Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya na uzima na kutuwezesha kukutana mbele ya Bunge lako hili Tukufu.
Mheshimiwa Spika, pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ridhaa yake yeye mwenyewe kuona umuhimu wa utekelezaji wa maazimio yote haya mawili na haya ndio maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndio yanatoa muelekeo wa Serikali na kututaka sisi kama Serikali kuangalia maslahi ya Watanzania, hasa Watanzania wa kawaida kabisa. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe tu kwamba michakato hii hasa ya maazimio haya haikuanza chini ya utawala au uongozi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, yalianza na viongozi waliomtangulia na sasa ni takribani zaidi ya miaka saba, tumehangaika tumekwenda na kurudi. Sisi kama Serikali tumejitahidi katika nyakati zote kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hizi hasa za wananchi wetu hawa wa kawaida, kuwapatia maeneo ambayo watakwenda kuyatumia kwa maslahi yao.
Mheshimiwa Spika, tatu, nikushukuru sana wewe na Kiti chako kwa kuendelea kutupatia miongozo mbalimbali, lazima nikiri mafanikio na leo sisi kama Serikali kuwepo hapa ni kwa sababu ya miongozo yako, jitihada zako, kuhakikisha kwamba unasimama vyema kusimamia yale yaliyoelekezwa katika Ibara ya 63 na Ibara ya 64 na mengine katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunakupongeza sana kwa sababu kuna wakati kulikuwa kuna giza kidogo lakini ukasema unataka kuona mwanga. Hayo yote uliyoyafanya kwa sababu ulizingatia maslahi ya wananchi ambao wao ndio wametuweka hapa Bungeni, tunakupongeza na tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba dhamira ya Serikali yoyote, Serikali yoyote halali, dhamira ya Serikali yoyote iliyo madarakani, Serikali yoyote makini, ni ustawi wa wananchi wake, ndio dhamira ya Serikali yoyote. Serikali imepewa mamlaka yake na wananchi kwa misingi ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali imepewa mamlaka na wananchi kwa sababu nchi hii ni ya wananchi na wananchi wameelekezwa moja kwa moja kwa misingi ya Katiba kushiriki katika maamuzi yanayofanywa na Serikali na wananchi wanashiriki katika maamuzi ya Serikali kwa misingi iliyoainishwa katika Ibara ya 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watanzania wanashiriki kwenye maamuzi ya moja kwa moja yanayoamuliwa na Serikali. Ibara ya 21 imetoa mwongozo wa namna gani wananchi watashiriki kwenye maamuzi ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaipongeza Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, kwa sababu viongozi wa Mataifa mengine wangeweza kuamua wao wenyewe kama viongozi. Mheshimiwa Rais angeweza kuamua yeye mwenyewe, lakini akaona kwamba, Serikali ya Chama hiki ikaona kwamba ni muhimu wananchi wakashirikishwa moja kwa moja na ndio msingi ulioainishwa katika Ibara ya 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi wanashiriki kwenye maamuzi katika mikataba, katika majadiliano, katika mambo kama haya ya kupandisha hadhi hifadhi na kuzishusha hadhi hifadhi. Ibara ya 21 imetoa maelekezo ni namna gani wananchi watashiriki kwenye maamuzi ya Serikali na namna ambavyo wananchi wanakwenda kushiriki kwenye maamuzi ya Serikali ni kupitia wawakilishi wa wananchi waliochaguliwa na wananchi wao na hao wawakilishi ndio hao tunaowazungumzia, Waheshimiwa Madiwani na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wametoa maoni mengi sana katika maeneo yote haya mawili, eneo la Kigosi lakini pia eneo la Ruaha, nasi kama Serikali tumesikiliza maoni ya Waheshimiwa Wabunge. Kwanza tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, katika maoni ya Waheshimiwa Wabunge, Wabunge takribani 10 wote wameunga mkono Maazimio. