Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Kwanza kabisa nampongeza Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu, Naibu Waziri Mheshimiwa Chande, Makatibu Wakuu kwa bajeti nzuri, bajeti kubwa ya shilingi trilioni 44.38 ambayo ina wagusa Watanzania wote, inaleta matumaini mapya. Kwa kweli Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Chande mnafanyakazi nzuri sana ya kumshauri Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa na mazuri ambayo yanayoendelea kufanyika ndani ya Tanzania. Tunaona kwamba uchumi unaendelea kukua na kwa kutambua kwamba Watanzania wengi ni wakulima tumeona kwa jinsi gani bajeti ya kilimo ambavyo imekuwa ikipanda kila mwaka, lakini vilevile imekuwa ni tatizo na watu wengi wamelizungumzia. Sasa hivi Serikali imekubali inaenda kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma kwenye vyuo vya kati, hawa ndio wataalamu tutakaohitaji katika viwanda vyetu, lakini hawa watoto au wanafunzi watapata stadi zitakazowawezesha waweze kujiajiri na hivyo tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira katika Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali ya CCM kwa kuwajali watu wenye ulemavu kwa sababu nimeangalia kwenye bajeti hii ukurasa wa 10 unasema Serikali inaenda kutenga shilingi bilioni moja, iwekwe kwenye mfuko wa watu wenye ulemavu ili waweze kuweza kupata vile vifaa wanavyohitaji, Mheshimiwa Waziri bajeti ni nzuri hongereni sana kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda leo nitaongelea kitu kimoja tu; na nitaongelea Mkoa wa Kagera na umaskini ndani ya Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera ni maskini, lakini kwa fursa zilizo Mkoa wa Kagera, Mkoa wa Kagera haupaswi kuwa maskini, Mkoa wa Kagera una ukubwa wa kilometa za mraba 35,686, una idadi ya watu wanakaribia milioni tatu, una mvua misimu miwili kwa mwaka, una wasomi kibao, umepakana na nchi jirani nne, lakini mkoa bado ni maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa za mwaka 2022 pato la mwananchi mmoja mmoja kwa kigezo hicho Mkoa wa Kagera ni mkoa wa mwisho katika Tanzania Bara kwa umaskini, lakini kwa miaka zaidi ya mitano consecutively Mkoa wa Kagera umekuwa kati ya mikoa mitano ya mwisho kichumi. Kwa hiyo, Mkoa wa Kagera ni mkoa maskini. Kwa kutumia kipimo cha umaskini wa mahitaji ya msingi (basic needs poverty), Mkoa wa Kagera una wastani wa asilimia 31.9 wakati wastani wa kitaifa ni asilimia 26.4 kwa maana hiyo Mkoa wa Kagera bado una hali mbaya kimaskini. Kwa kutumia kipimo cha umaskini wa chakula ambayo ni food poverty Mkoa wa Kagera una asilimia 12 wakati wastani wa Taifa ni asilimia nane. Kwa hiyo, inaonesha kwamba mkoa bado ni maskini zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera kama nilivyotangulia kusema kwa zaidi ya miaka mitano sasa unaendelea kuwa kati ya mikoa ya mwisho mitano kwa umaskini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Waziri Mkuu statistics au takwimu huwa hazidanganyi, hivyo Mkoa wa Kagera tukubali, Mkoa wa Kagera una hali mbaya, umaskini umekithiri, lakini Wabunge tumeongea sana humu, kila Mbunge wa Kagera alipoinuka alizungumza juu ya umaskini wa Mkoa wa Kagera, mimi mwenyewe nafikiri ni mara ya tatu. Ukisoma kwenye mitandao ambayo imeundwa kwa watu wa Kagera wanaokaa Tanzania na wanaokaa nje kila mtu anaguswa na kila mtu anazungumzia juu ya umaskini wa Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile hata Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipokuja mkoani Kagera kitu cha kwanza ambacho wazee wa Mkoa wa Kagera walimkabdidhi ni kwamba tunafanyaje, tunatokaje kwenye huu mkwamo ambapo kwa sasa hivi inaonekana kwamba mkoa wetu ni wa mwisho, ni mkoa maskini kuliko mikoa yote Tanzania Bara na yeye akatoa maagizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napenda Serikali mtueleze baada ya kuona mkoa ambao ulikua upo kati ya the best three, kati ya mikoa mitatu iliyokuwa inafanya vizuri kielimu, kati ya mikoa miatatu iliyokuwa inafanya vizuri kimaendeleo, sasa hivi umekuwa mkoa mwisho. Nina uhakika Mheshimiwa Mwigulu na wewe hili linakugusa, nina uhakikia Mheshimiwa Chande na wewe linakugusa na Waziri Mkuu na wewe na wote. Tunafanyaje? Mmeshafanya utafiti mkaleta REPOA, mkaleta kamati zenu hizo zinazoshauri kiuchumi katika Wizara wakaangalia tatizo ni nini ndani ya Mkoa wa Kagera? Kwa nini tunakuwa wa mwisho? Mnapopeleka hizi pesa mafungu yote miradi mnaleta, it doesn’t work bado tunaendelea kuwa wa mwisho. Kwa hiyo ina maana kwamba tunahitaji mkakati zaidi ya hizi hela za kawaida zinazopelekwa katika Mkoa wa Kagera na kwa sababu sasa sina muda nitaongelea mambo machache tu ambayo mimi nafikiri yakifanyika yanaweza kusaidia kufungua Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza biashara ya mpakani; sisi tunapakana na Uganda, tunapakana na Kenya, tunapakana na Rwanda, tunapakana na Burundi. Kwa kufanyabiashara tu ya mpakani ambapo ni eneo ninalofikiri Mheshimiwa Waziri wa Fedha naona kama Tanzania hatufanya vizuri kwenye kutafuta biashara ya kuendeleza biashara mipakani, lakini sisi kama Mkoa wa Kagera tunaona kwamba biashara ya mpakani ikiweza kuboreshwa inaweza ikatusaidia na kututoa katika mkwamo tuliopo.
