Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, ninachukua fursa hii kukushukuru lakini na mimi pia nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhati kabisa ya kutuletea Maazimio haya mawili muhimu sana. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Kaka yangu Mohamed Mchengerwa, kwa jambo hili muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, mimi nianze kwa kueleza kuwa mwaka 2018/2019 nilibahatika kuwa katika timu ya awali ya Mawaziri Nane ambao tulipewa jukumu la kwenda kuangalia migogoro ya vijiji 925. Maeneo yote haya mimi nilipata fursa ya kuyatembelea.

Mheshimiwa Spika, katika migogoro yote ambayo inafahamika, jambo kubwa linaloonekana ni kwamba, wahifadhi wanasimamia Sheria lakini pia wananchi ambao tunasema wanavamia, wanalazimika kuvamia kwa sababu hayo ni mahitaji yao ya msingi kulingana na mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kusema nini? Maazimio haya mawili kuja, nadhani ni mpango mzuri ambao hata mimi sikuutarajia katika kipindi kile na hata kipindi hiki ambacho tunaendelea, kwamba sasa hivi tunapoamua kwa mfano, tumeeleza Azimio la kurekebisha mipaka pale Mbarari kwenye Ruaha Mkuu, Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri sana faida ya kurekebisha mipaka. vilevile, siyo kurekebisha tu, wameamua kugawa eneo kilometa za mraba 478, hili ni jambo kubwa sana na Mheshimiwa Waziri ninakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya msingi hapa nyepesi sana ambayo ni mahusiano katika ya wananchi wa Mbalali na Wahifadhi. Sasa, kugawa tu maeneo inaweza isitoshe, kinachoweza kutusaidia sisi kama Serikali lakini sisi kama wananchi, tukae pamoja tukubaliane na tuwe na mahusiano mazuri kati ya wahifadhi na sisi ambao tunahitaji kutumia maeneo yale. Tofauti na hapo maana yake tutakuwa hatujatatua tatizo la Msingi.

Mheshimiwa Spika, tunajua hapa kuwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere tunategemea maji kutoka katika Ruaha Mkuu, pia imetajwa Kidatu na maeneo mengine kote, watakaolinda maeneo haya ni wananchi na siyo wahifadhi peke yake, lakini kama wao ndiyo wanalinda maeneo haya, tunatarajia kuona Serikali inawaunganisha wananchi na wahifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Hifadhi ya Taifa ya Kigosi, historia imeelezwa vizuri, kwamba awali lilikuwa pori, ikawa hifadhi ya misitu na baadaye ikawa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi. Kwa nini? Ndilo eneo ambalo limehifadhiwa vizuri. Sasa umefika wakati ambao ndiyo mimi naipongeza Serikali imekuja na njia nzuri ya kuhakikisha kwamba wananchi watakuwa na sehemu ya kutumia lakini pia Serikali itakuza uchumi kupitia hifadhi hii ya Kigosi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hili na maeneo mengine ni muhimu sana. Tunazo hifadhi nyingi na sisi kule Mugori pia tunahitaji eneo hili liweze kuhifadhiwa lisibaki kuwa ni hifadhi ya misitu lakini pia liende kuwa Hifadhi ya Taifa na hata baadae kurudi kuwa hifadhi ya misitu ni jambo jema kwa sababu ya matumizi ya binadamu.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano; hata kule Kagera Nkanda nilishawahi kufika. Ule msitu wa Kagera Nkanda ule msitu ni mkubwa sana. unaweza kuutazama ukaona kwamba msitu umehifadhiwa, lakini kule katikati tayari kuna kilimo, ufugaji na vinginevyo kiasi kwamba kuna uharibifu mkubwa sana wa mazingira. Sasa, maeneo kama haya Serikali inapokuja na mpango kama huu ni vizuri ikaangalia maeneo yote ambayo yana changamoto ili tuweze kushirikishana kwa pamoja, wananchi wapate sehemu ya kuweza kufuga, kulima kwenye hifadhi hiyo hiyo lakini pia na hifadhi iweze kuendelea.

Mheshimiwa Spika, ninataka kushauri nini hapa? jambo la kwanza ni elimu. Tunatunga Sheria lakini pamoja na kutunga sheria wananchi wanahitaji waeleimishwe namna ya kuhifadhi mazingira, namna ya kushiriki katika hifadhi zetu hizi kwenye kilimo na shughuli nyingine. Usipotoa elimu kama Serikali utakuwa haujatatua tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni hifadhi ya mazingira na hifadhi ya maji. Maeneo haya yote yamehifadhiwa vizuri sana na ni vyanzo vya maji lakini mazingira yake ni mazuri sana. Sasa, tunaporuhusu shughuli za kibinadamu maana yake tumeruhusu shuguli za kuuchumi ambazo zinaweza kuleta athari nyingine kama sisi hatujchukua hatu za kuwaelimisha watu wetu kwamba, athari hii ikitokea maana yake turekebishe isitokee tena athari nyingine, turudi hapa tuone kuwa tulichokiamua hakiko sawa.

Mheshimiwa Spika, jambo hili ni la msingi sana na niiombe Serikali kabla haijaamua kuanza kufanya iende ikatoe elimu na ijue hapa tunahitaji kuhifadhi mazingira na hapa tunahitaji kuhifadhi maeneo ya maji ili wananchi wetu waweze kujua jukumu lao kubwa na maisha yao yanategemea hizi hifadhi.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningependa nishauri ni matumizi bora ya ardhi. Kamati imeseama vizuri na niwapongeze kwa kazi nzuri. Matumizi bora ya ardhi ni eneo muhimu sana ambalo wenzetu wa Wizara ya Ardhi nao wanapaswa kushirikishwa ili waende kutoa elimu ya matumizi bora ya ardhi. Hatuwezi kufika na kusema tu eneo hili litakuwa ni eneo la kichumi, eneo hili litakuwa ni eneo la hifadhi lakini matumizi yake tunatumiaje?

Mheshimiwa Spika, wenzetu ambao tumewapa hii sheria waweze kuismamia nao washiriki kwa ajili ya kutoa elimu ya matumizi bora ya ardhi badala ya kuachia tu jambo hili likaenda kiholela na baadaye kurudi kuanza kutatua mgogoro wa ardhi, hii inaweza kutuletea changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia hata katika hiyo mipaka tunapoamaua kwenda kuweka alama (beacons) wananchi wawepo, tusizungumze tu kwamba tumetenga eneo la kilometa za mraba 478 lakini tunapokwenda kule wenzetu wakaamua kusogeza kwa sababu wananchi hawapo hii itatuletea changamoto. Wananchi wawe sehemu ya kuweka mipaka ambayo na wao wataiheshimu ili kesho tukirudi sisi tusiwe sehemu ya hiyo migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikushukuru sana na niendelee kukupongeza, miezi minne siyo jambo dogo, sisi tumekaa hapa tumekupa ushirikiano na kwa kweli tukutakie kila la heri kwenye safari yako hiyo ya kidunia. Wewe ndiyo utakuwa icon ya Tanzania. Icon hii tunaitarajia na wewe kufikisha ujumbe, hata wenzetu wa maliasili na wengine tunataka tuone wanakuunga mkono kwa sababu uwepo wako kule Serengeti itajulikana, kila kitu kitajulikana na Tanzania itajulikana vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mungu akubariki sana na ninaunga mkono Azimio hili, ahsante sana. (Makofi)