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia taarifa ya Kamati imeunga mkono Maazimio lakini nikushukuru pale ambapo ulipoagiza Kamati hasa kwenye hoja moja ya eneo la Ruaha, ukatutaka tuende tukajiridhishe, tunakushukuru sana sana kwa sababu haukutoa mwongozo tu kwa Kamati lakini ulitoa mwongozo kwa sababu unalinda maslahi ya wananchi na hiki ndicho kilichotuleta hapa Bungeni, tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi na Kamati tulipata fursa ya kwenda kujionea kule Ruaha na yale ambayo hoja za Kamati kuhusu ni kwa nini Mwekezaji ameachwa na wananchi wameondolewa. Mimi nilipata fursa ya kujionea hali hii na Wajumbe wa Kamati, tulifanya vikao kadhaa na baadae tukaenda site kujionea hali halisi, niliporejea niliwaambia wenzangu kwamba sisi ni wawakilishi wa wananchi lakini pia kilichofanyika pamoja na jitihada kubwa na kazi nzuri ambayo imefanywa na Waheshimiwa Mawaziri Nane waliozunguka kuhakikisha kwamba wameyaangalia maeneo yale ambayo hayana hadhi wakapendekeza yaondolewe, ni lazima tuwapongeze kwa kazi kubwa na kazi nzuri sana ambayo wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakatoa takribani hekta 74,000 kwa wananchi kule eneo la Ruaha lakini baada ya kwenda kujionea eneo lile, mimi nilishawishika pia na niliporejea nikawaambia wenzangu hapa ni lazima tufanye jambo ili kulinda maslahi ya wananchi, kwa sababu hiki ndicho ambacho wananchi wametuweka hapa kwa sababu ya kulinda maslahi yao na kama ambavyo nimesema dhamira yetu sisi Serikali ni kulinda na kuendeleza ustawi wa wananchi wetu, kwa hiyo isingelikuwa na maana yoyote ya safari yetu kule Mbarali kama tusingeliweza kuliona hili na tukaona kwamba hili changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuliporejea tulifanya kikao na nimshukuru Mwenyekiti wetu nae aliridhia kwa sababu mchakato huu unapita taratibu za kisheria, taratibu za kitathmini. Sisi kama Serikali baada ya kuwa tumefanya mapitio kwa viongozi wetu tukaona kwamba ipo haja ya kuwafikiria hawa wananchi katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa michakato hii ni michakato ya kisheria, kwa kuwa michakato hii ina taratibu zake za kufanya tathmini ili tuweze kujiridhisha ni eneo gani ambalo wananchi wataweza kulitumia kwa sababu kama mwekezaji amebakizwa kwenye eneo hilo hilo ambalo tunasema ni ardhi oevu wananchi walipoondolewa, basi ili kutenda haki, mwekezaji naye alipaswa kuondoka kwenye eneo lile, lakini kama Serikali tumeridhia tunasema kwamba mwekezaji ana miundombinu ya maji kwenye eneo hili, sisi kama Serikali ni lazima tujitathmini kwamba hapa kama tumemuacha mwekezaji, ni muhimu tukalinda maslahi ya wananchi pia katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili tuliliangalia na tukasema kwamba ipo haja ya kulifanyia tathmini hili na tunafanya commitment mbele ya Bunge lako Tukufu kwa sababu Kamati imetuagiza na inapoagiza Kamati maana yake imeagiza Bunge kwa misingi ya Kanuni. Sisi tunaliomba Bunge lako liridhie kupitisha Azimio hili lakini tunaomba tuliahidi Bunge kwamba tutarejea hapa mwezi Septemba ili kufanya marekebisho tuwaangalie wananchi wa eneo lile la Mbarali ambao wameondolewa, katika maono ambayo mimi nimejiridhisha kabisa kwamba kulikuwepo na haja ya kufanya tathmini ya kina ni kwa nini wananchi wameondolewa kwenye