Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

Hon. Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nisiwe mchoyo wa fadhila, nianze kwa kumpongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo amesimamia mazoezi haya ya migogoro, hatimaye leo tumeanza sasa harakati za kuleta maazimio ili turekebishe baadhi ya maeneo. Nampongeza kwa moyo wa dhati kwa sababu hata Wabunge wenyewe wamekiri leo kwamba safari ilikuwa ni ndefu, lakini hatimaye tunaanza kuiona nuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe umekuwa ukitusimamia vizuri sana, miongozo ni mingi sana iliyokuwa inatoka humu Bungeni ikihusiana na maeneo haya yenye migogoro, lakini umetusimamia vizuri sana. Tunakupongeza na tunakuahidi kwamba tutaendelea kushirikiana na Wabunge na wewe binafsi ili kuhakikisha kwamba tunaitendea haki Serikali lakini pia tunawatendea haki Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, naendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameendelea kutusimamia kutuongoza pale ambapo tunakwama ametuonyesha njia. Tuendelee kumshukuru na awe na moyo huo huo pale ambapo tunamhitaji hasa kwenye harakati hizi za kutatua migogoro. Pia, niendelee kumshukuru sana bosi wangu Mheshimiwa Waziri Mchengerwa kwa namna ambavyo tunaendelea vizuri kuyaangalia haya maeneo, lakini pia kwa hatima ya zoezi hili la kupitisha haya Maazimio mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikumbuke tu na kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati yetu, Makamu Mwenyekiti lakini na Waheshimiwa Wajumbe. Hawa wamekuwa nguzo, wametupa maelekezo mahususi, wametusimamia na hatimaye leo tumeingia Bungeni tukiwa kifua mbele tukitetea Maazimio hayo mawili. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge na tunakiri kwamba tutaendelea kushirikiana nao na yale maelekezo yote ambayo wametupa kwenye Kamati na hata yaliyotoka kwenye ripoti yao hapa tumeyapokea na tutaendelea kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge wamechangia, tunawashukuru sana kwa michango yao mizuri na tunaendelea kuwaomba waendelee kutuelekeza ili tuendele kufanya kazi nzuri ili Watanzania wapate haki yao, lakini pia Serikali iendelee kuhifadhi na kulinda rasilimali za Taifa kwa maslahi ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, ningependa nitoe mchango wangu katika maeneo mawili, eneo la kwanza linahusiana na Azimio la Kushusha Hadhi Pori la Hifadhi ya Taifa Kigosi kuwa Forest Reserve. Kwenye Sekta yetu hii ya Maliasili na Utalii tumekuwa na mchakato mzima wa uanzishwaji wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu hususan mazao yanayotokana na nyuki. Tuna viwanda 97 nchini, lakini tuna viwanda sita katika Wilaya ya Mlele, Kibondo, Bukombe, Nzega, Sikonge na Manyoni. Hivi viwanda vipo kwa ajili ya kuchakata asali na viwanda hivi vipo kwa ajili ya kutegemea rasilimali inayotokana na mazao yanayotokana na nyuki.

Mheshimiwa Spika, niliwahi kutembelea Wilaya ya Bukombe, wazalishaji wakubwa wa zao la asali na ni moja ya wilaya hizi nilizozitaja. Changamoto tuliyoikuta pale ni kwamba tulikuwa tunawaondoa wale wananchi waliomo ndani ya hifadhi, kwa sababu hifadhi hii imepanda hadhi kuwa National Park. Nakumbbuka nilifanya ziara na tukaomba pamoja na kuwa nature ya reserve ile imeshazuia shughuli za kibinadamu lakini uzalishaji wa mazao ya nyuki ulikuwa ni wa hali ya juu. Kwa bahati nzuri kabisa Serikali imepeleka kiwanda pale na kiwanda kinazalisha vizuri na wananchi uchumi wao umeimarika, Watanzania wanapata ajira kutokana na mazao hayo. Kwa hiyo tuliweza kuwaruhusu hawa wananchi waendelee kurina asali na kufuga nyuki, lengo lake ni kuwafanya waendelee kuzalisha mazao hayo.

Mheshimiwa Spika, kushuka kwa hadhi ya mapori haya, kutasaidia sana wananchi kuimarika kiuchumi, kimapato, lakini pia tunaamini ajira za Watanzania zitaendelea kuongezeka. Eneo hili linazungukwa na mikoa minne, Mkoa wa Kagera, Mkoa wa Geita, Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Shinyanga. Kwa hiyo kushuka kwa hadhi kwa pori hili kutasaidia mikoa minne iende kufaidika na mazao ya uchakataji wa asali lakini yanayotokana pia na nyuki.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili lingine la Azimio la Ruaha pia niendelee kukushukuru, niwashakuru Wabunge kwa namna ambavyo wamelipokea vizuri. Kama ambavyo nimesema mwanzo, eneo hili limekuwa na mgogoro wa muda wa siku nyingi, lakini niwapongeze sana Kamati ya Mawaziri nane. Tumeenda mara kadhaa kule lakini hatimaye leo tumeleta azimio Bungeni. Kuna mawazo mbalimbali yametolewa na Waheshimiwa Wabunge ikiwemo kuendelea kuwashirikisha wananchi, lakini pia wametuomba sana mipaka iweze kuonekana kwa uwazi zaidi na iwe shirikishi kwa wananchi. Tunaahidi kwamba tutaendelea kuwashirikisha wananchi, lakini pia mipaka tutaweza kuiweka kwa ufasaha kabisa ili kila mtu aone na eneo hili liweze kuhifadhiwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amekubali kupunguza eneo hili kuwaachia wananchi hususan wakulima na tunaendelea kuwaomba wananchi kwamba kila ambacho kinaombwa Mheshimiwa Rais anawasikiliza na anatekeleza. Kwa hiyo tuendelee kushirikiana pamoja na Serikali tuendelee kushirikiana pamoja na Mheshimiwa Rais na tuendelee kumuunga mkono ili migogoro hii ifikie hatma na hatimaye tuweze kuendeleza rasilimali hizi tulizoachiwa na waasisi wetu kwa maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)