Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kuunga mkono mapendekezo ya maazimio haya yote mawili, Azimio la kwanza la Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Ruaha na Azimio la Kushusha Hadhi Hifadhi ya Kigosi kwenda kuwa Hifadhi ya Misitu ya Kigosi.
Mheshimiwa Spika, ninampongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nia njema na ya dhati ya kutaka kutatua migogoro mbalimbali kati ya hifadhi na wananchi. Tukianza na mgogoro wa Mbarali, mgogoro wa Mbarali ni mgogoro mrefu wa tangu mwaka 2008 ilipowekwa GN ya 28.
Mheshimiwa Spika, tukianza na mgogoro wa Mbarali, mgogoro wa Mbarali ni mgogoro mrefu wa tangu mwaka 2008 ilipowekwa GN ya 28. Mheshimiwa Rais alituma Mawaziri nane kwenda kutatua mgogoro huu, vilevile viongozi wakubwa wa Serikali, akiwemo Waziri Mkuu, walikwenda pia Mbarali katika kutatua tatizo hili la mgogoro wa Mbarali. vilevile Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, aliamua kutoa hekta 74,432.12 na kuwapa wananchi ili waweze kuendelea na shughuli za uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, mama yetu ana nia njema, ana nia ya dhati, tumuunge mkono. Ametoa pesa nyingi, vigingi vimewekwa, mipaka imewekwa ili kuzuia uvamizi na kuweza kudhibiti migogoro isiweze kuendelea tena.
Mheshimiwa Spika, kwa nia hii njema, ya dhati, ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameionesha, naiomba Serikali sasa tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa kutekeleza haya yafuatayo; ombi la kwanza, Serikali itayarishe mipango na utaratibu wa uwekezaji ambao unaonesha tarehe na lini zoezi litakwenda kuisha sambamba na kukamilisha zoezi hili la wakati.
Mheshimiwa Spika, ombi langu la pili kwa Serikali; tathmini ifanyike haraka, walipwe fidia wale wote ambao wamekutwa kwenye mpaka huo wa Hifadhi ya Ruaha ili kuweza kupisha na waweze kuondoka. Fidia zao zilipwe kwa wakati. maana yake matatizo huwa yanakuja kuanza hapa kwenye kuchelewesha fidia, mmalize ili mambo yaweze kuendelea.
Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia kushusha hadhi Hifadhi ya Kigosi na kuweza kuruhusu Hifadhi hii ya Kigosi kuwa Hifadhi ya Misitu ya Kigosi. Kwenye Kamati mara nyingi tumekuwa tukilalamika kwamba TANAPA ina mzigo mkubwa wa kuendesha hifadhi hizi.
Mheshimiwa Spika, TANAPA ina takribani hifadhi 22. Tangu ilivyokuwa na hifadhi 16, bado TANAPA walikuwa na bajeti ya bilioni 104, hifadhi zikaongezeka kuwa 22, TANAPA wakawa wanapewa bilioni 111. Hitaji halisi la pesa ili TANAPA waweze kuendesha hifadhi hizi ni takribani bilioni 222.
Mheshimiwa Spika, kwa uhaba wa pesa ambazo wanapewa TANAPA kuendesha hifadhi hizi, naona suala hili ni muhimu, linaendelea kushusha gharama za uendeshaji wa hifadhi za TANAPA. Ukizingatia kwamba Hifadhi hii ya Kigosi mwaka huu wamekwenda watalii 10 tu, kwa hiyo, mapato ni madogo na uendeshaji TANAPA inalemewa mzigo.
Mheshimiwa Spika, vilevile nimpongeze Rais kwa kuona umuhimu wa kushusha Hifadhi hii ya Kigosi kwa sababu hifadhi hii inakwenda kuwa Hifadhi ya Misitu ya Kigosi, itaruhusu wananchi kuweza kufanya shughuli za uzalishaji ikiwa ni pamoja na kurina asali, uvuvi na kufanya shughuli zao za matambiko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuruhusu uzalishaji wa asali kuendelea itatusaidia vile viwanda vyetu tulivyovianzisha vya asali kupata malighafi ya asali kwa wingi. Kwa hiyo, malighafi hii itakwenda kulisha viwanda vyetu vya asali na yale mazao ya asali tutaweza kuyauza nje ya nchi na Serikali itapata pesa za kigeni, na inasemekana kwamba tutakwenda kupata takribani dola milioni 50 kwa kuruhusu shughuli hizi za uzalishaji wa asali ndani ya Hifadhi hiyo ya Misitu ya Kigosi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo, nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kutatua migogoro, sambamba na kuona matumizi sahihi ya Hifadhi hii ya Misitu ya Kigosi ambayo itakwenda kuleta manufaa zaidi kuliko ikiendelea kuwa hifadhi, tunapata watalii wachache, na pesa tunapata kidogo na TANAPA inapata mzigo mkubwa wa kuhudumia hifadhi hii.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuongea haya machache, naunga mkono hoja ya mapendekezo haya yote mawili. Ahsante. (Makofi)