Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia bajeti hii muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninaishukuru sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mambo mengi sana ambayo hatuwezi kuyataja yote lakini utekelezaji mzuri wa bajeti ya mwaka 2022/2023 ambayo imetuwezesha sasa kuingia kwenye bajeti hii ya 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi katika Jimbo langu la Mwanga ni mingi ambayo imetekelezwa lakini tunaomba kusisitiza juu ya ukamilishaji wa miradi muhimu ambayo bado inaendelea. Mradi wa kwanza ni Hospitali ya Wilaya ambapo tulitengewa bilioni 3.3 mpaka sasa hivi tumepata bilioni mbili tunaomba hiyo bilioni 1.3 ili tumalizie ile kazi iliyobakia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi mkubwa wa Maji wa Same, Mwanga - Korogwe, tunaishukuru sana Serikali imekwamua mradi huu ambao ulikuwa umekwama tumeahidiwa kukamilika ndani ya miezi 14 na nikuambie tu kwamba kuna mama mmoja aliniita kwenye eneo lile la mradi, amepigilia vijiti 14 kwenye ukuta wake kila mwezi ukipita anang’oa kimoja ananiambia Mheshimiwa Mbunge vinavyozidi kupungua hivi vijiti ndiyo mimi nategemea maji yanywewe. Kwa hiyo, kuna siku atakapong’oa cha mwisho kama maji hayajanywewa tutapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mwanga wana imani kubwa sana kwamba miradi hii itakamilika na sababu kubwa ni mbili, sababu ya kwanza ni kwamba wanamuona Mheshimiwa Rais jinsi ambavyo ameendeleza mahusiano katika diplomasia ya uchumi kiasi ambacho tunaendelea kupata fedha za maendeleo. Pili, kinachowapa imani kubwa ni bajeti hii ambayo kwanza imepanua wigo wa kodi lakini pili imeweka commitment ya kutumia utaratibu wa PPP na pia kufufua Ofisi ya Tax Ombudsman ambayo nayo itatuharakishia fedha kuingia kwenye mzuguko, kodi kulipwa kwa wakati na mambo kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo imani ya watu wa Mwanga ni kwamba kwa sababu hiyo basi, miradi yao itaendelea kutekelezwa vizuri. Wito wangu ni kwamba Serikali iendelee ku-negotiate vizuri mikataba ya PPP, tui-negotiate kibingwa ili tuweze kupata faida tunayostahili sisi kama wananchi wa Tanzania. Ile mikataba inayofanya vizuri tuendelee kuiheshimu kama mkataba wa SONGAS kwa mfano, ni moja kati ya PPP ambazo kwa ufahamu wangu zimetuletea heshima kubwa sana kama nchi tujifunze kwamba tulifanya nini hawa SONGAS wakatufanikisha kiasi hicho tuendelee kuutunza mkataba huu lakini pia tuendelee kuingia mikataba mingine mizuri kama huu wa SONGAS ambao unaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kilio kikubwa sana ambacho kinasumbua katika nchi hii kwa sasa hivi, nacho ni suala la wakandarasi wazalendo na malimbikizo ya madai yao katika miradi ambayo wanaifanya. Wako wakandarasi wengi sana ambao wanashikilia certificate sasa hivi zaidi ya miezi tisa na hawajalipwa na wameanza kukata tamaa, wameanza kufilisiwa na mabenki kwa dhamana zao kuuzwa, lakini kikubwa pia ni kwamba pamoja na kwamba wakati mwingine tunapata hasara ya kulipa interest lakini ile interest ile riba haisaidii chochote kwao, kwa sababu wamekopa benki kwa riba kubwa za asilimia 20 halafu fedha zikichelewa ile riba inazidi kukusanyika wakati wao huku riba wanayolipwa ni kidogo sana kwa mujibu wa Mkataba. Kwa hiyo, wanaendelea kwenda chini na pia iko hatari ya mabenki kufikia mahali kuona kwamba miradi hii ya Serikali ni miradi hatarishi jambo ambalo si jema na wala halifai kwa afya ya uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza mara nyingi kwamba walipwe kwa wakati ili tuweze kukwepa riba hizi ambazo Serikali upande mmoja inapata hasara lakini pia wakandarasi wetu wanazidi kupata hasara kwa sababu riba ile ni ndogo ukilinganisha na riba ambayo wanalipa kwenye mabenki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nishauri tu juu suala la Tax Ombudsman ambalo nimelizungumza, nimejaribu kuangalia kanuni zilizotengenezwa mwaka jana kwa bahati mbaya zinaleta mlolongo mrefu kidogo wa jambo kuamuliwa mbele ya ile Ofisi ya Tax Ombudsman. Ukiangalia zile notice zinavyokwenda ni karibu siku 154 kwa shauri moja kuamuliwa, hiyo inaweza iturudishe kulekule ambako kulikuwa na mlolongo wa kwenda kwa Kamishna halafu uende TRAB, uende TRAT uende Mahakama ya Rufaa unatumia karibu miaka mitano. Nchi jirani hapo mwaka 2016/2017 Ofisi ya Tax Ombudsman ilishugulikia masuala ya malalamiko 92,000 na ikafanikiwa kuamua 77,000 na hiyo ni kwa sababu regulation zao kidogo zinachukua muda mfupi kukamilisha malalamiko ambayo yamepelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo mimi kwa kweli ninaunga mkono bajeti hii kwa asilimia zote, nikitarajia kabisa kwamba kasi ya miradi iliyokuwa ikienda katika Majimbo yetu hasa Jimbo langu la Mwanga itaendelea kama vile ambavyo imekuwa ikiendelea na pengine kwa kasi zaidi kutokana na jinsi ambavyo bajeti hii imeleta matumaini makubwa. Mheshimiwa Waziri tukupongeze na tukushukuru unatuwakilisha vizuri katika sekta yako na kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kukuamini kama ambavyo sisi tumeweza pia kukuamini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)