eneo lile. Kwa hiyo, tunaomba tuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba tutarejea mwezi Septemba na kwa kuwa tumekwishampa taarifa Mheshimiwa Waziri Mkuu haja ya kufanya tathmini kuwaangalia wananchi katika eneo lile ambalo tutaleta mapendekezo iwapo Bunge litaridhia, basi eneo lile hatutalirejesha kwa wananchi kwa sababu tunajua tukilirejesha kwa wananchi watu wachache watanufaika na eneo hili. Kwa hiyo, tutalirejesha kwa Serikali pengine kupitia Mkoa au TAMISEMI au kupitia Wizara ya Kilimo ili liweke utaratibu wa kuandaa miundombinu ya maji na wananchi waweze kunufaika katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara yetu ina migogoro jumla karibu 836, na kama uliusikiliza maoni mengi ya Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, wapo wengi wamekuwa na imani na mimi. Mimi ni mtu wa field, naomba niwathibitishie katika kipimo ambacho nitaomba Wabunge wanipime ni kwenda kumaliza migogoro hii 836. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na Ndugu yangu Ole-Sendeka alikwenda nje kidogo ya hoja kuzungumza kule Jimboni kwake lakini nimpe taarifa kwamba nitafika huko Jimboni kwako. Mara nyingi huwa sipendi kuletewa taarifa mezani, ninapenda nifike kule field nijionee mimi mwenyewe ili pale tunapopeleka maoni au ushauri kwa Mheshimiwa Rais uwe ni ushauri ambao unakwenda kulinda maslahi ya wananchi hasa wanyonge kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo pamoja na migogoro hii 836 lakini tumeongezewa mgogoro mwingine jumla migogoro 837 wa kule Iringa kwa sababu ya simba ambao wameingia kwenye maeneo yetu tayari tumekwishapeleka helicopter, tumepeleka askari wetu zaidi ya 21 wapo kule wanaendelea kuwasaka wale simba, lakini migogoro hii mingine ninaomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge nitafika kila kona kuhakikisha kwamba tumetatua migogoro hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulipopewa nafasi hizi tuliaminiwa na Mheshimiwa Rais lakini ukweli ni kwamba wapo Watanzania wana uwezo mkubwa huko nje pengine wangepewa nafasi hizi wangefanya vizuri zaidi. Kwa hiyo, tuna jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba tunalinda na kutetea maslahi ya wananchi na hapa ndipo tunakiri kabisa kwamba kazi aliyofanya Rais wetu kurejesha maeneo haya kwa wananchi ni lazima tumpongeze na tumshukuru sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, walijaribu wengi lakini Rais Dkt. Samia ameweza kurejesha maeneo haya kwa wananchi. Tulisimama hapa katika hotuba ya bajeti yetu tukaeleza Mheshimiwa Rais aliendeleza yale ambayo yalianzishwa na Rasi wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ya kwenda kufanya mapitio kwenye maeneo ya migogoro na wakati nahitimisha hotuba yangu ya bajeti tulisema, kufikia Tarehe 28 mwezi wa Sita, wale waliokasimiwa mamlaka ya kuhakikisha kwamba wanatatua migogoro kwenye maeneo yao wafanye hivyo, lakini pamoja na hilo tunatambua yako maeneo mengine bado kuna vuguvugu la migogoro. Nitafika huko ili nitakapokuja kwa wenzangu tutawashauri namna bora ya kwenda kumaliza migogoro tuliyonayo kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, msingi wa hoja zetu zote mbili nimeona hapa kumekuwepo kidogo na hofu ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu kukabidhi eneo la Kigosi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Misitu chini ya TFS chini ya Sheria Namba 323. Wahifadhi wetu tulipowapa nafasi katika maeneo yao tuliwakabidhi majukumu katika misingi ya sheria ambayo nimeitaja hapa.
