Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya upendeleo. Mimi ningeomba kuchangia mambo machache ili kuwa miongoni mwa wachangiaji kwenye hotuba hii ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi yake kubwa ya kuendelea kulitumikia Taifa, na kwa kazi yake kubwa ya kuendelea kutafuta vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania. Ni kazi kubwa, ngumu, inahitaji ujasiri, uimara na umakini wa ku-focus wapi Tanzania iende. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza wasaidizi wake wawili ambao kwa kweli ili nchi yetu iendelee inahitaji vijana makini ambao kwa kweli watatusaidia na watalisaidia Taifa kwa kufanya kazi chini ya mama ili kuhakikisha kwamba nchi inaendelea. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wako wote. Hakika mnafanya kazi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niwatie moyo, kwa sababu, kama Taifa linahitaji kusonga mbele; na ili Taifa lisonge mbele lazima tuwe na vyanzo vya mapato kutoka maeneo mbalimbali ambavyo vitalisaidia Taifa, ili kuweza kutimiza mahitaji ya Watanzania. Moja kati ya hayo, mlituletea hapa Muswada na tukaupitisha kwa ajili ya kuiunga mkono Serikali ili iendelee kutafuta wawekezaji. Naomba sana kwenye hili msirudi nyuma kwa sababu tunafanya uwekezaji mkubwa ikiwemo kujenga SGR, na kufufua reli zetu zote pamoja na reli ya TAZARA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, SGR kama hesabu zangu zinaniambia sawasawa, wametuambia inahitaji mzigo wa tani milioni 25 kwa mwaka, leo tuna uwezo wa chini ya tani milioni 20. Kwa hiyo, tuna SGR, tuna Reli ya Kati, tuna TAZARA, tuna reli nyingine na Barabara. Zote hizi zinahitaji mizigo. Sasa kama tunahitaji kuendelea, lazima tuwaunge mkono wenzetu ili waweze kutafuta mizigo zaidi ili Serikali iweze kuwahudumia wananchi. Naomba hapa msivunjike moyo, kwa sababu ili tuweze kuwahudumia wananchi ni lazima tutekeleze au tutimize ahadi zetu kama Serikali ambayo inasimamiwa na Chama cha Mapinduzi, msirudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema kelele za mlango huwa hazimzuii mwenye nyumba kulala. Tuendelee kuchapa kazi kwa sababu ndio wajibu wetu. Tumeaminiwa na wananchi, tuhakikishe kwamba lazima tunawahudumia. Ndiyo Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, tuendelee ku-stick on the game. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba univumilie, mimi nina kawaida ya kusoma hiki kitabu, maana ndiyo nilichokikuta. Naomba ninukuu Katiba yako hii ya mwaka 1977 ya Jamhuri ya Muungano, kwenye Sura ya Kwanza ile inasema: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano,” lakini kifungu cha pili inasema: “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo la Tanzania Bara na eneo la Tanzania Zanzibar na ni pamoja na sehemu yake ya Bahari ambayo Tanzania inapakananayo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa naomba kutoa angalizo, hasa kwa wenzetu wote, wale ambao wanadhani kwamba chama chetu na Serikali yetu haishughuliki na matatizo ya Watanzania. Ni kweli Katiba hii imetoa nafasi ya kutoa maoni, nafasi ya vyama vingi, lakini haikutoa nafasi ya kuvunjiana heshima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kuwakumbusha wenzetu, sisi wa umri wetu, kwa mujibu wa data zilizopo, zaidi ya asilimia 70 ni vijana ambao wako chini ya miaka 50. Maana yake tunachokijua ni Katiba hii ni ya Tanzania, ndicho tunachokifahamu. Kwa hiyo, wenzetu msitengeneze maneno ya kuligawa Taifa hili. Taifa hili limepiganiwa na Taifa hili linaitwa Taifa la Tanzania. Hakuna Mtanzania nusu, wala hakuna Mtanzania kipande, msituvuruge. Nawaombeni sana, wala msimvunje moyo mama kwa sababu analihudumia Taifa. Analihudumia kama Mtanzania mwenye haki kamili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna mmoja anadhani yeye ni Mtanzania zaidi kuliko mwingine, ajitathmini. Kwa sababu haiwezekani, Katiba hii imetupa haki sawa sote kama Watanzania. Kwa hiyo, asijitokeze mmoja kwa sababu ya ulevi, kwa sababu ya kulewa madaraka, akadhani yeye ana haki zaidi kuliko mtu mwingine yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo haki zote kama Watanzania. Kwa hiyo, nawaomba sana, tuheshimu matakwa ya Katiba hii, na pia tuheshimu haki ya kila Mtanzania. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba, jitihada zinazofanyika zinafanyika ili kutuondoa Tanzania tulipo ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana mama yetu ambaye ni Rais wetu, mama usivunjike moyo. Tulikuahidi hapa, tunakuunga mkono, tutaendelea kukuunga mkono kwa sababu dhamira yako tunaielewa sisi watoto wako kwamba ni kuiongoza Tanzania ili iweze kupiga hatua. Shika kamba, endelea, tunakuunga mkono. Sisi vijana wako, Wabunge wenzako, tuko pamoja na wewe kuendelea kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuliko yote naomba sana hili tulizingatie kwa sababu sisi kama Watanzania hatuna Taifa lingine. Sisi kama Watanzania tunao wajibu wa kulilinda Taifa hili ili vizazi vyetu vije kurithi Tanzania iliyo bora kuliko iliyo leo. Kwa hiyo, tusiwavunje moyo. Wale wanasiasa wenzetu ambao wanajifunza kufanya siasa, kwa sababu, wako vijana wanajifunza kufanya siasa, siasa siyo kuwadanganya watu, siasa ni kutekeleza matumaini ya watu kwa kutumia vyanzo vilivyopo ili kuboresha maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tujiheshimu, tuheshimu Katiba, tuheshimu viongozi wetu, na pia tuwape nguvu ili waweze kufanya kazi ya kulihudumia Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naiunga mkono sana bajeti hii. Asanteni sana. (Makofi)