Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Leo nitaanza kwa maeneo machache sana kwenye elimu kwa sababu mengi wameyafanya. Kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita. Mambo mengi sana yanayohusu elimu hasa ya vyuo vikuu yametekelezwa lakini niseme tu machache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaja kwako katika kuchangia, Mheshimiwa Waziri wa Elimu kuna mambo fulani inabidi umuone huyu Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kwanza niseme ukweli Waziri wa Fedha pamoja na msaidizi wake mmekuwa ni watu mnaoweza kufikika, hakuna ubaguzi ninyi ni kati ya wale Mawaziri ambao ni rahisi sana kufikika, nyie wenyewe mnajua jamani Waheshimiwa Wabunge, Wizara ya Fedha tumekuwa na Mawaziri ambao unaogopa hata kumkaribia lakini Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nikupongeze kwa hilo na hasa kwa kujali makundi yote ya Wabunge wanafika kwako unawasikiliza. Wakati mwingine ndiyo hapa ndani lazima utibuliwe wewe ni Waziri wa Fedha lakini huna hasira, huna chuki wala huweki kinyongo. Endelea na hivyo and that is leadership. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme suala la mikopo nikuombe sana sana Waziri hivi vyuo vya kati vipewe mikopo ikiwemo vyuo vya maendeleo ya jamii. Nimeona wakati Waziri wa Elimu anajibu anasema ooh, vyuo vya kati sijui VETA na nini tunaangalia. Tukiaza hivyo lazima kutakuwa na malalamiko. Kama tumesema vyuo vya kati vipewe mikopo ni vyuo vyote vya kati ili isilete shida. Hawa watu wataleta shida tu, tutapata tena message mimi nimechaguliwa chuo cha kati sijapata mkopo. Kwa hiyo, hakikisha wewe ni mjanja tafuta fedha ili kama kuongeza muweze kuongeza ili fedha hizo hata hivi vyuo vya kati vyote vipate mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije jingine naomba tu kukumbusha kwamba kwenye ile fedha ya HEET nimepata tetesi mnafanya allocation. Fedha za HEET ni kwa ajili ya universities. Mnafanya allocation sasa kama mnafanya hakikisheni kwamba hata Chuo cha Mwalimu Nyerere wanapata kwa sababu wana miundombinu ambayo inabidi waitengeneze lakini pia kuna branch yao kule Pemba. Kwa hiyo, kama mtafanya allocation kwenye HEET fanyeni allocation hiyo muhakikishe hiki chuo kinapata fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye elimu, Waziri wa Elimu aliahidi kwamba mishahara ya Wakuu wa Vyuo itafanyiwa kazi, mpaka leo kimya. Nimuombe Mheshimiwa Mkenda aje aonane na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, aonane na Mheshimiwa Simbachawene wa Utumishi mlimalize hili limechukua muda mrefu. Mkuu wa Chuo anapata mshahara sawa na lecturer wa kawaida, jamani inatoka wapi hiyo? Hebu tulimalize hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemaliza huko. Nakuja kwenye Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii. Nashukuru kwamba walitengewa shilingi bilioni 40 Bajeti iliyopita, sasa hivi wana shilingi bilioni 71 ni vizuri ongezeko ni zuri lakini niseme bado ni kidogo mno. Hii Wizara ina madudu mengi mengi, maadili, ukatili wa kijinsia, ubakaji, ulawiti, vipigo, ukeketaji ambao unaendelea ingawa Waziri alisema eti amemfunga ngariba mmoja. Ngariba mmoja unamfunga halafu unakuja kutuambia hapa kwenye Bunge kweli? Wakati mangariba wako kibao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ulawiti unaendelea, ndoa za utototni. Kwa hiyo hii Wizara ina mambo mengi mengi. Nimuombe Waziri wa Fedha sasa nikuombe. Hizo fedha za kodi unazokusanya hizo naomba uzitenge nyingine kwa ajili ya ulinzi wa watoto. