Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami kuwa sehemu ya wachangiaji katika hoja iliyoko mbele yetu. Awali ya yote, ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya uzima wa afya ambayo ametujalia, tumekaa hapa, hatimaye tunaenda kufikia ukingoni kwa hoja hii iliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba sana nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumpongeza sana. Mheshimiwa Rais, mbeba maono wa Taifa hili, mwenye macho haambiwi tazama. Mbeba maono maana yake siyo tu kwamba anahamisha sera kutoka kwenye makaratasi na kuzipeleka kwenye vitendo, bali hata salamu mama anaipeleka kwenye vitendo ana uwezo mkubwa sana wa kutafsiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliposema Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee, hiyo ni salamu. Tumeona leo dhahiri kabisa salamu hii imetafsiriwa kwa vitendo, hakuna Wilaya, hakuna Halmashauri ambayo hakuna maendeleo au mradi wa maendeleo ambao unafanyika kule. Miradi yote mikubwa tuliyonayo inatekelezwa kama SGR, umeme mpaka vijijini, Bwawa la Mwalimu Nyerere, mama ameenda kulitekeleza kwa vitendo. Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi na hii haikuja burebure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais yeye ni neema na ni baraka kutoka kwa Mungu. Kwani ukiniruhusu naweza toa tafsiri kwa ufupi tu. Jina la Mama anaitwa Samia Suluhu Hassan, utanisamehe naenda kwenye kiarabu kidogo, watu wa nahau wanasema “inna samian suluhuun hassanaah” kwa hakika Mama huyu ni msikivu wa kusikiliza changamoto za wananchi wake na kuzipatia ufumbuzi mzuri hiyo ndiyo tafsiri yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wilaya zote leo lipo vumbi linapeperuka kwa sababu ya ujenzi wa barabara, ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, lakini ujenzi wa madarasa, kila kitu. Hii kwa sababu ya tafsiri la jina lake haikuwa bure bure, hii ni neema. Kwa hakika Mama ni msikivu ambaye anasikiliza changamoto za wananchi wake na kuzipatia ufumbuzi ulio mwema. Siku ukiwa na muda mzuri tunaweza kutia irabu kwamba inna ni nini, samian ni nini? na suluhu ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ni mbeba maono kweli kweli. Nimpongeze sana na kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Waziri Mkuu. Viongozi wetu hawa wanasimama imara kutuelekeza na kusimama imara katika kujenga maendeleo ya Taifa letu hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Wahenga hunena: “kijua ni hiki tusipouanika tutaula mbichi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, nikisema hivyo mnanifahamu? Huu ndiyo wakati, huu wakati wa leo, sasa ndiyo wa kujenga maendeleo yetu, ndiyo wa kuchagiza maendeleo ya nchi hii. Ni wakati huu na siyo wakati mwingine, ndiyo maana unasema kijua ni hiki usipouanika utaula mbichi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wangu, Dkt. Mwigulu Nchemba, mentor wangu, bosi wangu, kwa kiasi anavyonikuza kisiasa lakini na kikazi. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Mungu akubariki sana. Wewe ni mtu mwema sana, ni mtu wa kipekee, nakushukuru sana na nakuhaidi kwamba nitaendelea kushirikiana na wewe katika utendaji wa kazi pamoja na wataalam wetu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza sana Wabunge, Waheshimiwa Wabunge nawashukuru sana kwa namna wanavyotushauri, kutuelekeza lakini hata kutoa mapendekezo yao, hongera sana kwa Waheshimiwa Wabunge. Kwa nini nawapongeza Waheshimiwa Wabunge? Waheshimiwa Wabunge wanaishi katika maneno ya hekima yaliyosemwa kwamba aliyekufanyia wema, basi mlipe mithili ya wema aliyokutendea, kama huwezi kufanya vile basi mwombee dua, mwombee kwa Mungu. Waheshimiwa Wabunge wanaishi katika hekima hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maneno yalisemwa kwa Kiarabu; “Tatamanswana maarufa alaykum au manswanaa alaykum maarufa fakatiuhu,” maana yake aliyekufanyieni wema mlipeni “fainlam tajiduu” mtakapokuwa hamuwezi basi “swallu alaiy, mwombeeni dua. Waheshimiwa Wabunge nyinyi mnaishi katika hekima hii, kila Mbunge aliyenyanyuka alimshukuru na kumpongeza na kumwombea dua Mama yetu, kila Mheshimiwa Mbunge. Wabunge wote mnaishi katika hili, Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, nasikia, huko mitandaoni, nasikia, toba sikio. Wako wanaosema kwamba wanabeza Bunge, wanabeza Bunge hili, wako wanaobeza Bunge hili, lakini niwaambie Wabunge taingia katika historia maalum, ya wakati maalum, ya siku maalum na kwa tukio maalum. Majina yenu yataandikwa kwa wino mahususi, wino