Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia Maazimio mawili yaliyoletwa hapa na Kamati yangu. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai mpaka sasa tumekaa hapa miezi mitatu tupo hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuchangia suala la Azimio la Bunge la kuridhia kufutwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi na kuruhusu kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi. Napenda nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa na Naibu wake, Mheshimiwa Masanja lakini na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri waliyoifanya mpaka tumefikia leo hapa tupo kwenye majadiliano ya Azimio hili.
Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kufutwa Hifadhi ya Kigosi na kuanzisha Hifadhi ya Msitu wa Kigosi. Ninazo sababu za kumpongeza, kwa sababu inapokuwa hifadhi wananchi hawaruhusiwi kuingia ndani ya hifadhi, lakini inapokuwa hifadhi ya misitu wananchi wa eneo hilo wataweza kupata fursa za kuingia kwenye hifadhi na wataweza kwenda kufanya shughuli zao za kijamii kama kutundika mizinga, kuvua samaki lakini pia na kufanya mambo yao ya asili kama matambiko.
Mheshimiwa Spika, eneo hili ni kubwa ni kilometa za mraba takribani elfu saba mia nne na kitu. Ni eneo kubwa ambalo wananchi wanaozunguka maeneo hayo watafaidika nalo. Pia eneo hili linakwenda kuifungua nchi kiuchumi kwa sababu tunaweza kupata wawekezaji wakawekeza hata kwenye mambo ya hewa ya ukaa. Mbali na hapo kutakuwa na viwanda, viko kule viwanda vitano ambavyo vinachakata mazao ya asali kama nta, lakini asali pia inapouzwa nje ya nchi inaleta pesa za kigeni na wananchi wanapata manufaa kutokana na mazao hayo.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita na nalipongeza azimio hili na naunga mkono kuwepo kwa azimio hili na naomba Wabunge wenzangu waliunge mkono kwa faida ya wananchi na faida ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kupongeza Azimio la Ruaha kwa sababu linakwenda kutatua matatizo yaliyopo pale Ruaha, lakini pia ni faida kwa wananchi kwa sababu maji yanayotokana hapo yanakwenda kujaza Ziwa la Kidatu na pia yanakwenda mpaka Ziwa la Mwalimu Nyerere ambako Serikali imewekeza mradi mkubwa kwa ajili ya kufua umeme.
Mheshimiwa Spika, eneo hili ni eneo ambalo maji yanayokwenda kwenye Ziwa la Mwalimu Nyerere yanatokea sehemu hiyo. Hivyo basi, kupitishwa kwa azimio hilo kutasababisha yale maji yaweze kuwepo kwa wingi na kwenda kwenye Ziwa hili ambalo litatengeneza umeme mwingi ambao tutaweza pia kuuza hata kwenye nchi za jirani.
Mheshimiwa Spika, kwenye Azimio hili la Ruaha, niombe sana wale watendaji ambao watakuwa wanakwenda kutekeleza ile mipaka wawe marafiki na wananchi wa maeneo hayo. Vilevile niombe Wizara ya Maliasili na utalii, sisi kama Kamati tulikuwa tumeomba sehemu ya eneo ambalo liko karibu na yule mwekezaji mkubwa Kapinga One, wananchi wapewe hilo eneo ili na wao waweze kuendeleza shughuli zao za kilimo kwa sababu hili eneo limeleta mgogoro maana yake wapo wananchi wanaolalamika kwamba kwa nini yule mwekezaji ameachwa pale. Tuliomba na yeye eneo lake la juu, tulikubaliana kwamba waweze kwenda kupima lile eneo la Kapinga one wananchi waweze kugawiwa ili nao waweze kufanya shughuli zao za kilimo.
Mheshimiwa Spika, viko vitongoji ambavyo vimechukuliwa vitakuwa ndani ya hifadhi kwa maana kwamba vile vijiji vitano vinaenda kufa kama vijiji. Ombi langu kwa Wizara ni hili, wale wananchi walioko kwenye hivyo vijiji na vitongoji vinavyoenda kufa, wafanyiwe uthamini wa mali zao waweze kulipwa haraka iwezekanavyo. Pia kama Serikali itaona jicho la huruma, iweze kuwaonesha sehemu nyingine ili wananchi hawa waweze kwenda kujenga nyumba zao kwa sababu vile vijiji na vitongoji vinakufa. Viko vijiji vitano vinaenda kufa kabisa kwa sababu vitakuwa ndani ya hifadhi, lakini pia vipo vitongoji vingine ambavyo vinaenda kufa.
Mheshimiwa Spika, tuombe malipo yao yaharakishwe na sio Sheria ipite hapa Bungeni halafu inapofika wakati wa malipo ije iwe shida. Jambo hili litaleta mgogoro kwa wananchi kwa sababu kama umechukua eneo, basi ni wajibu wa Serikali kufanya uharaka wa kulipa hayo maeneo ambayo watakuwa wameyachukua, lakini kuwaangalia wananchi kwa jicho la huruma waweze kuwasaidia kupata maeneo mengine ya kuishi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza ni suala la vibali. Niombe sana hawa Idara ya Misitu ambao wanakwenda kuangalia hii Hifadhi ya Misitu ya Kigosi waangalie jinsi ya kutoa vibali. Vibali visigeuke kuwa manyanyaso kwa wananchi, wanapokwenda kuomba vibali kwenda kutundika mizinga au wanapokwenda kuomba vibali vya kwenda kuvua samaki, basi wale wafanyakazi wawe rafiki kwa wananchi ili kutoa migogoro ambayo inaweza kutokea kati ya wale wahifadhi wanaolinda hiyo misitu, watu wa TFS pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Spika, hapa Azimio linaweza likapita kwamba ni azimio rafiki ambalo Mheshimiwa Rais amelileta linalokwenda kuwafaidisha wananchi, lakini pia linaweza likageuka likawa kitega uchumi kwa yule Mhifadhi ambaye atakuwa analinda ule msitu. Kwa hiyo ombi langu ni kwamba, wale wahifadhi ambao watakuwa wamepewa jukumu la kutoa hivyo vibali wawe rafiki kwa wananchi ili hivyo vibali visije vikageuka tena vikawa ni kitega uchumi cha Mhifadhi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine la mwisho kabisa ambalo nataka kulizungumza hapo, niombe wale wataalam wetu wanapokwenda kwenye maeneo haya yote ya Hifadhi ya Kigosi lakini pamoja na kule Ruaha wakawe marafiki na wananchi, waitishe mikutano, sio mwananchi anaamka asubuhi anakuta mpaka umewekwa, ni bora mikutano wakashirikisha Wenyeviti wa Vijiji pamoja na wananchi kwa kuitisha mikutano ya hadhara na wananchi waone ile mipaka inavyowekwa.
Mheshimiwa Spika, naona umewasha taa, naomba kuunga mkono hoja suala la Azimio la Hifadhi ya Kigosi pamoja na Azimio la Ruaha. Ahsante. (Makofi)