Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rombo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii na mimi ya kuchangia Hotuba hii ya Bajeti Kuu ya Serikali. Naomba nitangulie kusema naiunga mkono 100% na ni matumaini yangu kwamba Wabunge wote kabisa tutaunga mkono hoja hii ya Waziri wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwanza kwa kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa mapendekezo mazuri sana yaliyoko kwenye Bajeti Kuu pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Hamad Hassan Chande, Katibu Mkuu Dkt. Natu, Naibu Makatibu Wakuu, Kamishna wa Bajeti na wengine wote kwa sababu wameleta mapendekezo mazuri na nitazungumzia kidogo kwenye Sekta ya Elimu na baadaye nitajibu hoja moja tu iliyotolewa ambayo ni kubwa kwenye suala la elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote hawa katika maandalizi yao kwa kweli wamejitahidi sana kulenga yale maono ya Mheshimiwa Rais aliyoyaelekeza na kama tunavyoona katika Bajeti na kama alivyosema Mheshimiwa Waziri hapa kuna vipaumbele ambavyo Mheshimiwa Rais aliviweka. Elimu ni kati ya kipaumbele kikubwa sana cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa hilo kwa kweli nadhani tumpongeze sana Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua ni rahisi sana kutafuta vitu ambavyo matokeo yake unayaona sasa hivi lakini katika mageuzi ya elimu kama nitakavyosema hapo baadaye matokeo yake huwezi kuyaona mapema. Wanasema kwamba a politician focuses on the next election; a state man focuses on the next generation. Rais wetu anaangalia na vizazi vijavyo kwa jinsi ambavyo ameamua kuwekeza katika elimu. Baadhi ya matokeo ya mageuzi haya yatakuja wakati 2030 ameshamaliza urais wake amepumzika na matunda yake yataonekana mbele ya safari. Kwa kweli Rais wetu lazima tumpongeze sana kwa maono yake haya na hii Bajeti kwa kweli inazingatia maelekezo ya Rais wetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba nakushukuru na kukupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitataja baadhi ya maeneo ambayo wote tunajua. Tunafahamu na wote tumesikia elimu bila ada. Kuna baadhi ya watu wanadhani ile ada ni ndogo sana na wengine wanadhani kwamba pengine kuondoa ada kuna madhara katika elimu lakini tukumbuke tulivyoanza tu Serikali ilivyoanza kuondoa ada kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, tulishangaa wanafunzi waliosajiliwa mashuleni idadi iliongezeka kwa ghafla sana kuonyesha kwamba kumbe tulikuwa tunaacha baadhi ya wanafunzi wanashindwa kwenda shuleni kwa sababu ya ada hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alivyoingia madarakani mara moja aliamua kuongeza elimu bila ada kwenda form five na form six na vilevile kuondoa ile ada ya mitihani ambayo kwa kweli inanufaisha familia nyingi ambazo vinginevyo baadhi ya wazazi walikuwa wanajaribu kushawishi watoto kwamba jitahidi usifaulu sana kwa sababu sina hela za kukupeleka shuleni. Tunamshukuru sana Rais wetu na tunashukuru sana Waziri wa Fedha kwa kutekeleza maagizo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine tunajua kwa mfano, ongezeko la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Tunajua kwamba wakati Mheshimiwa Rais alivyoingia alikuta ni shilingi bilioni 464. Hakuacha nyongeza iende progressively, jump kubwa imeshafanyika sasa hivi mikopo ya elimu ya juu imefikia shilingi bilioni 731. Hilo ni ongezeko kubwa sana lakini zaidi ya hapo katika bajeti hii inabeba ongezeko la fedha ambazo wanafunzi wanazipata kwa siku kutoka shilingi 8,500 mpaka shilingi 10,000 na haya yalikuwa maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Rasi baada ya kukutana na uongozi wa wanafunzi wa elimu ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kingine ambacho kinaonekana ni fedha kidogo sana, Samia Scholarship. Mnakumbuka wakati tulivyokuja hapa mwaka jana kuomba fedha hapa tuliomba tutenge fedha kwa ajili ya kutoa scholarship kwa wanafunzi wanaofanya mtihani wa form six kupitia Baraza la Mitihani wafaulu vizuri sana kwenye masomo ya sayansi na wakubali kwenda kusoma sayansi (engineering au medicine). Mliipitisha Waheshimiwa Wabunge hapa tumeiweka ile sisi baadaye Wizarani tukasema tuiite Samia Scholarship. