Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia katika bajeti hii ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea na juhudu za dhati za kuhakikisha tunafikia kujenga uchumi shindani na viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu ambayo ni adhma ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha Daktari Mwigulu Nchemba ambaye kwa kweli anafanya kazi kubwa sana katika kuhakikisha nasi tunajenga uchumi wa viwanda ambao kimsingi unategemea ushirikishwaji kati ya Serikali na sekta binafsi na Serikali tumeendelea kufanyakazi kubwa ili kuweka maboresho mbalimbali ambayo tunaamini yanaendelea kusaidia kupunguza urasimu katika ufanyaji biashara lakini pia katika uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo nitumie nafasi hii kueleza kidogo kuhusiana na mpango wa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ambayo Wizara yangu inaendelea kuratibu lakini kwa kushirikiana na sekta zote muhimu katika nchi hii ili kufikia azma ya kuwa na uchumi shindani kama nilivyosema na viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2023 jumla ya marekebisho 307 ambayo yameondoa na kupunguza tozo mbalimbali yamefanyika lakini katika kipindi hicho Sheria 48 zimefanyiwa marekebisho ambapo kwa mwaka 2022/2023 pekee zaidi ya Sheria 12 zilifanyiwa marekebisho ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa na maboresho jumla ya 105 yanayohusu ada, tozo na kodi mbalimbali ambazo zilikuwa kero katika kufanyabiashara na uwekezaji nchini lakini kubwa zaidi katika hili ni mfano wa usajili kuanza kutumia fedha za Kitanzania badala ya dola ambazo zimekuwa kero katika kuhakikisha tunatoa huduma kwa Watanzania. Moja ya mfano huo ni usajiri wa chakula cha watoto wachanga na formula za ukuzaji kabla ya maboresho ilikuwa inatumia dola za Kimarekeni 900 ambayo ilikuwa ni sawa na shilingi 2,120,400 lakini sasa tunatoza kwa shilingi milioni moja pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea pia kuboresha, kuondoa na kupunguza tozo katika maeneo mbalimbali muhimu, moja ni sekta ya kilimo, afya, mifugo, utalii pamoja na taasisi za udhibiti zilizoko hapa nchini. Pia maboresho mengine ni uimarishaji wa mfumo TEHAMA ambao Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kwamba tuendelee kuboresha. Kwa mfano, sasa hivi mifumo 58 ya kutoa vibali na leseni zinatumia njia za kielektroniki katika mamlaka mbalimbali za udhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mfumo wa malipo ya Serikali wa kielektroniki ambao umeimarishwa kwa maana ya GePG ambao unatoa huduma zaidi ya 900 ambazo zimeunganishwa na kurahisisha walipaji kodi na huduma mbalimbali wanazolipa Watanzania ili kupata huduma kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na mfumo unaowezesha mifumo mbalimbali ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa, maana yake kulikuwa na hoja kwamba ndani ya Serikali hakuna mawasiliano lakini tunaendelea kuboresha, hadi sasa zaidi ya mifumo 50 katika taasisi 45 zimeweza kubadilishana taarifa ambazo zinasaidia ufanyajikazi ili kuhakikisha tunaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo tumeendelea pia na kuanzisha sasa vitengo maalum, changamoto kubwa tuliyonayo ni katika ngazi za Halmashauri. Sasa tunaenda kuanzisha kitengo ambacho kitashughulikia masuala ya uwekezaji, viwanda na biashara ili shughuli hizo ambazo wengine wanalazimika kuja Makao Makuu kwa maana Wizarani sasa waweze kuapata huduma kule katika ngazi ya Halmashauri. Hii yote ili tuweze kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa matokeo ya haya ambayo tunaendelea nayo kumekuwa na angalau sasa kupunguza malalamiko kama si kumaliza, angalau tumepunguza kwa asilimia 71. Matokeo ya kupungua kwa siku za kuhudumia kwa mfano katika taasisi zetu, mfano OSHA wamepunguza muda wa kupata vibali kutoka siku 14 mpaka siku tatu. Pia muda wa kutoa leseni na kukabidhi matakwa ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kutoka siku 28 mpaka siku tatu, muda wa kupata cheti cha usajili wa sehemu za kazi kutoka siku 14 mpaka siku moja. Muda wa usajili wa hospitali binafsi kutoka miezi 12 hadi miezi mitatu. Muda wa usafirishaji wa mizigo umepungua kwa mfano kutoka Dar es Salaam mpaka Tunduma ilikuwa wastani wa siku saba na sasa hivi imeenda kuwa siku tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi tumepunguza kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kutoka zaidi ya siku 14 hadi siku tatu mpaka saba. Pia tumepunguza mchakato wa ushughulikiaji wa maombi, mfano taasisi ya OSHA hatua ambayo imepunguza kutoka hatua 33 mpaka hatua saba, zaidi tumepunguza foleni ya kuomba huduma katika taasisi zetu ambazo zilikuwa ni foleni kubwa ukifika kwa mfano pale BRELLA na maeneo mengine utakuta msururu wa watu wanasubiri kupata huduma katika Taasisi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka niseme haya kwa sababu kwa kweli pamoja na changamoto tulizonazo kwenye uwekezaji na viwanda wamesema hapa kuna viwanda vingine ambavyo vimefungwa lakini tunahakikisha sasa sababu zile au changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge wamechangia Serikali tunazichukua kwa umakini kabisa ili tuendelee kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ili nasi sasa tuendelee kuwa nchi shindani katika Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki lakini pia katika SADC lakini katika Eneo Huru la Biashara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeendelea kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni mbalimbali ambazo kwa kweli tunadhani ni muhimu katika kutekeleza shughuli za Serikali. Kwa mfano, Serikali imepitia na kurekebisha Sheria na Kanuni 12 hususani katika sekta za uwekezaji, viwanda na biashara, kilimo, ufugaji, afya na maliasili na hii imeenda kuboresha katika kuhakikisha tunaimarisha mifumo ya taasisi, kama nilivyosema tumeanzisha dawati au kitengo maalum cha viwanda, biashara na uwekezaji katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ngazi ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja hii muhimu, nashukuru sana. (Makofi)