Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijalia na mimi kuchangia katika hoja iliyopo mezani. Katika falsafa ya uchumi wanazungumza hivi, we need to plan for future and not for wait and see attitude. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Mtwara, Mkoa wa Ruvuma ndiyo mikoa ambayo iliachwa nyuma katika maendeleo, hasa katika suala la miundombinu, lakini Mwenyezi Mungu hii mikoa ameipa neema kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na Mkoa wa Lindi. Tumeingia katika uwekezaji mkubwa wa viwanda vya LNG na kutoa nafasi kubwa kwa wawekezaji kwenda kuwekeza katika Mkoa wa Lindi. Cha kusikitisha, kwa nini ninasema we don’t plan for future we are planning for wait and see attitude, kiwanja cha ndege kiko karibu na uwekezaji wa viwanda, hakimo ndani ya kitabu hiki. Sasa unajiuliza, mwekezaji anahitaji kutoka Dar es Salaam kwenda Kikwetu, uwanja ambao ni mkubwa, wa pili katika Afrika, ule uwanja ulikuwa unatumika, ndege zikitoka Ulaya zinateremka Kikwetu, zikitoka Kikwetu zinakwenda South Africa, angalieni ndani ya Encyclopedia Britannica inakupa taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ule uwanja umetupwa kwa miaka yote 50, halafu mnakwenda kuwekeza maeneo hayo. Hapa mmetufunika tu, tutakwenda kurekebisha uwanja wa ndege wa Kikwetu, sijui wa Lindi, wa Kilwa, tumejipanga? Hatujajipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuingia katika uwekezaji mkubwa wa gesi na tumeambiwa Tanzania tumepata trilioni tano gesi, lakini hatuna uwekezaji katika eneo lile, hata uwanja wa ndege haupo. Wanataka kutumia viwanda Bandari ya Lindi haipo, Bandari ya Kilwa haipo, Airport ya Kilwa haipo, tunawekeza nini hapo? Hizi ni bla bla.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja suala la mawasiliano. Huamini ukifika Airport ya Kikwetu hakuna mawasiliano. Wanapoweka Kiwanda cha Likong‟o hakuna mawasiliano, huyo mwekezaji anakuja kufanya kazi gani pale? Bila kuwa na mtandao anafanya kazi gani? Wanakwenda kisasa, wanakwenda kidijitali sisi tunakwenda kianalogia, tumefika katika uwekezaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli. Katika maisha yangu sijapata kusikia tatizo lililofanyika reli kutoka Mtwara ikang‟olewa, waling‟oa kwa sababu gani? Kwa nini wasingeiacha? Leo tunataka kuwekeza katika mazao ambayo yatatoka Nachingwea, Liwale, Ruangwa yanapelekwa Bandari ya Mtwara, reli hamna. Wananchi wanaingia katika kutumia gharama kubwa ya kukodi magari kupeleka ufuta wao ukanunuliwe Mtwara wakati reli ilikuwepo Nachingwea. Hapa sijaiona reli ya Nachingwea inarudishwaje pale ili kuwarahisishia wananchi waweze kuingia katika hali bora ya maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia suala la barabara katika mikoa ya kusini. Katika ilani na ahadi zilizotolewa na Rais kuwa barabara ya kutoka Nangurukuru kwenda Liwale mpaka Nachingwea itapatikana lami. Leo mtu anakwenda Liwale, sasa hivi mvua zimekwisha ndiyo mtu wa Liwale anaweza kwenda Liwale; lakini inambidi atoke Dar es Salaam mpaka Lindi, Lindi mpaka Masasi, Masasi – Nachingwea ndipo anakwenda Liwale. Jamani hata huruma hatuwaonei hawa watu? Wakisema hawako Tanzania wako Tanganyika mtakubaliana nao watu wa Liwale wako Tanganyika. Hawawezi kwenda Liwale, nauli ya kwenda Liwale utafikiri anatoka hapa anakwenda Kampala