Kwanza kabisa tunaomba tujengewe masoko, tujengewe soko pale Mtukula ambapo ni Misenyi kwenye mpaka wa Mrongo ambapo ni Kyerwa, kwenye mpaka wa Rusumo na Kabanga ambapo ni Ngara. Kwa kufanya hivyo tutafanya biashara na nchi jirani, na hii itafungua mkoa na kutakuwa na mzunguko wa pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika sasa unaona kwamba hata wafanyabiashara wa Tanzania wanahama wanaenda kufanyiabiashara zao upande wa pili kwenye nchi jirani badala ya kufanyia Tanzania. Ni kwa sababu sera za kule, uharaka wa kuanzisha biashara kule, sera zao za kodi zinawavutia kuliko za hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali tujiangalie upya, tuangalie sera zetu mipakani zinasemaje kusudi tuweze kuwavutia sasa wasiende upande wa pili. Serikali ya Tanzania, National Housing imejenga mall pale Mtukula, lakini ni kwa muda mrefu imeshindwa kujaa, wafanyabiashara wana-prefer kwenda upande wa Uganda kuliko kufanyia Tanzania. Mlituahidi kutujengea pale soko, lakini ukienda ni vumbi tupu, wakati wa mvua ni matope matupu. Nani atakuja kuwekeza? Hakuna hata storage facilities. Tunaomba tujengewe masoko ya uhakikia kuweza kuufungua Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Spika, lakini Mkoa wa Kagera mnajuwa tupo pembezoni ni mbali sana na Dar es Salaam ambapo ndio malighafi nyingi zinapatikana kilometa zaidi ya 1,500. Kwa hiyo, huyu mwekezaji ambaye anaamua kuwekeza ndani ya Kagera, cement wakati Dar es Salaam inanunuliwa shilingi 13,000; shilingi 15000 ikija kufika Kagera imekuwa ya shilingi 23,000 na shilingi 25,000. Gharama za uzalishaji zinakuwa nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali mmeshajiuliza wakati mnahamasisha viwanda vingi vianzishwe watu wawekeze kwenye viwanda, kwa nini Mkoa wa Kagera tulipata wawekezaji wachache sana? Ni kwa sababu ya gharama za uzalishaji tuko nazo mbali sana, ndio maana mwaka 2015 Mkoa wa Kagera ulikuwa na kongomano la uwekezaji, waliomba na wameleta Serikalini na hamjatujibu, tunaomba tupate upendeleo maalamu (preferential treatment) ya kikodi, ya kisera, ya kisheria ili kusudi tuweze ku- compete, tuweze kuwa na ushindani kuwa na ushindani ulio sawa na nchi zilizo jirani ambapo inaonekana sera zao zinavutia zaidi, lakini mpaka leo hamjatujibu na sisi tunaendelea kuwa maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali mtusaidie kwa kuboresha biashara za mipakani, lakini vilevile tupate hiyo preferential treatment ili tuweze kushindana na kuboresha biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera ni predominantly rural yaani maeneo mengi yamekaa kama vijiji. Kwa hiyo, kitu cha kututoa sasa ni kilimo, Mheshimiwa Bashe kitu cha kututoa kwenye umaskini Mkoa wa Kagera ni kilimo. Tunalima kilimo ambacho hakina tija, matumizi ya mbolea yako chini sana, mazao/mimea tuliyokuwa nayo ni imezeeka, kwa hiyo tunaomba Serikali waje watusaidie watupe pesa kusudi tulime kilimo ambacho kina tija, wang’oe ile mibuni na migomba ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza mwaka jana Serikali ndio imetuletea mbolea tani 2,600 yenye thamani ya shilingi bilioni 7.5 na kati ya hizo shilingi bilioni nne zote zilikuwa ni ruzuku iliyotolewa na Serikali, tunasema ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri awahamasishe Wanakagera walime kwa kutumia mbolea ili tuweze kupata kilimo chenye tija, lakini vilevile tunapopata ushuru haya mazao yote yakiuzwa kahawa ikiuzwa, kwa mfano kama mwaka jana ushuru kutoka kwenye kahawa ilikuwa shilingi bilioni 4.5, ni kiasi gani kilirudishwa katika kuendeleza zao la kahawa? Unakuta kwa sababu Halmashauri zina mambo mengi yanayofanywa haziwezi kuendelea kurudisha hela kwenye kilimo zinaenda kwenye huduma kama afya, kama maji ni vizuri, lakini ni kiasi gani kinachorudi kuendeleza kilimo? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Wizara ya Kilimo…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba yako mengi ya kuongea Waziri wa Fedha anapokuja kuhitimisha tunaomba atueleze kuna mpango gani makusudi wa kuweza kwenda kusaidia Mkoa wa Kagera, kuutoa kwenye mkwamo, waondoke kuwa mkoa wa mwisho wa umaskini ndani ya Tanzania, ahsante sana. (Makofi)