Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Mwita hayupo nadhani nitakula na zake nipate 10, hiyo ni zali la mentali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nianze kwa kukupongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa sana kwa kweli uliyoifanya kwenye kipindi cha Bajeti iliyoisha. Mheshimiwa Waziri ni Mbunge nina miaka saba humu ndani. Unaona mishale siyo mingi, kiukweli umefanya kazi kubwa sana katika kila Jimbo tuna kila sababu ya kukupongeza yaliyoko ni madogo madogo ambayo tunahitaji kukushauri uyafanyie kazi ili baadaye mwakani mambo yaendelee kuwa mazuri zaidi tunapoenda kujiandaa na Bajeti nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushauri sana Mheshimiwa Waziri, Mchango wangu wa leo mwingi nitakushauri. La kwanza; unakumbuka tulikuwa wote pale kwenye vurugu za Kariakoo, watu waligoma tukashinda siku nzima pale na sisi tulishawaambia mapema humu, mkatanguliza mizaha sasa naomba nikushauri. Mbunge mwenzangu Kanyasu hapa alilalamika kuhusiana na utendaji kazi wa mtumishi wa TRA pale Geita anaitwa Bwana Njau kwamba ameshika mtu akiwa kwenye drip ya diagnosis ya kusafisha figo chini ya kiti yaani yuko kwenye stuli na akajibu majibu. Kesho yake mkafuta kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nikwambie sijui mnataka labda na Geita nako kuandamane kwa sababu mtendaji huyu ana miaka karibia nane pale na kila siku watu wanalalamika. Anaenda anafunga biashara ya watu yaani wewe akikuona una duka la piki piki linafanya vizuri anakuletea kodi, anakuchimba mkwara, anafunga account baada ya wiki mbili yeye anafungua duka la kwake. Ukienda ukiangalia watu wote wenye biashara ya bar pale Geita wanaombwa risiti toa hivi, kesho unafungiwa account yeye bar yake inafanya twenty-four, seven na haina hayo mambo ya risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuombe Waziri nimekutajia anaitwa Njau tunalalamika hapa kwa mara ya mwisho. Vinginevyo kitaumana kule. Kama ni mzuri mchukue mpeleke wilaya nyingine, kwetu Geita ametosha tuletewe watu wengine. Hatuhitaji kuendelea kulalamika. Tutachukua maamuzi maana na sisi wananchi wametuamini kule wametuamini tuwasemee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; nataka kujiuliza na bahati nzuri Ndugu yangu Mwigulu yeye ni mchumi. Tunahitaji kuwa na viwanja vya ndege vilivyo na biashara kubwa. Kiwanja cha Ndege cha Mwanza hivi mmetuonaje yaani kila mwaka sisi mnatusomea tu takwimu, mnatupiga tu kanzu, tunasikia tu mabilioni, kiwanja kiko vilevile. Jengo limejengewa speed limewekewa vioo mpaka vimeanza kuanguka. Tumelogwa na nani Mheshimiwa labda utuambie tuna tatizo gani tulichowakosea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya ndege kwa Tanzania hapa ukiondoa Dar es Salaam kiwanja cha pili kilicho busy ni Mwanza, tatizo ni nini? Haiwezekani, tulikuwa na Mkuu wa Mkoa Gabriel aliyefukuzwa anasema kiwanja kiwe cha halmashauri. Amekuja mwingine aliyepelekwa Morogoro na yeye yule yule. Nimuombe Ndugu yangu Makala na nikuombe na wewe Waziri. Tunahitaji kuwa na kiwanja cha kimataifa cha Mwanza. Kwanza mmenunua ndege kubwa hii ya mizigo. Mnaitoa wapi mizigo kama Kanda ya Ziwa uwanja hauendeki? Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri tunahitaji kuwa na kiukweli Mheshimiwa Waziri usipokuja na jibu zuri kuhusiana na Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, hii imeshakuwa ni too much, ni dharau. Tutasimama Wabunge wote wa Kanda ya Ziwa hatutakubaliana na kukupitishia bajeti yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa jengo lipo, ugomvi uliopo ni kati ya halmashauri. Halmashauri ilitoa shilingi bilioni mbili sijui Serikali rudisheni, unatoaje hela kulia unaweka kushoto? Chukua maamuzi tutengenezee uwanja. Tumechoka kupigwa swaga, mwaka wa saba kila mwaka tunaletewa Bajeti ya Uwanja halafu hivyo hivyo, eeh? Haiwezekani leo ndege zote za Tanzania hapa biashara kubwa iko Mwanza. Tunaingiza fedha mnatuona sisi mbahau tunaona tu watu wanaenda hatuwezi kukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usipokuja na majibu mazuri Mheshimiwa, kutoka Mwanza kwenda Serengeti ni kilometa 90 tunataka kuona wazungu. Tunataka kuona wazungu wanatua Mwanza, hivi hamjiulizi hata matajiri wakubwa wanaotoka Ulaya na jet wala hawaendi Kilimanjaro kwa sababu ni mbali. Kilometa zaidi ya 500. Ukitoka Mwanza wanatua Mwanza wanaacha jet wanaenda na ndege ndogo pale dakika 15 wanaona wanyama tatizo liko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga mahoteli, tumejenga kila kitu na Serikali imewekeza hoteli kubwa sana pale Kapripoint, mmeliacha tu limekuwa jumba la kulala popo kwa sababu hamna mikakati mizuri. Nikuombe Mheshimiwa Waziri ili tusiumane huko mbele nikuombe sana Mheshimiwa Waziri unapokuja hapa ututambie Uwanja wa Ndege jengo lile hebu hata wewe Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ukipita pale Mheshimiwa Waziri unaona mashine kubwa kabisa zimeletwa pale wanalala bundi tu mle halafu tunakaa hapa kupiga makofi, hatutapiga makofi mwishoni hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho; suala la mafuta, kwanza Ndugu yangu Mwigulu una wakati mgumu sana na nikuombe uchukue maamuzi. Nilijua utakuja hapa na taarifa ya kutuambia umepandisha bei, umepandisha ushuru wa mafuta yanayotoka nje ili shemeji zangu wa Singida wale wanaoshinda barabarani maelfu na maelfu wamening’iniza madumu mafuta yao yaende bei kubwa. Hivi kweli watu walivyolima vile kweli ndugu zangu, shemeji zangu wa Singida wale tushushe tena mafuta leo yanarudi shilingi 40,000, shilingi 8,000 kwa lita tano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri kuku kaangukia kwa sheikh kwa hiyo, inabidi uangalie unachinja kuanzia mguuni au unachinjia shingoni. Watu wanakuangalia tunahitaji kuona zao hili na wakulima hawa hawakatishwi tamaa na kushuka kwa bei. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho dakika moja...

MWENYEKITI: Ahsante sana, la mwisho lile kwa hiyo tayari umemaliza, ahsante sana.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sekunde moja. Mheshimiwa Mwigulu, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana sisi tunatoka kijijini. Nyumba zetu kule kijijini ziko hoi usije tena na swaga hapa brother ya kutuletea kutuambia unaongeza buku kwenye cement acha. Njoo na mawazo ya kushusha, tumechoka kulala kwenye matembe na sisi tunataka kuwa na mabati kama mlivyo watu wa Dar es Salaam na mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)