wa dhahabu, kwa sababu wamechapa kazi sana, nani ambaye haoni leo Waheshimiwa Wabunge wanavyopambana? Ni Wabunge wangapi leo siku zote maana yake ukiamka tu asubuhi simu wanadai maendeleo ya Majimbo yao. Waheshimiwa Wabunge hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze wataalam wetu wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Natu Mwamba na Manaibu Katibu wakuu na Wataalam wote nawapongeze sana, kwani usiku na mchana hawa wanafanya kazi. Wanafanya kazi mpaka usiku wa manane na asubuhi mapema kabisa wameshafika ofisini, nisiwe mchoyo wa fadhila, niwashukuru sana wataalam wetu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya salamu hizo, naomba tu niseme kwamba ushauri wote ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge, mapendekezo na maoni tumeyapokea na tunawahakikishia tunaenda kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni wa dondoo ndogondogo ndiyo hoja ambazo zimetajwa na Waheshimiwa Wabunge niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge. Walipokuwa wanachangia wengi wametoa hoja kwa njia ya ushauri, wametumia hekima kubwa sana, hongera sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja moja ambayo ilizungumzwa Serikali ihakikishe kwamba inafuatilia au inatafuta mikopo ya gharama nafuu. Serikali imekuwa ikifanya juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba mikopo yote ambayo inaingia Serikali ni ile yenye masharti nafuu na tunawahakikishia kabisa mikopo hii inaenda kutumiwa katika zile sehemu ambazo ni vipaumbele vya Taifa hili ya mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026. Vipaumbele vya Taifa hili ambavyo tumeviweka ndiyo mkopo huu unaenda kutumika, hautotumika tofauti na vipaumbele ambavyo tungeweka ili kusudi kupunguza gharama ambazo siyo za lazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo hoja imesemwa kwamba Serikali iboreshe mikakati na ikusanye mapato ya ndani ili kuhakikisha sehemu kubwa ya bajeti inagharamiwa na mapato ya ndani. Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuongeza wigo wa mapato kwa kusajili biashara na walipa kodi wapya. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaandaa mikakati maalum, tutaendelea kuitumia mikakati ambayo imeandaliwa na Serikali kuhakikisha kwamba tunapata ongezeko kubwa sana la mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matarajio yetu ambayo tumeweka, ni kupata mapato ya ndani kwa asilimia 70.7 ikilinganishwa na bajeti iliyopita au ambayo tuko nayo leo ya kupata asilimia 67.5. Niwahakikishie kwamba tutapambana, tutajitahidi kutumia maarifa yetu yote, tuone kwamba ongezeko la mapato limepatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu sisi wote tuwe mabalozi wa kuwa na utamaduni mwema. Tuwe na utamaduni wa kudai risiti na kutoa risiti kwa wale wafanyabiashara. Tufanye kama utamaduni wetu, kama vile ukiamka asubuhi unaenda kukosha uso, kupiga mswaki na kukoga, basi tufanye hivyo, kila unapokwenda dukani kutafuta bidhaa yoyote, basi dai risiti na wale wanaofanya biashara watoe risiti jambo hili litatusaidia sana. Hakuna mtu anayetoka mbali kuja kujenga maendeleo yetu kama siyo sisi wenyewe. Kilio kina mwenyewe, wewe mwenyewe ndiyo unajua uchungu wa nchi yako. Kwa hiyo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tuwe mabalozi wa kujitahidi kudai risiti na pia nakutoa risiti kwa wale wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo Waheshimiwa Wabunge wametoa hoja ya wakandarasi kwamba kuna madeni mengi sana ya wakandarasi. Tulikuwa tunateta hapa na Mheshimiwa Waziri. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba wakandarasi hao ambao certificate zao tayari zimeshawiva, mapema mwaka ujao wataenda kulipwa bila wasiwasi wowote. Serikali yetu iko tayari kuwalipa wakandarasi hao hasa hasa wale wakandarasi wadogo ambao tukiwaachia muda mrefu hawajalipwa wanaweza kufilisiwa kama walivyosema Wabunge. Hilo halitotokea katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nimalizie kwa kusema kwamba, Waheshimiwa Wabunge baadhi yao wapo wamezungumzia hoja ya kujengewa ofisi za TRA au Forodha mipakani. Niwahakikishie, kwa mfano kama Loliondo, Iramba kwa bosi wangu, Mkalama, Itilima na kwingine ofisi hizi zitaenda kujengwa hivi karibuni, mwaka wa fedha unaofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme naunga mkono hoja. Wale waliosema mama apewe maua yake mimi naongezea siyo tu maua, mama apewe maua yake na matunda yake yale yaliyo mema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)