Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Bajeti Kuu ya Serikali, na nianze kwa kutambua na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kuinua uchumi wa Tanzania pamoja na uchumi wa mtu mmoja mmoja. Aidha, kipekee ningependa kumpongeza sana na kumtia moyo mchumi mbobezi kabisa, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba na Wizara yake nzima kwa kazi kubwa wanayofanya, na kazi yao tunaiona na kupitia bajeti hii tuna ona dhamira ya dhati kabisa ya kufanya uchumi wa Tanzania upae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia haraka haraka kwenye maeneo matatu. Eneo la kwanza, naishukuru sana Serikali kwa kuyafanyia kazi maoni ambayo sisi Wabunge tunatoa, maana nafahamu Serikali ilitambulisha kodi ya huduma za kidigitali na kampuni za nje kama Facebook yaani meta wameshaanza kuwasilisha taarifa zao Serikalini, nawapongeza sana. Aidha, nawapongeza pia kwa uamuzi wa kuamua kutoza kodi kwa biashara za mitandao (online businesses) kwa maana halisi ya online businesses ambazo hazina maduka sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitoe tu angalizo kuhusu kutoa kodi kwa hawa watu wanaoitwa influencers. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, tuwe na definition sahihi ya influencer ni akina nani. Kwa sababu mathalani mimi naweza nikawa ni shabiki wako, nika-post kazi inayokuhusu wewe lakini utakuwa hujanilipa, mimi nimefanya tu kwa utashi wangu na kwa namna ambavyo ninakukubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hapa pia nimeona viongozi wengi pamoja na Wizara nyingi zimelipia kwenye Kampuni ya Twitter ili wapate verification. ambapo wanalipa gharama kwa dola nane mpaka kumi kwa mwezi. Sasa ningependa kufahamu pia Wizara ina mpango gani wa kupata kodi kupitia fedha inayolipwa Twitter kupitia viongozi wetu wa Serikali pamoja na Wizara husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili; Serikali ilishaweka dhamira ya dhati ya kuona namna gani ambavyo tunainua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja hususan makundi maalum kupitia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hii imefanyika kupitia sheria ya manunuzi, ya asilimia 30. Ningependa kupata kauli ya Mheshimiwa Waziri nini ambacho anapanga kufanya ili kuhakikisha kwamba wanawake, vijana na makundi maalum wananufaika na asilimia 30 ya manunuzi ya umma kama ambavyo Sheria ya Manunuzi ya Umma imeelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho, dhamira ya dhati ya Serikali ni kuinua uchumi wa nchi yetu, na ili tufanye hivi ni lazima Serikali iweke jitihada za makusudi kabisa kuangalia mikoa ambayo inatambulika kama ina hali kubwa ya umaskini ilhali ni mikoa ambayo haipaswi kuwa katika nafasi hiyo. Hapa nitaongelea Mkoa wangu wa Kagera. Mkoa wa Kagera umepakana na nchi tatu, umepakana na Rwanda, Burundi na Uganda na unabeba asilimia kubwa ya Ziwa Victoria. Una hali nzuri ya hewa, una ardhi yenye rutuba, unapata mvua misimu miwili na zaidi kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapaswa ije na mkakati thabiti wa kuona namna gani ambavyo itainua uchumi wa Mkoa wa Kagera, kwa sababu kwa hali ilivyo sasa haikubaliki na hairidhishi. Kwa hiyo kwa haraka haraka ningependa kushauri maeneo yafuatayo kuhusiana na kuinua uchumi wa Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ulikuwepo mradi wa Mto Ngono, na naishukuru Serikali wameshaanza kufanya upembuzi yakinifu. Lakini mimi naona na ninaomba sana Serikali mradi huu uwekwe katika orodha ya miradi ya kielelezo (flagship project) na uweze kutafutiwa wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, kwa kutambua kwamba Mkoa wa Kagera unapakana na nchi tatu na fursa zilizopo katika ukanda huo wa nchi za maziwa makuu, niombe sana Serikali irudishe mpango wa kujenga airport ya kimataifa, maana mpango ulikuwepo. Wakati sasa umefika tuurejeshe mpango ule ili Mkoa wa Kagera upate airport ya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo tunayo Airport ya Bukoba, wengi tunafahamu mchango wa Airport yetu ya Bukoba, niombe sana Serikali katika mwaka huu wa fedha ambao tunakwenda, 2023/2024, Airport yetu ya Bukoba iweze kufanyiwa uwekezaji kupata fog light pamoja na control tower ili safari za kwenda Mkoani Kagera ziwe ni safari zisizo kuwa na misukosuko na ikiwemo pia kufungua uchumi wa Mkoa wetu wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, natambua kwamba Wilaya ya Bukoba Mjini ndiyo reception ya Mkoa wetu wa Kagera unaounganisha Mkoa wetu na nchi zinazo tuzunguka. Naomba kipekee kabisa Stendi ya Bukoba Mjini ipewe kipaumbele katika Mkoa wetu wa Kagera ikiwemo pia na Soko Kuu. Haikubaliki kwamba Mkoa wetu kwa namna ulivyo na kwa ukubwa wake, na ukizingatia hata kitakwimu za sensa tunazaidi ya watu milioni tatu lakini mpaka leo Stendi yetu haieleweki ni lini itajengwa na fedha kupangwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoelekea kumalizia, Mkoa wa Kagera una zaidi ya ranch tano lakini bado ranch hizi hazijaonesha katika umahsusi wake unachangia vipi katika biashara ya nyama ikiwemo pia biashara ya maziwa. nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwa kushirikiana na Mawaziri wenzako mfanye tathmini, na hili jambo hata Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishalisema. Tufanye tathmini ya zile ranch nini kifanyike ili ranch hizi ziwe na tija ziweze kuchangia ukuaji wa uchumi si tu wa Mkoa wa Kagera lakini na uchumi wa Tanzania. Ili ranch zile wapewe wawekezaji ambao wataleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii nami naunga mkono hoja, na ninaendelea kumpongeza sana Mwanauchumi Mbobezi Daraja Moja Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Wizara yako nzima. Halikadharika namshukuru sana na ninampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya, ahsante. (Makofi)