Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja Kuhusu Bei ya Kuuza na Kununulia Mahindi

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja Kuhusu Bei ya Kuuza na Kununulia Mahindi

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, kulingana na hoja ambayo mtoa hoja aliitoa jana ni kwamba Serikali haijatoa katazo lakini imetoa maelekezo ambayo yanawafanya wakulima au wafanyabiashara wapate changamoto ya kutoa mazao nje ya nchi. Changamoto hiyo ikasababisha bei za mahindi kushuka. Ukatuagiza kwamba twende kwenye vituo vyetu tukaulize kama NFRA wameshaanza kununua mahindi.

Mheshimiwa Spika, hali iliyopo sasa hivi ni kwamba NFRA mpaka sasa hivi bado hawajaanza kununua mahindi kwenye vituo. Hoja yetu iko hapa; wazo la Serikali ni jema lakini masharti waliyoyaweka yanafanya wafanyabiashara wasiweze ku-export mazao hayo kwa wakati, hata NFRA kwenye hivyo vituo vilivyopo si rafiki kumfanya mkulima aweze kuuza mazao. Hivyo basi mazingira yanakuwa magumu kwa wakulima wetu, kwa hiyo sisi tulikuwa tunaomba tutoe hoja ili Wabunge tunaotoka kwenye maeneo hayo tujadili ili tuweze kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

SPIKA: Ngoja kwanza. Mheshimiwa Condester Sichalwe, hoja ya kutolewa mahindi nje ya nchi ama kuuza nje ya nchi imekuja kama sehemu ya kupungua kwa bei ya mahindi, maana yake kama yananunuliwa humu ndani kwa bei inayofaa hiyo hoja haipo.

Waheshimiwa Wabunge, kwa maelezo ya jana, na ndiyo maana nasema mwenye hoja; wewe kwa maelezo uliyotoa sasa hivi hapa nataka niulize jambo moja halafu ndio nijue cha kufanya. Kama mahindi yatanunuliwa kwa bei iliyopo na NFRA ile bei si ni sawa? Maana ndiyo majibu yalikyokuwepo hapa jana. Hoja ilikuwa ni kwamba NFRA ilikuwa haijaanza kununua mahindi kwa bei hiyo kwa sababu bei aliyotoa mtoa hoja ilikuwa shilingi mia nane sijui mia ngapi ndiyo ikaonekana bei inakuwa chini kuliko ile aliyotaja Waziri?

MHE.CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, naomba kukujibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama bei hiyo ambayo Serikali wametoa bado mahindi yataendelea kushuka kwa sababu mbili zifuatazo: -

i. NFRA ukipeleka mahindi, wanavyo vigezo vyao vingi unaweza kupeleka tani mia tano wakachukua tani kumi. Hivyo kufanya wakulima hawa wasipate mahali pa kuuza mahindi lakini wachuuzi wa kawaida wenyewe wanachukua mahindi maadam ni mahindi na wananchi wanapata nafasi ya kununua.

SPIKA: Haya, nani anataka kutoa taarifa? Mheshimiwa Yahaya ngoja. Mheshimiwa Condester Sichalwe toa hoja.

MHE.CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nomba kutoa hoja Wabunge wote waunge mkono. (Makofi)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, naafiki.