Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia bajeti yetu ya Serikali iliyowekwa mezani na kaka yangu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba pamoja na Naibu wake ndugu yangu Chande.

Kwanza nitumie nafasi hii sana kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nilikuwa nanukuu hapa sentensi iliyoandikwa na Kamati ya Bajeti, ikanipendeza sana; niinukuu; “Napenda nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuonesha kwa vitendo nia yake thabiti ya kuondolea Watanzania umaskini na kuwaletea maendeleo. Aidha utu wake katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii umekuwa ni msingi imara katika kutekeleza kauli yake mbiu ya kazi iendelee.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maneno ambayo kila Mtanzania hawezi kuyabishia. Ni maneno sahihi ambayo anastahili kupewa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ziada nimpongeze pia Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa jinsi wanavyoendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza yale ambayo ameahidi kuwafanyia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka kwa sababu ya muda nitajielekeza kwenye maeneo machache tu. Jambo la kwanza lilisemwa wakati tunachangia bajeti za kisekta, Wizara ya Afya; suala la urasimishaji. Nipongeze sana Serikali katika hatua sasa hivi iliyofikia ninao mkopo wad ola milioni 150, takribani bilioni 345 ambao utaenda kusaidia maeneo mengi kwenye eneo la Wizara hii ya Ardhi. Niombe sasa, utekelezaji huu Mheshimiwa Waziri wa Fedha ujielekeze kule, kama wenyewe walivyosema, fedha zitoke ziende zikamalizie mgogoro wa urasimishaji ndani ya mitaa iliyopo ndani ya Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wizara ya kisekta inasema itatatua mitaa 559 mimi nina mitaa 42 hivi; kwa hiyo ipo tayari kwenda kumaliza. Mwakani naamini wakati tunapitisha bajeti yetu ya Serikali sitoongea tena mambo ya ardhi. Nina imani sana mambo mazuri yatafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine niipongeze tena Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni eneo la barabara. Tumepiga kelele humu kwenye bajeti za kisekta; lakini hata hii bajeti kuu imeeleza vizuri juu ya barabara kubwa za kimkoa, kiwilaya na miradi mingine itakayoendelea. Kule ndani ya Jimbo la Kibamba barabara za chini ya TARURA na DMDP tayari, tunaishukuru sana Serikali. Tumeshasaini na wakandarasi na washauri (consultants); vilevile na stakeholders, tumefanyia Dodoma na Dar es Salaam. Leo wananchi wanajua kwamba miradi inaenda kutekelezwa kuanzia mwezi wa nne mwakani. Barabara ya Kingongo inaenda kutengenezwa kwa lami, tunaendelea. Barabara ya Msumi kilometa nane inafungua kutoka Madale hadi Stendi ya Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kwa Shija kilometa 4.2, pia na Barabara ya Konoike kule ambako kuna tenki kubwa la mshikamano ambalo tumejengewa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo mambo ni mazuri. King’azi – Malamba Mawili kilometa mbili za lami zinaanza mwezi wa nne kwa hiyo hili ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la Barabara, niliuliza swali la nyongeza asubuhi. Kuna ahadi nyingi. Bajeti yako inasema moja ya vigezo ukiondoa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na mambo mengine lakini ahadi za viongozi wa kitaifa ni eneo ambalo linazingatiwa. Hili nimesema asubuhi chini ya asilimia 50 embu tukaliangalie ili tuendelee kuwaheshimisha viongozi wetu hawa. Wanakwenda kutembelea maeneo wakitoa ahadi zitelekezeke. Ni vizuri sana kuangalia zote za miaka ya nyuma muweze kuzitengea fedha na kuzitekeleza zile ahadi za viongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo la maji. Mheshimiwa Waziri taarifa yako imesema na yenyewe vizuri, niendelee kuwapongeza. Dar es Salaam Jimbo la Kibamba mambo ni mazuri na tunaendelea kuunganishiwa maji. Lakini shaka yangu, wakati wa kiangazi tunakosa maji ya Ruvu ambayo ni tegemeo katika miaka tangu tunapata uhuru. Leo population ni kubwa, zaidi ya watu milioni 5.4. Haiwezekani wakategemea chanzo kimoja, tunajua tumewekeza kwenye Bwawa la Kidunda basi niombe sana utekelezaji wake uende haraka ili sasa wananchi hawa katika mikwazo ya vipindi vigumu tuendelee kuwapatia maji safi na salama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi naunga mkono hoja.