Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia angalau kidogo kwenye Bajeti hii ya Serikali. Naomba nianze kwa kumpongeza sana Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ya kumwakilisha Mama yetu ambaye anaitumikia nchi hii kwa moyo wa upendo na moyo wa kutujali Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze tu moja kwa moja kumwomba Mheshimiwa Waziri kaka yangu, najua mengi yameshaongelewa lakini katika Jimbo langu la Mkalama na Jimbo lake la Iramba Magharibi na Iramba Mashariki TRA wanafanya kazi kwa kuijbanza kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pale Jimboni kwake, Jimboni kwangu wamepanga vyumba viwili, hatuna watumishi, hatuna Meneja, sasa hii inatupa shida sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, angalau atenge hata kidogo, japo milioni 150 kila wilaya ili angalau tupate Ofisi ili tuweze kulipa kodi vizuri na wananchi wetu wasipate shida wakati yeye ndiye Waziri wa Fedha, charity begins at home hiyo haikwepeki. Akija kuondoka hapo hajajenga Ofisi tutakuwa tunamnyooshea vidole, tunamwomba atenge fedha ajenge Ofisi pale Mkalama na pale Iramba Magharibi na Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri, suala la kukwepa kodi kwa kutokuchukua risiti limezidi sana. Pia, hii inasababishwa na jinsi sheria yenyewe ilivyo. Kuna Mbunge mmoja hapa alitoa wazo kuhusu kutoa commission kwa watu watakaotudai risiti, hilo ni wazo zuri. Nami nataka niongeze jambo moja, Waziri amefanya vizuri sana kwa kuongeza kiwango kwamba mpaka milioni 200 ndipo mtu ataingia VAT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hiki kiwango cha kutoka milioni nne mpaka kufikia hiyo milioni 200 hakina madaraja, yaani ikishafika tu milioni nne Kwenda 11, Afisa wa kodi ndio anakaa anaangalia asilimia 3.5 ya mauzo. Ina maana mtu mwenye milioni 200 anapaswa kulipa milioni saba. Hiki kiwango ni kikubwa mno kinasababisha watu wakwepe kodi. Naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, hiki kiwango cha kutoka milioni nne mpaka milioni 200 kiwe na madaraja ambayo yatasababisha watu watumie EFD machine bila wasiwasi kwa sababu anajua daraja langu ikifika kiasi fulani nitalipa kiasi fulani. Pia, naomba nimshauri Waziri kuhusu madaraja ambayo mimi naona nafaa kupendekeza na wataalamu wako wataona, yako kama saba hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuanzia milioni nne mpaka milioni 11 wafanyabiashara wakilipa 150,000 itatosha. Kuanzia milioni 12 mpaka milioni 20 walipe 450,000. Kuanzia milioni 21 mpaka milioni 50 walipe 650,000. Kuanzia mauzo ya milioni 51 mpaka milioni 75 walipe 850,000. Kuanzia mauzo ya milioni 76 mpaka milioni 100 walipe milioni moja. Kuanzia milioni 101 mpaka milioni 150 walipie 1,500,000. Kuanzia mauzo ya milioni 150 mpaka hiyo milioni 200 waliyoweka walipe milioni mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mfanyabiashara wa daraja la chini, akienda kulipa kila baada ya miezi mitatu analipa 500,000, watu wengi watalipa kodi na hawatakwepa hiyo EFD. Atakuwa anatumia EFD, anatoa risiti hana wasiwasi, anajua nikifika milioni 200 nitalipa milioni mbili, nikifika 150 nitalipa milioni moja. Itakuwa hakuna suala la kukwepa na watu wengi sana watalipa kodi ambayo itakuwa haina maumivu wala nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la asilimia 3.5 ya mauzo kuanzia milioni 11, Afisa anakaa pale anakukadiria haiangalii ulipata hasara, haiangalii sijui mauzo na mtaji ule ni kiasi gani, mauzo yanaweza kuwa makubwa lakini faida ni kidogo, lakini unapigwa 3.5 na unatakiwa kutoa milioni saba, watu wataendelea kukwepa kulipa kodi kila siku. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri akae na wataalam wake, waweke haya madaraja, mimi nimetoa yangu, lakini mimi sio mtaalam wa kodi, lakini ninyi mnaweza mkayaboresha zaidi. Aidha, wakaongeza au wakapunguza. Haya madaraja yakiwepo watu watakuwa hawana hofu, anajua mimi daraja langu likifika nitalipa kiwango hiki, EFD itaonesha kwamba nimefikiwa hicho kiwango na watu watalipa kodi kabisa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, suala la kujenga Ofisi kwenye majimbo yetu mawili, langu na lake, sisi ni pacha asisahau. Ahsante sana. (Makofi)