Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Bajeti ya Serikali Kuu. Niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi Rehema aliyetupatia uhai hata kuchangia kwenye bajeti hizi zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake nzuri iliyotukuka ya kuwatumikia Watanzania. Nina sababu nyingi sana za kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi hii ambayo anaifanya, maana amefanya, amefanya na ameendelea kufanya na kuzidi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingi za Waheshimiwa Wabunge ambazo zimekuja katika Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Uchukuzi. Nitaanza kutoa ufafanuzi baadhi ya hoja nikianza na Taasisi yetu ya Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA). Kulikuwa na hoja ambayo inasema mabasi ya abiria kusafiri masaa 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la saa 24, tumekaa na wenzetu wa Jeshi la Polisi na baada ya kujiridhisha kwamba usalama upo, tukatoa masaa kwamba yaanze kusafiri saa 11.00 alfajiri badala ya saa 12.00. Baadaye tukatoa tena, baadhi ya mabasi yapatayo 68 kwamba tuanze kusafiri kuanzia tisa alfajiri na hii inafanyika. Tunakoelekea ni baadhi ya mikoa. Tunategemea mikoa yote tuanze kufanya hivi, lakini hadi hapo tutakapopata taarifa kamili za kiusalama kwamba inaruhusiwa kusafiri masaa 24. Kwa hiyo, tumeanza kama pilot study lakini tunaendelea na hadi hapo tutakapoanza kusafiri kwa saa zote 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja nyingine ya TRC kuhusu miundombinu ya Reli ya MGR. Ni kweli kwamba reli yetu ya kisasa inajengwa, na pia tuna reli ambayo ndiyo inafanya kazi hivi sasa. Tumeendelea kuiboresha na kuikarabati hususan katika maeneo ya kutoka Kaliua – Mpanda ambapo imegharimu takribani zaidi ya shilingi bilioni 357 na mkandarasi yupo site na njia ya kutoka Dar es Salaam mpaka Tabora tunaendelea kuikarabati. Kwa maana hiyo, hadi kutoka Tabora – Kigoma tutaendelea kuikarabati kwa kuwa pia kuna mkandarasi ambaye yuko site kwa reli hii ya MGR.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kulikuwa kuna hoja za SGR ya kutoka Dar es Salaam – Morogoro yenye kilometa 300. Tayari tumefanya kwa asilimia 98.14 na 2% zilizobaki ni kwa ajili ya kuunganisha pale bandarini. Tuna hakika ifikapo mwezi wa Tisa mwaka huu, kadiri mkataba ambao tumesainiana na mkandarasi, eneo la kutoka Stesheni Kuu - Posta kwenda Bandarini litakuwa imekamilika. Hivyo asilimia 100 ya reli hii kwa kipande hiki cha Dar es Salaam – Morogoro kilometa 300 kitakuwa kimekamilika chote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepokea mabehewa ya kisasa ya mfano na ya ghorofa ambapo mabehewa haya yataanza kutumika ifikapo mwezi wa Saba mwishoni, mara tutakapokuwa tumepokea vichwa vya umeme vya kuendeshea mabehewa haya. Kwa hili nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu katika historia ya nchi ya Tanzania, tutaanza kutumia mabehewa ya ghorofa ya kisasa na bora kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Morogoro mpaka Makutupora yenye kilometa zaidi ya 422 tuko asilimia 93. Tunategemea pia ifikapo mwakani reli hii tutakuwa tumeikamilisha na kutoka Makutupora – Tabora kilometa 368 tupo 7%, kutoka Tabora – Isaka kilometa 165 tuna 3%, Isaka mpaka Mwanza kilometa 341 tuko asilimia 31 na kutoka Tabora mpaka Kigoma tayari mkandarasi yupo site na anaendelea na mobilization kwa maana ya kujenga camp. Hii yote ni kutaka kuunganisha pande zote za nchi yetu kutoka Ziwa Victoria mpaka Dar es Salaam baharini; kutoka Ziwa Tanganyika mpaka Dar es Salaam baharini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo hata kwa wenzetu wa Mtwara Corridor (ushoroba wa Mtwara) mara nyingi imeulizwa maswali hapa kwamba ni lini reli ya SGR itaanza? Nataka niwahakikishie mikoa yote ya Mtwara, Lindi pamoja na Ruvuma kwamba reli hii yenye kilometa 1,000 ilishafanyiwa upembuzi yakinifu. Sasa tayari makampuni zaidi ya kutoka nchi tano yameonesha nia ya kuwekeza katika reli hii. Kikwazo kikubwa ilikuwa ni kwa namna gani sheria yetu ile ya ubia tuweze kuiboresha. Tayari ile sheria imeboreshwa na Waheshimiwa Wabunge mliipitisha wiki iliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kazi iliyopo, mara baada ya Mheshimiwa Rais kusaini sheria hii, tayari wakandarasi na makampuni kutoka hizo nchi wapo kutoka Uingereza, Marekani, Afrika Kusini, Croatia, Morocco na nchi nyingine. Wote wameonesha nia ya kuja kuwekeza katika Standard Gauge katika mikoa hii ya ushoroba wa Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la meli katika Ziwa Tanganyika. Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi, ninyi ni mashahidi, tumekaa kikao takribani zaidi ya masaa matatu mpaka usiku kujadili ni namna gani wananchi wetu waliopata shida kwa miaka mingi na wengine wengi wamepata changamoto ya usafiri katika Ziwa Tanganyika, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Bajeti ya mwaka ujao imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa meli kubwa mbili za kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushauri wa Waheshimiwa Wabunge katika maeneo hayo, walishauri badala ya kuwa na meli moja ya kubeba abiria 600 na tani 400 ya mizigo, ni bora tuwe na meli mbili. Hili ndilo ambalo limetufanya tusisaini mkataba ambao tayari tulishampata mkandarasi, lakini ile meli ya mizigo yenyewe tutaendelea kuitengeneza na pia tutaendelea kusaini mkataba wake. Kwa maana hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge katika mikoa hiyo kwamba katika Bajeti ijayo, nina hakika kwamba tunakwenda kuboresha usafiri katika Ziwa Tanganyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na suala la viwanja vya ndege. Waheshimiwa Wabunge wengi wameuliza, kwa nini ndege zetu ikifika saa 12.00 jioni, muda wa giza ukiingia nazo zinatua? Katika Bajeti ijayo tunakwenda kukarabati viwanja visivyopungua 15 na vingine ambavyo vinafanya kazi sasa. Tunaanza na kiwanja cha kwetu hapa Dodoma ambacho hakina taa. Sasa hivi taa zilizopo ni za solar, haziwezi kufanya kazi masaa 24. Kwa hiyo, kuna mkandarasi ambaye sasa hivi anaweka taa za kuongozea ndege usiku na mchana. Ifikapo mwezi wa Nane kiwanja hiki kitakuwa na taa, na tuna hakika tutakuwa tunatua usiku na wakati wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa mingine ambayo tunakwenda kuboresha viwanja hivyo ni pamoja na Mkoa wa Lindi na Iringa ambapo yuko mkandarasi. Kwa awamu ya kwanza Serikali imetoa fedha, lakini awamu ya pili Benki ya Dunia ndiyo itakayokamilisha majengo pamoja na kujenga control tower. Vile vile kuna Mkoa wa Tanga, Sumbawanga, Kigoma, Musoma, Bukoba ambako tutajenga control tower, kuna Mkoa wa Arusha ambapo tunategemea tujenge taa za kuongozea ndege, nako hakuna taa, na pia kubadilisha runway kwa sababu iko karibu sana na barabara, ile barabara tutaihamishia upande wa pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo la Chato, Msalato, Moshi ambako kuna mkandarasi lakini naye tutaendelea kumwezesha ili akamilishe Kiwanja cha Ndege cha Moshi Mjini. Kuna Shinyanga, Kahama, Mpanda, Songwe, Songea, Mtwara, JNIA, Mwanza na Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumepokea ndege ya mizigo yenye kubeba tani 54. Ni furaha iliyoje kwamba sasa ndege yetu itaanza kazi rasmi kuruka katika maeneo mbalimbali kwa maeneo ambayo tumekubaliana kuanzia tarehe 26 mwezi huu wa Sita. Tutaanza kuruka kwenda Kinshasa, Comoros, Lusaka, Harare, India, Dubai, Lubumbashi pamoja na Entebbe. Hii ni fursa kubwa kwetu kwa kuendelea kuwekeza katika mazao, kwa maana ya ndege hii itakapokuwa inabeba mizigo, tunategemea tukauze, lakini pia kuwe na mizigo ya kuja ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona tushiriki kuchangia katika hotuba hii katika haya ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wameuliza. Pia kuna reli ya kisasa kutoka Uvinza – Msongati – Itega yenye urefu wa kilometa 367 ambayo inafadhiliwa, ama itajengwa kwa ufadhili wa African Development Bank na tayari tupo katika hatua za manunuzi. Lengo kubwa la reli hii ni kwenda kuchukua malighafi zilizopo nchini Burundi (Nickel) na kuunganisha na reli yetu ya kisasa itakayokuwa inajengwa kutoka Tabora kuja Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja na ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)