Mheshimiwa Spika, TFS itakwenda kuandaa mpango wa usimamizi wa misitu hasa Msitu wetu huu wa Kigosi ambao tumeuzungumza. Mpango huu utaandaliwa katika kutimiza matakwa ya Sheria ya Hifadhi ya Misitu sura Namba 323. Kwa hiyo, ninaomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, TFS hawa ni wahifadhi lakini hawa wote ni Askari Jeshi. Kwa hiyo, jukumu lao kubwa ni kulinda hifadhi ya misitu lakini pia ikumbukwe kwamba maeneo mengi yenye vyanzo vya maji wanaolinda ni hawa wahifadhi - TFS. Kwa hiyo, naomba niwatoe hofu wale wote ambao walikuwa na hofu. Hili ni Jeshi kamili, wamepata mafunzo ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, katika eneo ambalo hatutakuwa na msamaha ni wale wahifadhi ambao tumewakabidhi mamlaka ya kwenda kufanya kazi na kusimamia kwenye maeneo yao na wao wakaenda kutuangusha kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, tutatoa kipindi cha maangalizo ili tumpime kila mmoja uwezo wake, kwa namna ambavyo anakwenda kutekeleza maelekezo ambayo ninyi Bunge mtatushauri katika Kikao hiki. Kwa hiyo, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba TFS ni Jeshi kama lilivyo Jeshi la TAWA, TFS ni Jeshi kama lilivyo Jeshi la TANAPA, wanapata mafunzo sehemu moja kwa hiyo hawa ni wanajeshi na kwa marekebisho ya sheria na kimuundo ambao tumekuwa tukiendelea kuyafanya tumeendelea kuwapandisha hadhi kuwa ni Jeshi USU. Kwa hiyo niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la ushirikishwaji wa wananchi tumelipokea hili, na sisi tunakiri kabisa moja ya changamoto kubwa ambayo tumeikuta kwenye Wizara hii, maamuzi mengi yalikuwa yakifanyika bila kuwashirikisha wananchi. Hili tunalikubali kabisa, nilikwishatoa maelekezo kwa Wakuu wa Hifadhi katika maeneo yote kuhakikisha kwamba wanashuka kuzungumza na wananchi na kazi hii tumekwishaianza kwa TANAPA, TAWA na TFS. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi tunapozungumza wanapita na kuzunguka katika kila Mkoa na wanavyopita katika kila Mkoa, wanakwenda kuzungumza na Viongozi wa Serikali katika kila Mkoa, Viongozi wa Chama Tawala katika kila Mkoa ili waweze kubeba maono ya wananchi kwenye maeneo yao. Tunaamini kabisa ushirikishwaji wa wananchi utatusaidia sisi kama Wizara kwenda kutatua migogoro hii ambayo nimeitaja zaidi ya 800 inayotukabili leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limezungumzwa hapa ni kuhusu uwekaji wa alama za mipaka. Kama ambavyo nimesema na kama ambavyo tayari tumekwisha waagiza wataalam wetu wahakikishe kwamba uwekaji wa alama za mipaka unakuwa shirikishi. Nimesema hapo awali, migogoro mingi imetengenezwa kwa sababu wananchi wengi wamekuwa hawashirikishwi kwenye maamuzi. Kwa hiyo, kwa kuwa tayari tumekwishatoa maelekezo na kwa kuwa tayari wataalam wetu wanaendelea kuhakikisha kwamba wanakwenda kuwashirikisha wananchi katika utatuzi wa migogoro kwenye maeneo mbalimbali, uwekaji wa alama za mipaka ni lazima wawashirikishe wananchi na haya tayari tumekwisha waagiza wataalam wetu, katika maeneo mengi tayari hili linaendelea kutekelezwa na niseme tu kwamba nimepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge wale ambao walikuwa na hofu na hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitahakikisha katika maeneo ambapo tunaendelea kufanya tathmini ya ardhi, katika maeneo ambapo tunaendelea kufanya tathmini ya hifadhi zetu tutaendelea kuhakikisha kwamba wananchi wameshirikishwa moja kwa moja. Tunapozungumza kuhusu wananchi siyo tu viongozi wawakilishi, Wabunge na Madiwani, lakini pia mpaka chini kwenye vitongoji, kwenye vijiji na wananchi wenyewe washirikishwe kwenye vikao mbalimbali ili tunapofanya maamuzi yawe ni maamuzi ambayo hayataleta