Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo amejionesha kwa vitendo kwamba anapenda amani kwa sababu anakwenda kutatua migogoro. Na naunga mkono maazimio yote mawili kwa sababu yana faida kubwa na tija kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yoyote yenye migogoro haitawaliki, kwa hiyo Mheshimiwa Rais anataka kuondoa migogoro. Nitaanza na mgogoro wa Mbarali; mgogoro huu umekuwepo tangu 2008 pale ilipowekwa GN 28. Baada ya GN 28 kuwekwa wananchi hawakuridhika kwa sababu kuna maeneo ya uzalishaji ambayo yalikwenda kwao.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya au nzuri kuna eneo la mwekezaji ambalo lenyewe lilibaki, eneo la Kapunga. Kwa hiyo, hili eneo lilisababisha wananchi waone kama wao hawakutendewa haki. Kiukweli eneo hili lilibaki kwa sababu lina miundombinu mazuri ya maji, kwa hiyo, maji hayapotei.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Kamati tumekwenda pale tumejionea na tumeridhika na yale maamuzi. Lakini ili kuondoa mgogoro wa Mbarali, Kamati tunashauri lile eneo ambalo liko sambamba na mwekezaji ambalo ni Mpunga Mmoja ambapo maeneo yote haya mawili awali yalikuwa ya wananchi, wananchi waliyatoa yale maeneo bure kwa ajili ya mwekezaji, basi nalo liwekewe miundombinu ambayo itasababisha maji yasipotee, na eneo hili wananchi walitumie kwa kilimo. Hili likifanyika wananchi wa Mbarali wameelewa kabisa na wanaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais kwa sababu wanaona kabisa uharibifu unaotokea.

Mheshimiwa Spika, tumejionea jinsi gani uharibifu unatokea katika hili Bonde la Ihefu. Hili beseni ambalo tunasema ni la maji, maji hakuna, yamekauka, maji yapo kidogo sana. Kwa hiyo, hii inakwenda kuathiri uzalishaji wa umeme Kidatu na Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatua hizi ambazo Serikali imechukua ni mahususi, tunaunga mkono asilimia 100 kwa sababu miradi hii imetumia pesa nyingi, Rais Dkt. Samia ameweka pesa nyingi kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. Bila kufanya hivi basi bwawa hili halitazalisha.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mbarali wanatambua kwamba wanahitaji umeme. Tunachotakiwa kufanya tusimamie yale tuliyoyaamua sasa. Tunayasimamia vipi, basi hivi vigingi viwekwe mahali pote ili mipaka iimarishwe. Kwa sababu bila mipaka kuimarishwa siku ya siku wananchi watarudi.

Mheshimiwa Spika, tumeona mpaka ng’ombe wameanza kwenda kule. Kwa hiyo, hii mipaka isipoimarishwa uharibifu utaendelea kufanyika katika Bonde hili la Ihefu. Kwa hiyo, miradi yetu ya umeme itaharibika. Tutaharibu mazingira yote, maji hayatapatikana ambayo yanatiririka kwa ajili ya kwenda kwenye Mto Ruaha.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali pia iweke mkuza kuzunguka yale maeneo muhimu, na siyo huko tu, nchi nzima, ili haya maeneo yetu tuweze kuyadhibiti kwa sababu tunavyokuwa tumelegalega ndiyo wananchi wanaingia, kuwatoa tunawatoa kwa gharama kubwa sana. Kwa hiyo, tuhakikishe kwamba tumejikinga kabla ya hatari ili wananchi wasiweze kuingia.

Mheshimiwa Spika, ushirikishwaji ni kitu ambacho wananchi wametuambia, wanaomba kushirikishwa. Washirikishwe kuanzia awali, waelimishwe ili wasione kama Serikali inawaonea, ili wasione kama Serikali inapendelea wawekezaji, ili wasione kwamba Serikali inawanyanyasa; waelimishwe na wapate elimu ya kutosha wao na wawakilishi wao.

Mheshimiwa Spika, sisi tulipata bahati ya kukutana na Madiwani na hili waliliongelea, kwamba sisi ni Madiwani, tukielewa tutawafahamisha wananchi wetu. Kwa hiyo, wawakilishi na wananchi wafahamishwe ili wananchi wetu waweze kuelewa.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumesikia, kuna vijiji vitano vitaondoka kabisa. Hawa watu wapewe fidia kwa wakati kwa sababu sasa baada ya kuambiwa kwamba wao wanaingia kwenye hifadhi hawawezi kuendelea kufanya chochote, hawawezi kuendelea kulima wala kuendeleza maisha yao. Kwa hiyo, watakuwa wamesimama, kama ikichukua muda mrefu basi wananchi hawa wataingia hasira na Serikali na kusababisha migogoro.

Mheshimiwa Spika, kwa juhudi hizi alizozifanya Mheshimiwa Rais, na hayo niliyoyasema yakizingatiwa, basi tuna uhakika kwamba bonde letu litaendelea kuwa salama, umeme utapatikana na migogoro itaisha.

Mheshimiwa Spika, niongelee Kigosi, Kigosi pia tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anajali wananchi wake. Haya matatizo ya wafugaji nyuki kukosa mahali pa kuweka mizinga yapo katika mapori mengi, ikiwemo Kigosi, hata Moyowosi kule ambako ni hifadhi ya wanyamapori, hii shida ipo.

Mheshimiwa Spika, ikishakuwa hifadhi, wananchi wetu ambao walikuwa wanafuga nyuki hapo awali kwenye hiyo misitu wanakosa pa kuweka mizinga. Kwa hiyo, kwa hatua hii ya Mheshimiwa Rais kuruhusu kwamba hii ishushwe hadhi ina maana wananchi wanaruhusiwa kufanya shughuli zao. Watafanya shughuli hizo za ufugaji nyuki, watafanya shughuli za uvuvi na za matambiko.

Mheshimiwa Spika, tunaomba sasa Serikali kufanya uratibu mzuri kwa sababu bado ni hifadhi ya misitu, bado tunahitaji kulinda misitu yetu, haimaanishi misitu ikatwe sasa, hapana, ametoka TAWA lakini sasa TFS anachukua charge.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba Serikali iweke uratibu mzuri na hasa wa zile tozo. Tozo zieleweke; anayekwenda na baiskeli anakwendaje, na pikipiki anakwendaje, kwa sababu hizi tozo pia ni moja ya sehemu ambazo zinapigiwa kelele.

Mheshimiwa Spika, tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais, anawajali wananchi wake ndiyo maana anaachia maeneo, maeneo yote anayoachia anasema wapelekewe wananchi kwa sababu anataka waweze kuendelea na uzalishaji. Amerudisha maeneo hifadhi hii iwe na misitu ili viwanda viweze kufanya kazi ili sasa wananchi waweze kuweka mizinga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunasema sisi sasa hivi ondoa shoka uweke mzinga. Kwa hiyo tunaamini miti yetu sasa badala ya kukatwa, mtu hawezi kukata kwa sababu yeye mwenyewe anataka kuweka mzinga, kwa hiyo, kwa kuwashirikisha wananchi wao wenyewe watakuwa ni wahifadhi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa haya machache, naunga mkono hoja. Naipongeza Serikali, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa ushirikiano mkubwa aliotupa; Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima. Wao ndio wamesababisha tuweze kuratibu jambo hili na tuweze kufika hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)