Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania. Wenzangu wamesema apewe maua yake, nami nasema Mheshimiwa Rais apewe maua yake, anafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na timu nzima ya wizara, mnafanya kazi nzuri, taarifa nzuri sana, kila unapoisoma unaona raha, kwa kweli package ni nzuri kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninayo machache ya kuchangia katika bajeti hii. Mheshimiwa Waziri katika hotuba yako umesema kabisa kwamba wastani wa watu waliochangia kodi ni asilimia 20 tu ndio waliochanga vizuri. Umesema kwamba walipa kodi waliosajiliwa ni 4,455, wenye TIN halali ni 4,400,000; wenye TIN halali ni milioni moja, hawa milioni moja wamechangia trilioni 16.7 kwa maana ya asilimia 80 ya mapato yetu, ambayo mwenyewe umesema kabisa mapato hayo yamepatikana na idadi ya wachangiaji wadogo sana, asilimia 20. Palepale ukasema kwamba katika maneno muhimu ya kuzingatia ni ukweli kabisa kwamba wastani wa walipa kodi siyo mzuri sana kwa sababu wanaolipa kodi ni wachache kwa hiyo wachache ndio wanachangia kodi ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini; nataka kusema kwamba bado kuna kazi kubwa tunatakiwa kufanya ili tuweze kuongeza mapato, ili tuweze kuongeza hawa wachangiaji wa hii kodi yetu. Na hii inaweza kusaidiwa kwa kuendelea kuongeza vyanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichangia hapa mwaka jana, na leo nasema; bado tu sisi tunaotoka majimbo ya mpakani; Kakonko, Kibondo, bado tuna fursa ambayo haijatumika vizuri, fursa ya mipaka yetu. Bado masoko ya ujirani mwema yanafanyika kiholela, masoko ya ujirani mwema ni shamba la bibi kwa sababu uratibu haupo. Kila mtu pale ni afisa mkusanyaji mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba hapa kujengewa forodha ya pamoja ili tuwe na TRA pale, tuwe na polisi na migration ili biashara iweze kufanyika vizuri kwenye Soko langu la Mkarazi na Soko langu la Kibuye. Haya yote yameshindikana. Haya ni mapato ambayo yanapotea. Tungeweza kudhibiti haya mapato tusingeendea kukandamiza wananchi kwa kung’ang’ania vyanzo vichache, lakini walipa kodi wachache ndio wanatuchangia Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nakuomba uje kwenye masoko yetu ya ujirani mwema. Kule Muhange, Mkarazi na Kibuye, tunaomba uje, kuna pesa kule, turatibu zile biashara za kwenye mipaka ili tuongeze walipa kodi na ili tuweze kuratibu hizi biashara za mipakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, tukiongeza walipa kodi hatutakuwa tunaongeza kodi kwenye vile vyanzo tunaona kwetu ni rahisi. Nimeona hapa tumeongeza tena kwenye mafuta na cement, ina maana tunatafuta urahisi wa kupata hii pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo ninavyoongea Jimbo la Muhambwe cement inauzwa 23,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50. Sasa ninajiuliza hii kodi ikiongezeka kwenye cement wananchi wa Muhambwe tutajenga kweli? Mtu wa Dar es Salaam ananunua 14,000, tunaambiwa usafiri ndiyo unasababisha cement iwe 23,000 Kibondo. Sasa mafuta nayo yameongezeka, wananchi wa Muhambwe hii cement hawataweza kuinunua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, ninawaomba, hebu tutoke nje ya boksi na wataalamu watusaidie, akili ichangamke kidogo, basi turatibu hii bei, bei iliyoko Dar es Salaam na bei iliyoko Kibondo iwe ileile ndiyo tuongeze hizi kodi. Lakini kama tunasema usafirishaji unasababisha cement iwe ghali basi tunaomba hii kodi ya cement itolewe. Maana yake mpaka sasa ni 23,000, kwa hiyo, itakuwa changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, mafuta yatakwenda kuleta matatizo mengi; nauli itapanda, mazao yatapanda, kila kitu kitapanda. Kwa hiyo, ninaomba wataalamu wetu nao akili zao zijiongeze tunasema watoto wa mjini watafute vyanzo vingine ili tusiendelee kumkamua ng’ombe wa maziwa mmoja huyohuyo, atakufa maana yake atakamuliwa mno Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, vilevile niombe; ni hakika tunahitaji hizi pesa, hata natamani tuzipate kwa ajili ya kuratibu na kuharakisha miradi, maana yake tunayo miradi kwenye majimbo yetu ambayo kwa kweli kasi yake haifurahishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi karibuni tu miliona vibonzo vinapita vikionesha vumbi la Kibondo. Hata sisi watu wa Kibondo hatujisiki vizuri, tunatamani lile vumbi liishe. Tunaomba miradi yetu ya kimkakati ya barabara yetu ya kuunganisha Kasulu, Kibondo, barabara ya kuunganisha Kigoma, Tabora, zipelekewe pesa, wakandarasi walipwe pesa zao ili hizi barabara ziweze kuisha na sisi tusiwe vibonzo kwenye mitandao kwa ajili vumbi linaloendelea katika majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, miradi hii ya kimkakati inayojengwa katika Mkoa wa Kigoma inayo miradi ya complementary ambayo inategemea kujengwa Kasulu, Buhigwe na Kibondo. Barabara zipo asilimia 60, 70, 80, lakini miradi hii haijaanza kabisa. Tunaiomba Serikali miradi hii ianze, kwa sababu kama hizi barabara zitaisha halafu miradi haijafanyiwa chochote matokeo yake hii miradi itakwenda kupotea. Na sisi tulishawaambia wananchi wetu kwamba hii miradi ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niombe Mheshimiwa Waziri, bajeti ya mwaka 2021/2022 majimbo yote ya Mkoa wa Kigoma yalipewa milioni 150 kwa ajili ya kumalizia maboma ya zahanati, kasoro Jimbo la Muhambwe. Nimeshakwenda TAMISEMI zaidi ya mara nne, nimeshakwenda Wizara ya Fedha zaidi ya mara nne, naambiwa vifungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi pesa mlitupa ninyi na majimbo yote yamepewa. Afisa mipango vifungu anavitoa wapi? Nilishakwenda Kumkuyu nikafanya mkutano; Rukaya nikafanya mkutano, tena kwa kujinasibu jamani naleta milioni 50 ya zahanati, leo hii naambiwa vifungu ambavyo hizo pesa mmeleta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri unavyokuja kuhitimisha hapa naomba milioni 150 yangu kama ambavyo majimbo mengine yamepewa ili na mimi niende kutimiza zile ahadi ambazo niliwaahidi wananchi wa Jimbo la Muhambwe. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja asilimia 100. (Makofi)