Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipatia hii nafasi. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri Mheshimiwa Chande, lakini vilevile nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya na kuhakikisha ile miradi ambayo endelevu ya kutoka Awamu ya Tano kwenda katika Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya. Tunamwona muda wote yuko mbioni akihakikisha kuwa maeneo mbalimbali ambayo yana utata, yeye anakwenda kuyarekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitaishukuru sana Serikali kwa ajili ya Mkoa wangu wa Lindi. Mkoa wa Lindi ni mkoa Tajiri, lakini ulikuwa nyuma hasa katika maendeleo kwa vile ulikuwa hauna miradi. Sasa nitaitaja miradi ambayo ni mikubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameipitisha katika mwaka huu. Mradi wa kwanza umesainiwa Mradi wa LNG, huu mradi ni mkubwa ambao unakwenda katika eneo la Likong’o katika Jimbo au Manispaa ya Lindi. Utaleta mafanikio makubwa katika nchi yetu, lakini ningeomba sana katika huu mradi Wabunge tuje tupewe taarifa nini kinaendelea katika LNG? Mafanikio ya LNG, lakini vilevile tunataka wananchi wetu kule wajue wanatuuliza maswali mengi ili kujua nini kinaendelea katika LNG? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Waziri mwenye dhamana aje afanye semina na Wabunge, aende Lindi na Mkoa wa Lindi na Mtwara tuunganike tujue lini LNG inafanyika? Maendeleo yale yawazindue wananchi ili wajitambue katika suala la local content na miradi ya corporate social responsibility ili na wananchi wajiandae kibiashara kwenda na maeneo hayo. Tunahitaji mahitaji ya smart city kwa ajili ya wale wanaokuja kuwekeza wasije kwenda mikoa ya jirani kwa vile Lindi hatuna mahoteli ya kutosha. Tunaomba uwekezaji mkubwa wa mahoteli na maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi mkubwa vilevile ambao umezinduliwa mwaka huu Ikulu, Mradi wa Madini ya Graphite Ruangwa – Chilola. Huu ni mradi mkubwa na Lindi ambayo ilikuwa ya maskini, itakuwa ni Lindi ya matajiri. Ni mkoa ambao una ufanisi mkubwa katika madini. Ni matumaini yangu Wanalindi tumefika muda sasa hivi kuwa tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha hatutakuwa tena ni mikoa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa tatu, miaka nenda tulikuwa tunalia barabara Nangurukuru, Liwale, Masasi, mwaka huu wameshasaini tayari barabara ya lami na nina imani itatoa kero na uzia mkubwa na ambao tulikuwa nao kwa ajili ya barabara hizi ambazo zilikuwa hazipitiki. Ilikuwa Mbunge wa Liwale kipindi cha masika hawezi kwenda Liwale, lakini huu ukombozi wa kutupatia huo mradi mkubwa wa kupitisha barabara nasema Mwenyezi Mungu azidi kumbariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati juzi tulitembelea Arusha, tumepata taarifa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Royal Tour imeleta mafanikio makubwa sana. Watalii wamejaa Arusha ila tuna changamoto hatuna hoteli. Tunaomba wawekezaji wakubwa, tunahitaji uwekezaji, hakuna kupinga uwekezaji. Uwekezaji uliokuwa umetukuka na mikataba mizuri ijenge mahoteli, hii Royal Tour ambayo tumeleta watalii wengi wapate mahali pa kukaa na kuweza kujisikia raha katika utalii wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaombe TANAPA wajenge mahoteli, tuwaombe Ngorongoro wajenge mahoteli, wachukue mikopo wajenge hoteli kwa sababu sasa hivi watalii wanahangaika, wanakwenda kulala katika mahoteli ya chini kabisa na kwa kweli Arusha imefurika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji wa Bandari; sisi tunahitaji uwekezaji. Mikoa ambayo inazungukwa na bandari tunahitaji ufanisi mkubwa sana katika uwekezaji. Hizi changamoto wanazolalamikia wananchi kama sheria mbalimbali zifanyiwe marekebisho na ni matumaini yangu ushirikishwaji wa bandari na uwekezaji umeshirikisha Bunge, umeshirikisha Mashirika ya Dini, Waziri Mkuu vilevile amekwenda kutoa ufafanuzi, sijawahi kuona eneo ambalo limeingia mradi limeshirikisha wananchi kama mradi huu. Nini faida yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kwanza SGR itafanya kazi, tutakuwa na mzigo wa kutosha ambapo reli hii tunayotengeneza itapata mzigo hapa kupitia huu Mradi wa Bandari. La pili, TAZARA ambayo imekuwa haina mzigo, mizigo itakayokuwa inakwenda Zambia itakuwa inapita katika reli ya TAZARA. Ni kitu ambacho ni kizuri, lakini kwa nini watu wanapiga kelele? Kuna maeneo matatu yana changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao ni competitor, hawakubaliani na huu mradi hata siku moja. Competitors kwa vile mizigo mingi ilikuwa inakwenda nchi za Jirani, hawatakubali Tanzania iweze kupata mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mawakala, kuna mawakala wamo mle ndani ambao walikuwa wanafanya biashara ya kupitisha mizigo bila kufuata sheria. Anasema mzigo huu ni wa transit, anapiga mihuri humu njiani mote, lakini mzigo uko Dar es Salaam. Wale wanaona kabisa katika kuleta ufanisi huu, katika uwekezaji na wao watapata changamoto na ulaji wao utakuwa haufanikiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira katika bandari zetu za Mtwara na Tanga. Mkoa wa Mtwara ile bandari ilishasimama kwa muda mrefu. Ni imani yangu uwekezaji huu, utafufua uchumi katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Mzigo ambao unatoka Zambia, unaotoka Malawi, badala ya kuja Dar es Salaam utakatisha Makambako kuja Lindi, kuja Mtwara. Kwa kweli sisi hatuna cha kusema zaidi ya kusema, yale ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho yafanyiwe marekebisho na ni imani yangu kuwa Mheshimiwa Rais anawapenda wanawake, anawapenda Watanzania, hathubutu kufanya kitu ambacho hakitaweza kumfanya yeye apate nanii, mama ni mlezi, wakati wote mwanamke ni mlezi, hawezi mwanamke mwenye ulezi wake akataka kuiangamiza. Huu mradi naomba Mwenyezi Mungu ausimamie na katika kuusimamia kwake, Watanzania tutakuja kufarijika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasema naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nimuunge mkono Mheshimiwa Waziri, yeye ni Balozi wa watu wenye ulemavu, ametoa bilioni 1.0 kwa ajili ya kusaidia watu wenye ulemavu na kutuwekea Mfuko watu wenye ulemavu. Walemavu wanasema yeye ni Balozi wao na hawatamwangusha, tuna kila namna ya kusema ahsante kwa niaba ya walemavu wote Tanzania, nasema Mwenyezi Mungu azidi kumbariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.