Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii nipate kuchangia Bajeti yetu ya Serikali ya mwaka 2023/2024. Kwa sababu ya muda nitakimbia kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshika kitabu cha Bajeti aliyoisoma Mheshimiwa Waziri wa Fedha tarehe 15 wiki iliyopita na ninataka nianze kwa kunukuu ukurasa wa 182 unasema. “Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii tena kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwa uongozi wake bora na thabiti wenye mafanikio makubwa hususan katika kuleta mageuzi ya kiuchumi pamoja na kuimarisha hali ya kisiasa nchini na mahusiano ya kikanda na kimataifa katika kipindi kifupi cha miaka miwili ya uongozi wake. Hakika Mama apewe Maua yake.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika Bunge hili nimeifuatilia kwa ukaribu sana bajeti hii na nimeisoma vyema sana Finance Bill ambayo tunaendelea Kamati ya Bajeti kuwasikiliza wadau. Ninaungana na Waziri wa Fedha kusema Mama apewe maua yake kwa kupitia Bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza; mwaka jana tulikuwa na Bajeti ya shilingi trilioni 41.48. Bajeti hii tunayokwenda kuipitisha ni ya shilingi trilioni 44.39, hili ni ongezeko la shilingi trilioni tatu nzima na ni ongezeko la almost 7%. Ndugu zangu katika macho ya kibajeti na kitaalamu hili siyo jambo jepesi, ninasema Mama apewe maua yake. Miaka miwili iliyopita tulishauri hapa kwamba nchi yetu ifanyiwe credit rating. Serikali sikivu ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ikafanya jambo hilo. Hivi sasa ninavyozungumza nchi yetu iko rated na makampuni mawili makubwa duniani ya credit rating, Kampuni ya FITCH na Kampuni ya MOODY’S. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mara baada tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha kusoma Hotuba yako ya Bajeti siku zile, wenzetu ambao tumewapa kazi ya kutusimamia kwenye mambo haya ya fedha na kutushauri, Kampuni ya MOODY’S wametoa taarifa yao sijui kama umeiona. Taarifa hii na yenyewe imedhihirisha kwamba Mama apewe maua yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenzetu wame-appreciate kwamba kwenye Bajeti yetu, mapato yameongezeka. Lakini la pili, hatua zote za kikodi ambazo zimechukuliwa zinatufanya Tanzania tuendelee kuwa nchi inayokopesheka. Kwa hiyo, tutaendelea kuaminika kwenye masoko ya kifedha makubwa huko duniani lakini kwa nini Mama apewe maua yake? Wenzetu wa MOODY’S hawa wanastaajabu. Wanashangaa kuna mambo makubwa matatu yanafanyika ndani ya nchi yetu pamoja na ongezeko hili la bajeti na pamoja na kipindi kigumu hiki cha uchumi kwa dunia nzima. Jambo la kwanza wanasema, wanalishangaa, linawezekanaje kwa Tanzania kufanyika? La kwanza; higher spending for ongoing infrastructure projects. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya MOODY’S wanashangaa inawezekanaje Tanzania inaongeza bajeti na inaenda kuongeza makusanyo ili hali inapeleka fedha nyingi sana kwenye miradi mikubwa ambayo kwa ukanda wetu wa Afrika na hasa hasa Kusini mwa Jangwa la Afrika haipo miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kwanza ni reli ya SGR na ambayo inajumuisha ununuzi wa vichwa na mabehewa. Kwenye hili ushauri wangu kidogo tu tutafute vichwa na mabehewa angalau kwa root moja tu kwa Serikali halafu tuwaachie private sector. Tuwe na line moja tu inayoweza kutusaidia kufanya kui-regulate biashara lakini tuwaachie private sector ifanye eneo hilo la vichwa na mabehewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo wanatushangaa ni ujenzi wa Bwawa kubwa la Mwalimu Nyerere. Kote huko kunakwenda na trillions. Wanashangaa ujenzi wa Daraja la Busisi kule Kigongo. Wanashangaa skimu kubwa za umwagiliaji ndiyo maana wamekuja na taarifa wanasema Mama apewe maua yake wanaungana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na mimi naungana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wanashangaa sana fedha zinatoka wapi za kujenga miundombinu kwenye Mji wetu wa Kiserikali pale Mtumba. Unajua, you cannot know what you have until you lose it. Mheshimiwa Waziri wa Fedha wewe ni mwalimu wangu lakini leo naomba nisione haya nikupongeze mbele ya Watanzania. Nakupongeza na ninataka nikwambie una bahati kufanya kazi kuwa Waziri wa Fedha chini ya Rais wa aina hii ambaye tunaye. Naomba nirudie hii statement, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu una bahati sana kuwa Waziri wa Fedha katika kipindi ambacho tuna Rais wa aina hii Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wanaendelea kushangaa wanasema inawezekanaje Watanzania wanayafanya haya wanapeleka miradi ya barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesaini hapa miradi ya barabara mingi sana lakini na mwisho kwenye miradi hii mikubwa mikubwa wanasema wanashangaa kuona miradi ya huduma za kijamii. Hakuna mahali Tanzania hii ambapo hapajengwi kituo cha afya, hakuna mahali Tanzania hii hapajengwi hospitali, hakuna mahali Tanzania hii hapajengwi shule, hakuna mahali Tanzania hii hapapelekwi umeme. Hakika Mama apewe Maua yake na kwenye hili. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)