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shilingi bilioni tatu tulipitisha mara ya kwanza na sasa hivi tumetengewa tena fedha nyingine. Kwa hakika imetushangaza jinsi ambavyo wanafunzi sasa hivi wanaonyesha mwamko mkubwa wa kusoma masomo ya sayansi na Taifa haliwezi kuendelea bila kuwekeza katika sayansi, teknolojia na ubunifu. Kwa hiyo, hata hilo nashukuru sana Waziri wa Fedha kwa sababu maelekezo ya kutoa fedha hizi kwa ajili ya scholarship yalikuwa maelekezo ya Rais wetu. Kuiita Samia scholarship tuliamua sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hii ni Bajeti ambayo inaenda kutekeleza kazi ya ujenzi wa zile kampasi mpya za vyuo vikuu katika maeneo chungu mzima ambayo yalikuwaga hayana kampasi ya vyuo vikuu. Mikoa kama Tabora, mahali kama Singida, sehemu kama Tanga. Mikoa yote hiyo sasa hivi itaenda kuwa na kampasi za vyuo vikuu, tunaenda kutekeleza ujenzi wa vyuo vikuu 14, mchakato unaenda vizuri sana. Kuna mchakato mrefu kidogo katika taratibu hizi na World Bank lakini tunaenda vizuri na utekelezaji wake umebebwa na Bajeti hii ndiyo maana naomba sote tuiunge mkono na tuiunge mkono kwa 100%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Bajeti hii inayotusaidia kwenda kuendeleza ujenzi wa vyuo vya VETA ambavyo tunavijenga katika nchi nzima katika takribani wilaya 64 pamoja na Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe. Najua Wabunge wengi wote ni wanufaika wanafahamu ujenzi unaoendelea kule sasa hivi na Waziri wetu wa Fedha kwanza mwaka jana alipewa maelekezo na Rais wetu tena baada ya Bajeti ya Wizara ya Elimu kwamba hebu kaongeze ujenzi wa vyuo vya VETA na sasa hivi ametenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo. Tunampongeza sana Waziri wetu huyu kwa kutekeleza maelekezo ya Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika Bajeti hii, kilio kikubwa kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba tuanze kuwaangalia wanafunzi wanaoenda vyuo vya kati ambavyo tunasema vinatoa elimu ya amali (mafunzo ya kazi moja kwa moja) ili wanafunzi wengi waweze kumudu kwenda kusoma kule. Waziri wa Fedha ametenga fedha kwa kuondoa ada katika baadhi ya course wanafunzi wanaotoka kidato cha nne kwenda kusoma DIT, kusoma Arusha Technical, na MUST. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wanaweza wakaenda kusoma kule bila ada tunapongeza sana Wizara ya fedha na mnaelekezwa na Rais wetu ni mwendelezo wa kukuza elimu ya amali ambao wako katika moyo wa mageuzi ya elimu na kadhalika. Kuanzisha programu ya kutoa mikopo sasa kwa vyuo kadhaa vya kati ambavyo ni ubunifu mwingine umeletwa na Wizara yetu ya Fedha kutekeleza maelekezo ya Rais wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kusema, kwa upande wa mageuzi ya elimu bajeti hii vilevile imebeba bajeti ya kuanza safari ya mageuzi ambayo tumekuwa tukiyajadili hapa. Mageuzi haya kama mnavyofahamu yalikuwa ni maelekezo mahususi ya Rais wetu. Alivyoapishwa tu, nadhani wakati alifanya mabadiliko kidogo katika Baraza la Mawaziri, alianza kuelezea anachotaka kuona katika elimu. Siku ile alikuwa anapitia wizara moja hadi nyingine, wakati huo Mheshimiwa Profesa Ndalichako alikuwa Waziri wa Elimu alisema hapa Wizara ya Elimu nataka nione mageuzi ya elimu, mitaala na bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ndalichako ananiona pale kazi hiyo inatekelezwa. Kwa hiyo watu wakisikia tunamsifu Rais