Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa uliyonipatia ya kuweza kuchangia na kwa sababu ya muda nitajitahidi niende kwa haraka haraka. Moja, ni kutoa pongezi kwa kazi kubwa ambayo inafanyika na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kule Mufindi tuna msemo wetu kwamba, mfupa ulioshindikana, Samia anautafuna, kwa sababu mambo mengi yaliyoshindikana yameanza kufanyiwa kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nashukuru hotuba nzuri sana ya Waziri wa Fedha. Kimsingi ni hotuba nzuri inayotoa uelekeo wa Taifa letu na tuna imani kubwa sana na Wizara kwa namna mnavyomsaidia Rais wetu. Namshukuru sana Katibu Mkuu wa CCM kwa ziara zake kwa sababu kwenye Jimbo letu la Mufindi Kusini ametugusa moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niungane pia na wengine wanaomwombea Spika wetu heri katika ushindi wa nafasi anayoiomba huko mbeleni kwa sababu amedhihirisha weledi mkubwa katika kuongoza Bunge letu. Tunaamini akiwa Rais wa IPU atafanya vizuri zaidi pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanya kwenye Mkoa wetu wa Iringa. Tunaona mipango mikubwa ya ujenzi wa uwanja wa ndege, tunaona barabara kubwa za Ruaha National Park na ndugu yangu hapa, jirani yangu wa pale Kilolo, naye barabara yake ya Ipogoro inakwenda vizuri, kwa kweli tunashukuru Mungu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee Mufundi Kusini, Mpango wa EPC + F ambao umeweza kufanyika umesaidia pakubwa sana, unaanza kujenga barabara yetu ya Mafinga kwenda Mgololo na maeneo mengine kama barabara ya Sawala, miradi ya maji ya Mbalamaziwa, Malangali, mradi wa Igowole pamoja na maeneo mengine mpaka kule Mgololo. Pia tunashukuru kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA pamoja na kiwanda kikubwa cha kuchakata parachichi katika eneo letu la Nyororo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maombi machache, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha anisikilize kwenye eneo hili na atusaidie. Rais Mheshimiwa Dkt. Samia amefanya ziara mwaka 2022 mwezi wa Nane, akaahidi barabara ya Mafinga – Mgololo na Nyororo – Mtwango. Tunashukuru kwanza Mafinga – Mgololo imeshaingizwa tayari na mkataba umeshasainiwa; Nyororo – Mtwango pia imeshatajwa kwenye bajeti, lakini imewekewa Shilingi milioni 500 tu, imeleta sintofahamu kubwa kwa wananchi wote. Hata ile furaha waliyokuwanayo kwa Rais wetu imeanza kuwa simanzi. Tunaomba unapoenda kuhitimisha Mheshimiwa Waziri wetu utuambie kuhusu barabara ya Nyororo – Mtwango kilometa 40, tusaidie angalau hata kilometa zianze hata kama zikiwa 20 au 30 ili hatimaye iweze kukamilika barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ombi letu lingine kubwa ni kwamba tunataka wenzetu wa Wizara ya Mifugo watusaidie vifaranga angalau milioni tano kwenye mabwawa yetu, wakati huo wenzetu wa Wizara ya Maji tunaomba mtusaidie kumalizia ujenzi wa Bwawa la Iramba pamoja na Ihuwanza. Ninaamini Mheshimiwa Aweso yuko pale atakamilisha hoja hii na ataweza kutusaidia iwe kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa TAMISEMI, Jimbo la Mufindi Kusini ndiyo jimbo pekee ambalo halijajengewa kituo cha afya hata kimoja tangu miaka miwili tulipoanza. Tunaomba kituo cha afya cha Mgololo na cha Mtwango mtusaidie. Kama haitoshi, tunaamini na tunaomba kabisa kituo cha afya kwa wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani watusaidie pale Nyororo ili tuweze kuimarisha ulinzi na usalama kwenye eneo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu. Moja, kwenye upande wa mapato, tunalo eneo muhimu sana, hapa tunazungumzia kuhusu mapato. Nataka Serikali itujengee mambo yote haya. Yako maeneo ya kupata fedha mojawapo ni eneo la biashara ya carbon. Wenzetu wa Gabon tumeambiwa watapata shilingi milioni 150, wenzetu wa Ghana wana pato la shilingi milioni 4.9, Ndugu yangu Kakoso kule kwake ana vijiji nane tu, kapata shilingi bilioni nne. Sisi tuna vijiji 12,000 hivi hatuoni kama kuna mabilioni ya pesa hapa? Hebu tutazame Wizara ya Fedha tukatafute pesa hapa, tukafanye kazi ya wananchi na kusaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, naomba mtusaidie kwenye kuboresha biashara nchini. Tunahitaji kuongeza walipakodi kama ambavyo kwenye hotuba wamesema, tax base iongezeke, lakini mkakati wa kuwajali na kuwaheshimu walipakodi kwa kweli hauridhishi. Tunawaomba Wizara ya Fedha mtusaidie, acheni utaratibu wa kukimbilia kufungia watu maduka. Wale ni Watanzania wenzetu, kaeni nao chini, zungumzeni nao, wapeni ushauri, wafundisheni. Hamkupelekwa shule ili kwenda kuzalilisha na kunyanyasa wafanyabiashara wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hoja hiyo pia nigusie kidogo kwenye ajenda ya upande wa Wizara ya Kilimo. Wenzetu wa Wizara ya Kilimo wana ajenda ya twenty thirty ni hoja ambayo ukiisikiliza inabeba maono makubwa. Wana mpango ikifika 2030 tuweze kupata tupunguze umasikini kwa takribani 64%. Tutakuwa tumefanya kazi kubwa lakini tunahitaji 17.3 trillion. Naiomba Serikali ianze kutenga fedha kila mwaka ili hatimaye tuweze kuja kufikia hatua ya kuweza kuboresha na kufanya mapinduzi makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu na tunatambua kwamba tayari tumeshaongeza Bajeti ya Kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mwaka juzi, mwaka jana ikafika shilingi bilioni 754, mwaka huu shilingi bilioni 970 lakini twende zaidi tufanye kilimo, mifugo na uvuvi kama ajenda namba moja kama tulivyofanya miundombinu kwa miaka mitano mpaka saba iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo nipende kushukuru sana kwa kunipa fursa hii ahsante sana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)