hitilafu na kuturejesha hapa katika mijadala ambayo tungeliweza kuitatua mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu utolewaji wa elimu. Tutaendelea kutoa elimu hasa katika maeneo ambayo tumeyarejesha kwa wananchi na kama ambavyo mwenzangu amezungumza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri Nane amekwishalisema hilo kwamba tutaendelea kutoa elimu ili yale maeneo ambayo yamerejeshwa kwa wananchi yaweze kutumika katika minajili iliyokusudiwa na Serikali. Kwa hiyo, hili tutaendelea nalo na nikuthibitishie tu kwamba mimi na taasisi zangu zote tunaendelea kutoa elimu na kupitia TAWA, TANAPA, TFS tunaendelea kutoa elimu, hivi sasa wanaendelea kuzunguka kama ambavyo nimesema awali na tutaendelea kutoa mafunzo kwa askari wa vijiji ili kuendelea kuhakikisha kwamba wanatatua baadhi ya changamoto za wanyama wakali kwenye baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili kwa kuwa Bunge hili tayari limekwishatupitishia bajeti, tutakwenda kuanza kulitekeleza baada ya kuahirishwa kwa Bunge letu hili Tukufu, lakini nikuthibitishie tu kwamba yale yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wametuletea hapa tutakwenda kuyafanyia kazi. Naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba maeneo mengi ambayo wameshauri, pamoja na kwamba wameunga mkono kwa asilimia 100 hoja zote zilizotolewa yale mengine machache ambayo tunaamini kabisa tuna haja ya kwenda kuyafanyia kazi ili kulinda maslahi ya wananchi wetu tutakwenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kimsingi hoja ambazo zimekwishazungumzwa tayari nimekwishazitolea ufafanuzi wa kina kabisa ili tuweze kuhakikisha kwamba Azimio hili linakuwa na msingi lakini Maazimio haya yanakuwa ni ya kulinda maslahi ya wananchi wetu tunaowawakilisha kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ya mwisho ambayo imezungumzwa hapa ni kuhusu mazoezi haya ambayo tumeyafanya hasa kwenye Hifadhi yetu ya Kigosi lakini Hifadhi yetu ya Ruaha yaweze kupita kwenye maeneo mengine. Zoezi hili halitaishia katika maeneo haya ya Ruaha na Kigosi, tutaendelea nayo. Hakuna sifa yoyote ya kuendelea kupata hasara kwenye maeneo wakati tunaweza kufanya jambo ambalo likasaidia Taifa letu. Kwa hiyo, tutaendelea kuyapitia kwenye baadhi ya maeneo kuhakikisha kwamba maeneo yetu yote yanakuwa na tija.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengi ambayo yameshauriwa na Waheshimiwa Wabunge yamekuwa na tija na sisi tunasema tu kwamba kama Serikali tutakwenda kuyafanyia kazi. Nikiri tu kwamba kwa wale Waheshimiwa Wabunge ambao wamezungumza kuhusu eneo letu lile la Kigosi hasa kuhusu eneo la uzalishaji wa asali, nikuthibitishie kwamba sisi tumejipanga vyema kuhakikisha kwamba eneo hili tunaliandaa kwa ajili ya wafugaji wa asali na shughuli nyingine mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe tu kwamba leo hii Serikali inaingiza karibu takribani dola milioni 14 peke yake katika sekta hii na hicho ni kiwango cha asilimia tano tu cha asali ambayo inauzwa nje ya nchi, lakini kwa zoezi hili ambalo tumelifanya hapa hasa la eneo la Kigosi itatusaidia kama Serikali kuhakikisha kwamba tunaongeza uzalishaji wa asali kutoka tani 38,000 mpaka tani 132,000. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kiwango hiki kitaisaidia Serikali kukusanya zaidi ya dola milioni 50. Kiwango hiki kitasaidia Serikali kukusanya takribani dola milioni 50 kwa asali ambayo itauzwa nje ya nchi. Nilitaarifu tu Bunge lako Tukufu kwa eneo ambalo tutalirejesha ukanda huu ndiyo ukanda ambao kwa Afrika unaongoza kuwa na asali nzuri. Tuseme kwa Afrika ni namba mbili, ukanda huu ambao tunarejesha eneo la Kigosi, kwa hiyo, tutaongeza jitihada.