wetu wajue tunamsifu hata wenyewe wanaweza waka-verify. Maelekezo mengine hamuyasikii wote lakini haya yalisemwa hadharani na alikuja akaahidi hapa Bungeni kwamba Serikali anayoiongoza itafanya mageuzi makubwa. Bajeti hii itatuanzishia safari hiyo, kwa hiyo naombeni sana tuiunge mkono kwa asilimia 100 utekelezaji wa mageuzi hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa labda niseme kitu kimoja na hili suala lililetwa na Mheshimiwa Janejelly James kuhusu wanafunzi wanaorudi kutoka nchi ambazo zina matatizo ya vita. Wanafunzi waliotoka Ukraine kwa sababu ya vita kati ya Ukraine na Urusi na wanafunzi wanaotoka Sudani kwa sababu ya machafuko ya hali ya hewa. Nitangulie kusema nchi yetu imebaki ya amani hili tulikumbuke siku zote, tunapoona changamoto hizo, wanafunzi wanarudi hapa wanatafuta mahali pa kusoma, tukumbuke vilevile nchi yetu ina amani na amani hii inatokana na jinsi tunavyoendesha siasa zetu, kwa ustarabu, kwa kuheshimiana, kwa kuunga mkono viongozi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa alichouliza Mheshimiwa Janejelly James ilikuwa ni kwamba sasa tumeona wanafunzi chungu mzima wameenda Muhimbili kutoka Sudan. Wale wa Ukraine vipi? Kwa nini wale hawajapata fursa ya kujiunga na vyuo vikuu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitolee maelezo kidogo jambo hili na Watanzania wengine wote wasikie. Wanafunzi waliokuwa wanasoma Ukraine, baadhi yao, si wote, waliomba kujiunga na vyuo vyetu na utaratibu unaoitwa credit counselor ukafanyika. Baadhi yao wameweza kujiunga na vyuo vyetu, si wote. Kwa sababu utaratibu wa kuhamisha masomo unayosoma Chuo Kikuu kimoja kuja chuo kikuu cha ndani unasimamiwa na TCU. Kuna vigezo vingi sana vinaangaliwa baadhi yao ya wale walioomba walienda kusoma Ukraine wamejiunga na vyuo vyetu na sio wote walioomba kuja huku. Kwa wale waliotoka Sudan mpaka sasa hivi hakuna hata mmoja ameweza kujiunga na chuo chetu. Mchakato unaendelea najua kesho kuna vikao vinaanza kwa wale ambao wanataka kujiunga na vyuo vyetu ili tuangalie utaratibu wa credit transfer waweze kuhamisha masomo yao kutoka Sudan kuja hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale walioonekana kwenye picha walipokelewa na Profesa Janabi Hospitali ya Muhimbili sio MUHAS. MUHAS Vise Chancellor anaitwa Profesa Pembe. Wale wanafunzi waliotoka University of Medical Science and Technology Sudan; wameshasoma miaka mitano wamekuja kwa ajili ya clinical trial kwa ajili ya clinical training na huu ni utaratibu. Tumepokea wote wanafunzi kutoka Zimbabwe ambao wamemaliza masomo yao ya medicine wanakuja hapa kuomba kufanya kazi kwenye hospitali zetu wapate certification halafu wanaenda ku-graduate kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanafunzi tuliowaona wameenda Muhimbili tunawatakia kila la heri tunafurahi wamekuja nchini kwetu, watafanya clinical training hapa Tanzania, na watakapomaliza watarudi kwenda kuhitimu kwenye vyuo vyao. Hao wengine walioomba tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu. Tungependa wote tuweze kuwa- integrate of course kuna changamoto. Kuna wengine kuna criteria zilizotumika kuwa-admit katika vyuo vyao kule sio criteria ambazo sisi tunatumia kuwa-admit wanafunzi huku. Kwa hiyo ni changamoto ambayo TCU inafanya. Najua kutakuwa na vikao kushirikiana na Wizara ya Elimu ya Zanzibar na kwetu na TCU kuona kwa wale wanaotaka kujiunga na vyuo vyetu tutatumia utaratibu gani. Kwa hiyo mpaka sasa hivi kwa kweli hatujaweza kuwachukua wale wanafunzi lakini navyojua nina taarifa kwamba kuanzia kesho kuna vikao vitaanza kuona namna ya kuwa- integrate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalize hapo narudia tena naunga mkono hoja hii ya Waziri wa Fedha na naomba wote tuiunge mkono asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)