Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Juliana Didas Masaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi niungane na wenzangu Wabunge wenzangu kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini kipekee pia kumpongeza Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba. Kusema ukweli wote mnastahili maua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kwa haraka haraka kwa ajili ya muda. Kwanza napenda kuchangia kwenye mambo matatu. Jambo la kwanza ni cargo consolidation na deconsolidation kusajiliwa kwa store na mfumo wa EFD Machine. Nikianza kwenye consolidation na deconsolidation. Kuna tatizo hasa kwenye hawa wasafirishaji wa mizigo ambao wafanyabiashara wakienda kwa mfano China, Uturuki, Marekani nchi yoyote wanaenda kununua mizigo kwa ajili ya kuleta nchini kwa ajili ya mauzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa wafanyabiashara wengi wanatumia wasafirishaji wa mizigo ambao kitaalam kwa lugha yao TRA wanaitwa consolidation na hao consolidation kazi yao kubwa inakuwa kukusanya mizigo ya wafanyabiashara wengi na kuweka kwenye cover moja au container moja. Sasa nachangia kuhusu hili kwa sababu gani? Kwa ajili ya mgogoro mkubwa uliotokea kama mwezi uliopita pale Kariakoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa consolidators ambao wanafanya biashara ya kukusanya mizigo ya wafanyabiashara wadogo wadogo na kuingiza nchini mfumo huu Serikali ilikuwa na nia njema kabisa kwa ajili ya kuandaa mfumo huu wa hawa wasafirishaji kukusanya mizigo ya wafanyabiashara. Walikuwa na nia njema kabisa na walikuwa sahihi lakini Mheshimiwa Waziri wa Fedha mfumo huu ndiyo unawasababishia kukosa kodi halisi, kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanyabiashara anapoenda Guangzhou au nchi yoyote ile anaenda kununua mzigo anapewa risiti kwenye manunuzi yake. Anaenda kwenye maghala kule Guangzhou au Beijing au popote, consolidator anachukua ule mzigo kwa nia ya kumsafirishia mpaka nchini kwake na consolidator anapofika hapa nchini anaingiza ule mzigo kwanza kwenye forodha anaingiza ule mzigo anasema yeye ni consolidator, anaingiza kwa pamoja lakini kwenye ulipaji wa kodi Mheshimiwa Waziri wa Fedha hawa consolidators wanatumia mbinu za kukwepa kulipa kodi halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale kwa kamishna wa TRA wa kodi za ndani wakiwa wanakaguliwa wanaingiza hii mizigo kwa majina yao au kwa kampuni zao na remind you Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakishaingiza hii mizigo kwa majina yao kwa kampuni zao wanalipia ile mizigo wao wenyewe pale TRA. Wakishailipia ile mizigo wanaenda sasa nje kwenye maghala yao mizigo ikishatoka wanawapa wafanyabiashara wale mizigo yao bila kuwapa risiti zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo linakuja sasa afisa TRA anapoenda Kariakoo kukagua mahesabu ya wafanyabiashara au mizigo tatizo linakuja wale wafanyabiashara wanakuwa hawana risiti halisia kabisa na ndiyo maana wanapokuwa wanakisiwa kodi wanasema wanaonewa kwa sababu kiukweli wanakuwa hawana kumbukumbu ya risiti na risiti zinabaki kwa msafirishaji. Nia ilikuwa njema lakini naona inafanyika vibaya sana sasa hivi.

TAARIFA

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tarimba taarifa.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana kwa mchango mzuri Mheshimiwa Mbunge. Nataka nimwambie sababu hiyo ndiyo inayofanya ulipaji wa VAT uwe mgumu kwa sababu kodi ya VAT ni input tax na output tax. Sasa bila kuwa na VAT uliyolipa wakati ukiingiza mzigo huwezi ukatoa risiti kwa minajili ya kulipia VAT wakati ukiuza na ndiyo maana kuna bei ya bila risiti na bei ya risiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Juliana Masaburi, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa hiyo ahsante sana Mheshimiwa Mbunge wa Kinondoni Mheshimiwa Abbas Tarimba. Sasa kama Mheshimiwa Abbas Tarimba alivyosema kwa hiyo hapa kuna tatizo Mheshimiwa Waziri na ninakuomba sana ili pia uwaziri wako siku ukiondoka uache legacy hili suala linatakiwa kushughulikiwa haraka na ipasavyo na hili suala la hawa consolidators unawaona hata wafanyabiashara wenyewe hawalalamiki kwa sababu kwanza wanapata faida. Wanapata faida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kariakoo nilienda kuhudhuria sijamsikia mtu kulalamikia kuhusu hawa wasafirishaji consolidators kwa sababu they know wanapata profit, I mean triple. Umeona Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu ni nini? Ushauri wangu sawa kuwe na hawa consolidators wasafirishaji hawawezi kuepukika kwa ajili ya urahisi wa kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara lakini Wizara yako na TRA waone njia sahihi ya ku-accommodate hawa wasafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependekeza mfanye kama ile bonded warehouse ya magari. Mizigo ikishafika ikae waipeleke kwenye bonded warehouse kila mfanyabiashara akafutae mzigo wake apewe risiti zake, akalipe kodi mwenyewe. Hii itasababisha kwanza Serikali nyinyi kupata kodi zenu halisi lakini pia wafanyabiashara kutoogopa kwamba kuwe na point kwamba kuna mlolongo wa watu au foleni au nini lazima kila mfanyabiashara alipe kodi kwa sababu ya mahesabu ya kampuni yake au biashara yake kuwa safi na sahihi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.