sasa tusiitenge kuwa ni lango la kibiashara? Kuna eneo limetengwa Dodoma ukienda wafanyabiashara wamejaa pale wengi zaidi ya 1,500. Biashara zilizosajiliwa tu Kahama ni zaidi ya 8,558.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tu magari ya nchi jirani yanayopita Kahama kwa siku ni zaidi ya 446 mpaka 600, na yanayolala pale Kahama ni zaidi ya magari 200. Kwa nini tusifanye Mji wa Kahama kama lango la kibiashara kwa ukanda wa maziwa makuu ili makusanyo ya kodi na mtandao wa kodi kwenye Serikali yetu uwe mkubwa? Kwa sababu tunaangalia wananchi wengi wanakwenda kuhemea mpaka wafike Kariakoo, mpaka waende Dar es Salaam. Wananchi pia na wafanyabiashara wanaposafiri kwa muda mrefu gharama za uendeshaji inaongezeka na biashara zina bei zao zinaongezeka lakini wanapoishia Ukanda huu wa Kahama, ina maana biashara yetu, wafanyabiashara na wakulima wanaweza wakaendelea na vitu vyao hapa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niendelee kukuomba Mheshimiwa Waziri…
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Cherehani, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.
TAARIFA
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji Mheshimiwa Cherehani kwamba Mji wa Kahama pamoja na biashara kubwa zinazokuwepo pale Kahama sasa hivi wapo maafisa wa TRA ambao si waadilifu na wanadharau mpaka kauli za viongozi wa Taifa kwamba habari ya kudai kodi za miaka mitano nyuma hizo ni kauli za kisiasa. Kahama ndiyo yanayofanyika, wanataka kuuwa ule Mji wa Kahama, naomba uendelee Mheshimiwa Mchangiaji.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Cherehani, taarifa unaipokea?
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa wananchi wa Kahama wanalalamika, wafanyabiashara wanalia na akina mamantilie wanateseka. Na kwa kuwa Rais wetu ni msikivu na Waziri wa Fedha uko hapa, ninaomba tenga muda, kaa na wafanyabiashara wa Kahama wasikilize ni wachangiaji wazuri sana wa mapato ya Serikali. Kama ni madeni yaliyoko kwa wafanyabiashara waiteni mzungumze nao, waiteni muwasikilize, walipe kidogokidogo. Na, nikupongeze juzi ulisema wafanyabiashara wasifungiwe biashara zao, akina mamantilie wasifungiwe biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mamantilie anauza nyanya, anauza biashara yake ya hoteli anafungiwa anawekewa seal sasa baada ya siku mbili, tatu ndio wanaenda kumfungulia. Hebu niambie zile nyanya zinakuwa na hali gani? Kama ni kanyama ka kuku kale katakuwa na hali gani? itakuwa imeshaharibika mama amekopa kwenye halmashauri, akina mama wamekopa benki. Tunaomba Serikali ipo ilifanyie kazi, biashara Mji wa Kahama uendelee kukua kwa kuwa ni tegemeo kwenye ukanda wa maziwa makuu nchi za maziwa makuu pamoja na mikoa yetu ya Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naunga mkono hoja nishukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ahsante. (Makofi)