Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. SEIF K. F. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii nyeti, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu, napenda kujielekeza katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa 128 alipokuwa akizungumzia masuala ya elimu katika masuala mazima ya usafirishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona namna gani ambavyo tuna vyuo mbalimbali vinavyotoa kozi mbalimbali zinazohusiana na masuala ya usafiri katika nchi yetu. Nijielekeze kwenye Chuo cha Taifa cha Usafirishaji. Chuo hiki ni Chuo ambacho kiliasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wetu wa Awamu ya Kwanza, mwaka 1975. Ni Chuo cha muda mrefu ambacho kimekuwa kikitoa kozi zinazohusu usafirishaji, kozi ambazo huwezi kuzipata kwenye vyuo vingine nchini. Miaka ilivyokuwa inakwenda, uwezo wa chuo ulikuwa unapungua kwa kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia miaka ya katikati miaka ya 2000, nilipata bahati ya kujiunga katika chuo hiki. Wakati nimeenda kuchukua Bachelor ya masuala ya uchukuzi, nilisoma mwaka wa kwanza na mwaka wa pili nikapata nafasi ya kuomba kuwa kiongozi, nikawa Rais wa wanafunzi pale Chuoni. Kwa hiyo, nilipata fursa ya kuingia katika Bodi za chuo, lakini nilipata fursa ya kutambua changamoto zilizopo ndani ya Chuo kile. Moja ya changamoto, Chuo kile kina majengo ambayo wameanzisha kuyajenga kwa ajili ya maendeleo au kupanua wigo katika kudahili wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walianzisha jengo mwaka 2004 lenye ghorofa nne na likapangiwa phase namna gani Wizara itapeleka fedha kwa ajili ya kulijenga lile kulimalizia; Wizara imepeleka phase; mwisho phase tatu. Phase ya nne wamewaambia wamalizie wenyewe. Chuo hiki kitapata wapi fedha za kumalizia jengo kubwa, linalohitaji gharama kubwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia jengo limechukua muda mrefu, tunaona Wizara mbalimbali zinavyoweka nguvu katika vyuo vyao katika kuhakikisha kwamba vinapanua wigo wa kuongeza majengo na infrastructure ya chuo, lakini Chuo cha Usafirishaji jengo limejengwa miaka 11 halijakwisha mpaka leo. Naiomba Wizara ya Uchukuzi iangalie hili suala mara mbili mbili; kama siyo macho mawili, basi waongeze na la tatu. Haiwezekani tule ng‟ombe mzima tushindwe kumalizia mkia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda tu kugusia, Chuo hiki kinatoa kozi ambazo sehemu nyingine huwezi kuzipata. Kwa mfano, wameanzisha School of Aviation. Pale kuna kozi ya Aircraft Maintenance Engineering ambayo kwa Tanzania huwezi kuipata; lakini TCAA wanachukua wanafunzi wanapeleka nje ya nchi kuwasomesha watoto wetu wa Kitanzania; gharama ya kusoma hii kozi nje ya nchi ni karibu shilingi milioni 100 kwa miaka mitatu. Chuo kimeanzisha kozi hii, gharama yake ni shilingi milioni 30 kwa miaka mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wa kimaskini wa Kitanzania, wameomba mikopo katika Bodi ya Mikopo. Sera ya Bodi ya Mikopo, katika watu wanaochukua engineering, ada zao hazizidi shilingi milioni moja na nusu, lakini kwa wale ambao wanachukua Udaktari wanapata mkopo mpaka wa shilingi milioni sita. Hawa watoto wanaokwenda kusoma pale wanaambiwa ada kwa mwaka ni shilingi milioni kumi. Sasa naomba Wizara iangalie hii, shilingi milioni moja Bodi ikilipa, wanabaki watoto wale wanadaiwa shilingi milioni tisa.