wakati anakwenda sehemu ya karibu tu hapa. Na ahadi zimetolewa za uwongo kwa muda mrefu. Tufike mahali tuachane na uwongo twende na ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Waziri mwenye mamlaka aniambie ni lini barabara ya Liwale itajengwa kwa lami? Tumechoka na ahadi za uongo ambazo hazikamiliki. Kama ni maisha bora ya Watanzania hata mtu wa Liwale anahitaji maisha bora, hata wananchi wa Nachingwea wanataka maisha bora, hata mwananchi wa Ruangwa anataka maisha bora. Tunataka barabara za lami zifike katika maeneo, Mkoa wa Lindi wote hauna barabara za lami, haiwekezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaingia katika suala la mazao, anatoaje mazao kutoka vijijini kwenda barabara kubwa, hakuna barabara. Nimejaribu kuleta maswali wakasema watatoa pesa hakuna pesa iliyofika mpaka sasa hivi. Nangalu – Chikonji waliniambia tutatoa milioni 700 hakuna pesa. Mchinga – Kijiweni hakuna pesa iliyopelekwa, Mkwajuni Mipingo hakuna pesa iliyopelekwa kule, tunaingiaje katika uwekezaji hakuna hata mazingira bora ya barabara na mawasiliano hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunataka kuwekeza kilwa na ndilo eneo la pili limeonekana bora katika uwekezaji, hakuna usafiri bora unaozunguka katika maeneo ya Kilwa. Kwenda Njinjo, kwenda Kandawale, kwenda Mitole, utafikiri eneo lile halijapata uhuru katika miaka 50. Watu wako katika mazingira magumu, kuna ubaguzi mkubwa unafanyika katika kugawa miradi. Kuna mikoa inapata upendeleo, Mkoa wa Lindi kila siku wa mwisho, lakini Mungu ameleta ruzuku ya neema, hii neema mnaifanya nini? Neema hii haitamsaidia mtu wa Lindi, itatusaidia Tanzania nzima, tufike mahali tutathmini tulijipanga kwa future au tumejipanga for wait and see attitude? Haikubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri mwenye dhamana aniambie katika uwekezaji alioupeleka Lindi anataka kutupatia kitu gani Lindi, amejipanga vipi kuhusu mawasiliano, kuhusu uchukuzi, amejipanga vipi kuhusu barabara, nitawaelewa kama kweli mnataka maendeleo, lakini bila hivyo sijaona kama kuna juhudi za kikamilifu za kupeleka maendeleo Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Lindi ni Mkoa ambao sasa hivi unaona neema, lakini unaona mipango iliyopangwa ya hovyo hovyo, tunahitaji mabadiliko ya kweli na ya dhamira ya kumkomboa mwananchi wa Lindi na Tanzania kwa Ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja suala la maendeleo ya barabara, nilileta maswali hapa wakasema fedha tayari zimeshapelekwa Lindi naomba Waziri mwenye dhamana aniambie ni fedha gani zimepelekwa Lindi vijijini kwa ajili ya zile barabara? Sasa hivi Ufuta huko vijijini unashindwa kuja mjini, barabara hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Nangaru leo wamekaa na ufuta vijijini wanatafuta barabara, hawana! Sasa tutafutieni njia maana yake tumejaribu kuongea imekuwa kama tumemfungia kengele mbuzi , tunaomba majibu yenye dhati, ni lini daraja la Mchinga, kijiji cha muda mrefu, Makao Makuu ya Jimbo hakuna daraja la kutoka Mchinga kwenda Kibiweni, Mheshimiwa Rais mwenyewe Magufuli alifika Lindi akasema nitajenga hili daraja la Mchinga na mimi ni mlezi wa hapa, naomba Waziri mwenye dhamana alimalize daraja la Mchinga na watu wa Mchinga waneemeke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ahsanteni sana.