Mheshimiwa Spika, na hivi karibuni tutazindua mpango tunaouita, “Ondoa shoka kamata mzinga.” Mpango huu utakwenda kuzihusisha Wilaya zote, mpango huu utakwenda kuhusisha Mikoa yote inayoguswa na Azimio hili hasa Azimio la Kigosi ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanashiriki moja kwa moja kwenye shughuli hii ili tuweze kuongeza mapato. Hatuna sababu hata kidogo ya kuwaambia Watanzania ni kwa nini leo hii mchango wetu kwenye Sekta ya Wizara ya Utalii ni asilimia 25 hasa kwenye fedha za kigeni, hatuna sababu ya kushindwa. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuongeza jitihada na mpango wa Ondoa shoka kamata mzinga utakwenda kuongeza fedha za Serikali, fedha za kigeni lakini pia utatoa mchango kwenye Pato la Taifa ili tuweze kutoka kwenye asilimia 22 na sisi dhamira yetu tutoke asilimia 22 tuende mpaka asilimia 30 kama mchango kwenye Pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, licha ya uamuzi wa Serikali wa kumega eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 478 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwenda kwa wananchi, Serikali itaendelea kufanyiakazi ushauri uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wa kufanya tathmini ya eneo lingine linalopakana na Shamba la Kapunga kwa upande wa Kusini Mashariki ili kujiridhisha kama eneo hilo bado lina hadhi.
Mheshimiwa Spika, nami nimesema inawezekana kwamba ni vema tukaangalia maslahi ya wananchi katika eneo hili, na nilithibitishie tu Bunge lako Tukufu kwamba tayari wataalam wamekwishaanza, wako uwandani na tayari wamekwishaanza kufanya tathmini ya kiwango gani tutarejesha kwa wananchi na baada ya hapo tutarejea kwa wenzetu chini ya Mwenyekiti wetu ili kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu na kushauri mamlaka waridhie kiwango ambacho tutaona kwamba ni muhimu kukitoa kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ninaomba sasa kutoa hoja. Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Waziri ngoja, ili tuongozane vizuri umehitimisha hoja zote mbili kwa wakati mmoja. Sasa ili Bunge liweze kufanya maamuzi kwa maana ya wewe kutoa hoja, toa hoja moja moja. Kuhitimisha umehitimisha pamoja nilikuacha tu uendelee ili umalize hoja zako zote. Toa hoja moja moja unatoa moja unaenda zako kukaa Bunge linaulizwa lifanye maamuzi halafu utaleta hoja nyingine. Kwa hiyo, unaweza kuanza na mojawapo kati ya hizi mbili, yoyote tu ambayo iko karibu hapo.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja ili Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liridhie katika Mkutano huu wa Kumi na Moja na kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha Nne cha Sheria ya Hifadhi ya Taifa, Sura ya 282 inayoazimia kuridhia kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,760 kama ilivyoainishwa kwenye kiambatanisho ili iwe Hifadhi ya Misitu ya Kigosi.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia manufaa ambayo Serikali imekwishazungumza kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na wananchi wa maeneo husika watayapata kutokana na marekebisho yaliyopendekezwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kumi na Moja na kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Hifadhi ya Taifa Sura 282, inaazimia kuridhia marekebisho ya mipaka ya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa kumega kilomita za mraba 478 kutoka kwenye hifadhi hiyo na baadaye marekebisho hayo kufanyika. Hifadhi ya Taifa ya Ruaha itakuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 19,822 kama ilivyoainishwa kwenye kiambatanisho.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naafiki.