Wanapata wapi watoto wa kimaskini kulipa shilingi milioni tisa kwa ajili ya kusoma kozi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ikae pamoja na TCAA badala ya kutumia fedha nyingi kwenda kusomesha nje ya nchi ni bora wawalipie watoto wetu wasomee hapa, waboreshe miundombinu ambayo pale chuoni inatakiwa iboreshwe ili kuhakikishwa kwamba hiki chuo kinaendana na hadhi na Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyuo hivi kwa Afrika wakati vinaanzishwa vilikuwa vinne tu; utakipata Tanzania, Afrika ya Kusini, Ghana na Egypt. Vyuo hivi ni adimu. Wakati nasoma, nimesoma na wanafunzi kutoka Botswana na Malawi; lakini sijaona kabisa jitihada za Wizara kuwekeza fedha kwenye chuo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara sasa ichukue jukumu la kuhakikisha kwamba, chuo hiki sasa kinapiga hatua; miundombinu ya pale iboreshwe. Vyuo vimeanzishwa kama UDOM; Chuo cha Nelson Mandela vinaanzishwa miaka mitatu minne mitano kinakamilika. Chuo cha miaka zaidi ya 40 bado tunakitelekeza na bado hiki chuo ni icon ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuchangia katika suala hilo la chuo hicho nipende sasa kujielekeza katika masuala ya ujenzi, nizungumzie Jimboni kwangu, Jimbo la Manonga.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa kipindi kabla ya kampeni Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alikuja kwetu Choma Chankola akaahidi ujenzi wa daraja la Mto Manonga, lakini nadhani Wizara inachanganya, inashindwa kutambua hili daraja liko upande gani. Rais alitoa maelekezo waje watutengenezee daraja kutokea Choma kwenda pale Shinyanga Samuye, daraja lile lillitakiwa lijengwe muda mrefu lakini ukienda kwa wataalam hawa, ukikutana na Meneja wa TANROADS Mkoa anakwambia mara huku, haendi specific sehemu ambayo daraja linatakiwa likajengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe kupitia Wizara hii kuwaambia, Mheshimiwa Dkt. Magufuli alikuja Choma 2011 akatuahidi ujenzi wa daraja la Manonga. Amekuja tena akiwa anagombea Urais akasema sasa nimekuwa Rais, daraja tutajenga na barabara ya lami tutaweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara sasa itambue ahadi hizi kwa muda mrefu. Kipindi ahadi ile inatolewa 2011 walikuwepo dada zangu Halima Mdee pamoja na Sabreena Sungura, walijificha pale Choma mwezi mzima wakiomba kura za CHADEMA, lakini siku hiyo Mheshimiwa Dkr. Magufuli alipofika akawaambia wananchi 2011 tuchagueni, tupeni kura, daraja tutatengeneza. 2011 Dkt. Kafumu akapata kura, 2015 nikawaambia sasa Jimbo limegawanywa, tumepata Jimbo letu, kwa sababu tumepata Jimbo letu maana yake tutatengenezewa daraja hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ahadi zimekuwa ni nyingi, niiombe sasa Wizara iangalie mara mbilimbili, tunahitaji daraja hili lijengwe. Likijengwa Daraja hili kutoka Choma kwenda Shinyanga hazizidi kilometa 50, lakini kutoka Choma ili uende Shinyanga sasa inakubidi urudi Ziba kilometa 30, utoke Ziba uende Nzega kilometa 30, kilometa 60, utoke Nzega kwenda Shinyanga kilometa 80, maana yake utembee umbali wa kilometa 140 badala ya kilometa 45 kwenda Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ilijenge daraja hili la Manonga, lakini pia mtuwekee ile barabara ambayo Mheshimiwa Rais ametuahidi ya kutokea Ziba kwenda Choma, Ziba kwenda Nkinga mpaka Simbo pamoja na kwenda Ndala na Puge. Barabara hii Mheshimiwa Rais alitoa ahadi hiyo, kwa maana ya kuwa kwanza inapita maeneo ambayo tuna hospitali ambazo zinatoa huduma si tu kwa watu wa Jimbo la Manonga, wanatoa huduma kwa watu wa Wilaya nzima ya Igunga, Wilaya ya Nzega, Wilaya ya Tabora Mjini, Mkoa wa Mpanda na Mikoa ya Kigoma wanakuja kutibiwa katika hospitali ya rufaa. Tuna hospitali ya rufaa, lakini hatuna miundombinu ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Wizara ihakikishe kwamba ile barabara yetu ambayo inapita kwenye hizi hospitali, tuna hospitali mbili kubwa, hospitali ya rufaa ya Wapentekoste na hospitali ya mission ya RC, tunayo pale Ndala. Tunaomba tupate hiyo barabara ambayo itasaidia kupunguza adha ya wagonjwa wanaopita katika maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni barabara ya muda mrefu ambayo iko chini ya TANROADS. Hivyo basi, nipende kuiambia Wizara ya Ujenzi, katika kuja kutujibu basi katika finalize yao sijaona kwenye kitabu chao wameacndika chochote. Hivyo basi, napenda kuhakikisha kwamba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.