Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/2024 kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema, namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha anawezesha vyema utekelezwaji wa bajeti ya Serikali. Nakupongeza Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Katibu wa Bunge na watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa. Nampongeza sana Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri Mheshimiwa Hamad Chande na Mawaziri wote na watendaji wote wa Wizara za Serikali kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kufanikisha malengo ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshmiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inayokwenda kuwagusa wananchi moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuendelea kuimarisha utendaji kazi katika utumishi wa umma ambapo imeanzisha mifumo miwili, ambapo mfumo wa kwanza ni wa usimamizi wa utendaji kazi wa utumishi wa umma (PEPMIS), na mfumo wa pili ni wa usimamizi wa utendaji kazi kwa taasisi za umma (PIPMIS), pia imeanzisha mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara (HCMIS). Mfumo huu umeunganishwa na mifumo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba taasisi mbalimbali zinaweza kubadilishana taarifa kwa mfano imeunganishwa na PSSF, HESLB, Sekretarieti ya Ajira, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mfumo wa Malipo ya Serikali (MUCE), mfumo wa mahudhurio, mifumo ya kibenki mbalimbali ili kufuatilia mikopo ya watumishi, PEPMIS na HCMIS lengo ni kurahisisha huduma za watumishi na pia mifumo yote inafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuja na mkakati wa kulinda majanga ya kimtandao mwaka 2022, pia imekuja na mwongozo wa matumizi bora, sahihi na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), naipongeza sana Serikali kwa juhudi kubwa sana inazozifanya na pia kati ya taasisi 522 za umma, taasisi 433 zimeweza kuunganishwa na mfumo wa kiutumishi na mishahara.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa taasisi 134 tu za umma ndiyo zimeweza kuhifadhi mifumo ya taarifa kwenye vituo vikuu vya kuhifadhi taarifa na mifumo ya Serikali (Government Data Centers) vyenye usalama na uhakika kwa upatikanaji wa taarifa za Serikali, hivyo tunaishauri Serikali katika bajeti ijayo ya mwaka 2023/2024 iwezeshe Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora kutenga fedha za kutosha kuwezesha taasisi zingine kuhifadhi taarifa zao kwa ajili ya usalama wa taarifa za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha uliopita yaani 2022/2023 naipongeza Serikali imeweza kulipa malimbikizo ya mishahara ya watumishi 116,792 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 199, imetoa vibali vya ajira mpya 7,499 na ajira mbadala 6656. Pia zaidi ya taasisi 62 zimeweza kuandaa na kuhuisha miundo na mgawanyo wa majukumu na imeidhinishwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia miundo 63 ya maendeleo ya utumishi na mishahara ya taasisi za umma imehuishwa na kuidhinishwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali imebuni Daftari la Huduma za Serikali Tanzania (GST) ambao mpaka sasa hatua za usanifu wa mfumo zimefanyika na taarifa kutoka kwenye taasisi 51 zimekusanywa. Naishauri Serikali katika bajeti ijayo iwezeshe Wizara hii kukamilisha huduma hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali katika nia yake ya kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, imeanzisha vituo viwili vya huduma katika majengo ya Ofisi za Posta katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam, mwananchi akifika katika vituo hivyo anaweza kupata huduma katika taasisi za NIDA, RITA, Uhamiaji, NHIF, BRELA, Polisi, NSSF na PSSF. Jambo hili limekuwa na matokeo chanya sana kwa wananchi, naishauri Serikali katika bajeti ijayo yam waka 2023/2024 iongezewe pesa ili vituo zaidi viweze kuongezwa katika mikoa mbalimbali ili kusogeza huduma kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, katika huduma za jamii, nimekuwa nikichangia mara nyingi eneo la afya, lakini nakumbusha tena bajeti inapotengwa katika Wizara yoyote hususani ya afya tunaomba pesa ifikishwe kwa wakati kwani maradhi huwa hayasubiri, mfano bajeti inapitishwa mwezi Julai, 2023 lakini inafika kwenye hospitali husika mwezi Septemba, hii haileti tija kwa kuwa ugonjwa hausubiri. Hivyo ninashauri bajeti inapotengwa, iwe inafika kwa wakati ili iweze kuleta tija.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kujali suala zima la elimu ya Mtanzania kwa ujumla, kuongeza mikopo na kuendelea kugharamikia mpango wa elimu bila malipo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuchangia hayo naunga mkono hoja mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/2024.