Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nyingi anazozifanya za kuwahudumia Watanzania. Vile vile, niwashukuru kaka yangu Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri kwa kazi wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kuhusu suala la kodi. Wenzangu wengi wamezungumza kuhusu ukusanyaji wa kodi, lakini yako mambo ya msingi ambayo kama Wizara wanatakiwa wayaone na wayaangalie kwa mapana na marefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza nikatoa mfano mmoja, leo kontena linatolewa bandarini na likitolewa bandarini charge zote zinafanyika mle ndani. Hata hivyo, yale makontena yakishaingia Kariakoo, wakati yanatelemshwa utakuta kuna askari zaidi ya 30 wanazunguka kwenye yale makontena. Pia wale askari kuondoka kwenye yale makontena ni lazima kuwepo na utamaduni wowote ambao wao wanaufikiria na ambao ndio unaotendeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni nini ambacho nataka kukiongelea? Kama kontena linatoka bandarini likiwa limelipiwa kodi stahiki zote na linakwenda maeneo ya Kariakoo kushushwa, hakuna tena haja ya yule mfanyabiashara kwenda kutoa rushwa wakati anateremsha lile kontena. Kwa hiyo, haya mambo ndiyo wanayoyazungumza Wabunge humu ndani, ukwepaji wa kodi ni mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia Mradi wa Maji wa Ruvuma kule kwangu. Hili nalizungumza kwa masikitiko makubwa sana. Huu mradi wa Ruvuma ambao unakwenda kuwasaidia wananchi wa Mtwara na pembezoni mpaka kufika Lindi, tayari mradi huu Benki ya ADB ilishaweka token kwenye miradi yake kwa zaidi ya dola 160, wako tayari ku–engineer huu mradi ufanye kazi, lakini iko kampuni ya China Railways International Group na wao waliweka dola milioni180. Sasa, sijui uzito uko wapi au shida iko wapi wakati Mheshimiwa Rais amefika mahali sasa ametanua wigo na amempa mamlaka Mheshimiwa Waziri wetu kwamba amsaidie Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaingia 2025 wananchi wa Mtwara hawana maji salama, lakini wako watu ambao inawezekana wakasaidia kutuleta maji. Mheshimiwa Waziri, akija hapa aje na majibu kigugumizi kiko wapi? Kwa kweli Mheshimiwa Mwigulu mimi ni mdogo wangu na msikivu sana, si vema nikazungumza hapa kwa ukali sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa hili anisaidie kaka yake. Namwomba sana Mheshimiwa Mwigulu, hajawahi ku–fail kwenye jambo lolote ambalo anali–engineer. Sasa kama mimi kaka yake ananifanyia hivi mpaka napiga kelele hapa, kwa kweli ni vitu ambavyo sio vizuri sana nianze kupiga kelele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kampuni ya Alliance inaleta magari aina ya TATA. Kampuni hii imekuwa ni kampuni ya kudhulumu Watanzania toka imefika katika nchi hii. Nazungumza humu ndani tukiwa ndani ya Bunge hili, kabla Wabunge hawajaja kuwa Wabunge humu, kuna wahanga zaidi ya 30. Unakwenda kukopa hela benki na wewe unakwenda kukopa gari, unaacha pale milioni 70, unapewa gari ya milioni 130. Unaposhindwa kulipa takribani zimebakia milioni tano au sita, zile gari unanyang’anywa na Mheshimiwa Waziri, Mwigulu Nchemba, anajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaleta kampuni tukiwa na lengo kubwa la kuwasaidia Watanzania, lakini kampuni hii haiwasaidii Watanzania. Leo tukipiga parapanda hapa tuwaite Watanzania waliodhulumiwa na ile Kampuni ni hatari sana. Sasa Serikali tunayo na niishauri Serikali waamke sasa. Hawa wenzetu tayari wamefika mahali wamewadhulumu Watanzania zaidi ya asilimia 80. Kwa kweli suala hili halikubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimezungumza hapa kuhusu madai ya vijana wetu na wazee wetu wa Jimbo la Mtwara Mjini ya fedha za Kampuni ya PRIDE. Deni hili ni deni la muda mrefu kaka yangu Mwigulu analifahamu sana, zaidi ya milioni 500. Leo hii wale wananchi ambao wanaidai PRIDE wengi wao ukiwaona wameshauziwa nyumba zao hawana pa kwenda, lakini Serikali kila nikiingia humu ndani Bungeni naambiwa kesho, kesho kutwa utapata majibu na majibu ni haya ya malipo kulipa fedha. Sasa mimi nataka Mheshimiwa Mwigulu atakapoingia hapa anieleze kwamba bwana wale wananchi wangu ambao wanadai fedha za PRIDE zaidi ya milioni 500 lini wanakuja kuwalipa wale Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu zilikuwa ni tano na mimi nimezitumia dakika tano na nusu, naunga mkono hoja.