Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuunga hoja ya bajeti hii, bajeti ya wananchi, bajeti ambayo kwa kweli imewasilishwa kwa umakini mkubwa na kwa umaridadi mkubwa sana, hongera sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa ufafanuzi kwa mambo machache ambayo yamejitokeza kutoka kwenye michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge na hasa ile ambayo iligusa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na hasa Sekta ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kupokea na kuwashukuru Wabunge wote ambao wamesimama na kuchangia, kupongeza jitihada na juhudi kubwa ambazo zinafanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jinsi anavyofanya, kuitendea haki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hili linafanyika kutokana na ukweli kwamba Mheshimiwa Rais ametambua kwamba uchumi wa Tanzania unaendelea kukua sana na ili uendelee kukua moja ya kigezo kikubwa sana ni kufanya miundombinu na hasa barabara iwe bora ambayo inaweza ikapitika kwa uharaka na kwa urahisi na hivyo kushusha gharama ya uendeshaji hasa katika ufanyaji wa shughuli za biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaomsaidia Mheshimiwa Rais kwa nafasi hizi, napenda tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwamba miradi yote ambayo tumeiahidi, tumeitangaza na ambayo tunaendelea kuitangaza, tuna uhakika kwa asilimia 100 kwamba itatekelezwa kama ilivyopangwa, kwani hatuna mashaka na yale ambayo ni makusudi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba ushauri, maoni na mapendekezo yote ambayo mmeyatoa tumeyachukua na tunaahidi kwamba tutaenda kuyafanyia kazi ili kuendelea kuboresha katika utekelezaji wa majukumu yetu katika Wizara yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie suala moja ambalo kuna Mheshimiwa Mbunge ameliongelea na hasa barabara za Kigoma pamoja na miradi ile complementary projects. Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Katavi ndiyo mikoa ambayo kwa kweli ilikuwa haijaunganishwa na lami kati ya mikoa na mikoa. Ambacho Serikali ya Awamu ya Sita inaifanya ni kuhakikisha kwamba Kigoma hii inaunganishwa yote kwa barabara za lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge atakuwa shahidi kwamba tunapoongea, wakandarasi watano kutoka Nyakanazi hadi Kigoma kwa maana ya Kasulu - Manyovu wako site na kwa kweli kasi ni kubwa na hasa baada ya kipindi cha mvua kwisha. Upande wa kutoka Tabora sasa hivi ukishafika mpaka Malagarasi ni lami na kipande kilichobaki, mkandarasi ameshika kasi kuhakikisha kwamba pia anamaliza tatizo lilokuwepo la kilometa 51. Kwa sasa zimebaki kilometa 51.3 ukitoka hapa Dodoma kwenda Kigoma ambazo ni za vumbi, lakini mkandarasi yuko site na upande wa Mpanda pia wakandarasi wako site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ile ya complementary ambayo ni CSR, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge hasa wa Jimbo la Kasulu kwa maana ya Wilaya ya Kasulu, Buhigwe na Kibondo, miradi hii itaenda kutangazwa muda wowote. Changamoto ambayo ilikuwepo ni ile ya kubadilisha miradi ama maeneo. Miradi hii inafaddhiliwa na ADB. Kwa hiyo, ukibadilisha sehemu yoyote, unaingia kwenye mgogoro, lakini tunajua sasa kwamba zile changamoto zimeshaondolewa. Mapema sana kuanzia Julai, hii miradi inaenda kutangazwa ambapo itagharimu fedha isiyopungua Shilingi bilioni 23.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kidogo Miradi ya EPC. Kuna watu wameendelea kuielezea kwa namna tofauti. Katika kipindi ambacho hatujawahi kukishuhudia ni kipindi hiki cha Serikali Awamu ya Sita kusaini mikataba ya barabara yenye Shilingi trilioni 3.7 na ushee kilometa 2,035 kwa wakati mmoja. Labda tu kwa ufupi katika mpango huu wa EPC tunasema ni dhana inayohusisha utekelezaji wa mikataba ya ujenzi, yaani EPC baina ya mkandarasi na taasisi ya umma, na kunakuwa na mikataba miwili; upande wa Wizara ya Ujenzi ni EPC na wenzetu wa fedha wanafanya F. Miradi hii ina faida kubwa sana. Moja ni kwamba zile risks zote haziko upande wa Serikali, lakini hakutakuwa na variation na hakutakuwa na extension. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yale makubaliano mliofanya ndiyo yatakayokuwa. Pia mkandarasi huyu ana uwezo wa kugawa maeneo maeneo. Kwa hiyo, katika barabara aliyopewa anaweza kuwa na vipande hata vitano ili aweze kumaliza haraka hizo Barabara. Vile vile kwa sababu ana uhakika wa kulipwa, kinachofanyika kwa Serikali sasa kwa upande wa Wizara, kuna watu wamehoji ubora, sisi tutahakikisha kwamba yaani anasimamiwa, anajenga kwa specification zilizowekwa, anajenga kwa ubora tuliouweka, na kwa sababu design ni ya kwake, akiharibu, kwa sababu wakati wa kukabidhi ile barabara, kila baada ya hatua ni lazima atahakikiwa. Tunafanya verification, pale ambapo ameharibu, gharama ni za kwake. Kwa hiyo, hatakuwa tayari kufanya hivyo kwa sababu anajua gharama itamsumbua. Hatakuwa tayari kupoteza muda, kwa sababu anajua hata akipoteza muda, hatalipwa chochote. Kwa hiyo, tuna hakika mpango huu utakwenda kuhakikisha kwamba barabara nyingi zinajengwa kwa uharaka sana, na kwa ubora mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tu ndio tulikuwa hatuaanza, lakini wale wanaosoma, ni miradi ambayo wenzetu ndio wanavyotekeleza miradi yao. Baada ya hapo ni kwamba hizi barabara zitakuwa ni barabara za kawaida, hakuna uhusiano wa EPC + F na PPP, tusichanganye. Baada ya hapo, hizo ni barabara za kawaida kama barabara zilizopo. Hizi ni highway, kwa hiyo, hakuna kulipia wala kufanya nini. Cha msingi tu ni kwamba hizi barabara zitajengwa kwa haraka na zikiwa zinasimamiwa na Serikali katika kila hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona nitolee ufafanuzi kwa sababu kuna watu walikuwa wanapotosha, labda kutakuwa na kulipia, Serikali hakutakuwa na mkono; Hapana. Suala la fedha, nina hakika Mheshimiwa Waziri wa Fedha atalielezea vizuri sana namna fedha itakavyokuwa inapatikana na inavyolipwa. Watalipwa tu pale ambapo Wizara ya Ujenzi inasema alichofanya ndicho hicho ambacho sisi tulimwagiza, kinyume chake ataambiwa abomoe kwa gharama zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, niseme hakika tuendelee kumpatia mama maua yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)