Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye Mapendekezo ya Bajeti yaliyowekwa hapa mbele. Nianze kwa kusema, naunga mkono hoja mapendekezo haya, kwa sababu bajeti hii imelenga kumkomboa mwananchi na ndiyo maana Wabunge wengi waliochangia wanasema ni bajeti ya wananchi. Waziri wa Fedha na timu yako, hongera sana kwa kazi nzuri mliyofanya ya maandalizi ya bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kwa nguvu zote mapendekezo haya kwa sababu Sekta ya Mawasiliano ziko hatua kubwa sana zimependekezwa kwenye mapendekezo ya Bajeti hii na sisi watu wa Sekta ya Mawasiliano tunayaunga mkono na kuwashawishi Wabunge wayaunge mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kuna jambo la msingi linazungumzwa kwenye Mapendekezo ya Bajeti hii, kuhusu kupeleka nchi yetu kwenye cashless economy, kwenye uchumi ambao hatutumii hard cash. Nimewasikia Wabunge wakiliunga mkono jambo hili. Jambo hili kubwa litaipeleka nchi yetu kuwa moja ya nchi ambazo zinafanya vizuri kwenye eneo hili la uchumi wa kidijitali. Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwa kutupeleka kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna fedha zimetengwa za uwekezaji kwenye Sekta ya Mawasiliano. Tunaendelea kujenga mkongo, kupitia bajeti hii kuna fedha zimetengwa za kuunganisha nchi yetu na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na maeneo mengine ya uwekezaji kwenye Sekta ya Mawasiliano. Mheshimiwa Waziri ahsante kwa usikivu, wewe na timu yako kwa kutenga fedha kuendelea kuwekeza kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni hatua za kikodi ambazo zimependekezwa kwenye bajeti hii ambapo hatua hizi zitaenda kusaidia kushusha gharama za mawasiliano katika nchi yetu. Mheshimiwa Waziri nakushukuru na kukupongeza kwa kuitikia wito na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia. Rais Samia alituelekeza; moja, tuhakikishe Sekta ya Mawasiliano inatulia katika nchi yetu. Tukachukua hatua, na kumekuwa na kelele kwamba kumekuwa na gharama kubwa za mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza ilikuwa ni kuzuia gharama zisiendelee kupanda. Nilisikia juzi baadhi ya Wabunge walikuwa wakilijadili jambo hili, lakini toka mwezi wa Kumi mwaka 2022, miezi tisa mpaka sasa gharama za mawasiliano kwenye nchi yetu hazijaongezeka, na hazijapungua bundle. Toka Mwezi wa Kumi mwaka jana. Kuna hatua zilichukuliwa na ndiyo maana hali ikatulia. Kwa hiyo, mtu leo akisema kuna gharama zimepanda, kwa kweli ni kupotosha. Kwa miezi tisa haijaongezeka kitu, hakijapanda chochote kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua hatua ya kutuliza gharama zisiendelee kupanda. Hiyo ilikuwa hatua ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ilikuwa ni kuzishusha gharama hizo sasa. Kwenye mapendekezo hapa, liko pendekezo kubwa la msingi sana. Gharama za mawasiliano nchini zinachangiwa na gharama ya uwekezaji. Uwekezaji kwenye miundombinu. Hapa watu wa mawasiliano tulikuwa tunalipa Dola 1,000 kwa kilometa kwa mwaka tukipitisha miundombinu ya mawasiliano kwenye road reserve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yaliyoletwa kwenye bajeti hii na ndiyo maana sisi watu wa mawasiliano tunayaunga mkono. Yako mapendekezo ya kuitoa dola 1,000 kwa mwaka kupeleka dola 100 kwa mwaka ambalo ni punguzo kubwa sana litapunguza gharama ya uwekezaji na ndiyo maana nasema hatua ya kwanza ilikuwa ni kutuliza gharama zisiendelee kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ni kuchukua hatua za kuzipunguza gharama na haya mapendekezo bila shaka ya kikodi hili la kushusha kutoka dola 1,000 kwenda dola 100, kutoka dola 1,000 kwenda dola 200 kama initial investment ni uamuzi wa busara utatuondoa kwenye gharama hii kubwa ambayo tumekuwa tukiitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za uwekezaji, gharama za mawasiliano moja ni hizo gharama za uwekezaji zilikuwa zinatupeleka kwenye tatizo kubwa la kuwa na gharama kubwa ya mawasiliano. Lakini ya pili kuna gharama za uendeshaji, Gharama za uendeshaji leo ukiendesha mnara mmoja wa mawasiliano kwa kutumia diesel unauendesha kwa shilingi 1,800,000 kwa mwezi lakini ukiunganisha huu mnara na umeme unauendesha kwa shilingi 400,000 pekeyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Bajeti hii imeelekeza upelekaji wa umeme kwenye vitongoji na Rais alielekeza kwamba umeme huu ukipelekwa uende ukaweke kipaumbele kwenye maeneo ya mawasiliano na sisi tunaamini gharama hizi sasa umeme huu ukifika tutaondoka kwenye kuendesha mnara mmoja kwa shilingi 1,800,000 mpaka kwenda kuuendesha kwa shilingi 400,000 na hizi ndiyo hatua ambazo zitashusha gharama za mawasiliano katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ninaunga mkono mapendekezo haya ambayo yameletwa hapa na ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wa kuelekeza uwekezaji huu mkubwa kwenye eneo hili kubwa la mawasiliano ili tumuunganishe kila Mtanzania na hasa wale walioko vijijini ambao hizi huduma zitaenda kubadilisha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa mapendekezo haya na kwa hatua hizi na ni matumaini yangu kwa sababu bado kodi kwenye huduma za mawasiliano bado ziko juu. Katika kila shilingi 100 tunayolipa, shilingi 41 inakwenda kwenye kodi. Uamuzi huu wa kuondoa hii ni uamuzi wa awali. Ni matumaini yangu kwamba Waziri tutaendelea kuzungumza tuendelee kufanya mapitio kama ambavyo Rais Dkt. Samia ameelekeza, kadiri tutakavyokuwa tukiwekeza, kadiri tutakavyokuwa tukiongeza miundombinu na hizi gharama tuendelee kushuka ili Watanzania waendelee kufaidi huduma hizi za mawasiliano katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii wakati namalizia kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kujenga nchi yenye kupenda haki. Ameunda timu imezunguka nchi nzima kukusanya maoni na kutuletea kuona namna ya kuboresha Hakijinai katika nchi yetu. Hatuna njia nyingine, haki ndiyo itakayoinua Taifa letu. Tukitenda haki watu wetu watapata haki, Taifa letu litastawi, Taifa letu litanawiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja iliyopo mezani na ninaomba Wabunge wenzangu tupitishe Bajeti hii kwa sababu imelenga kugusa na kuboresha maisha ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)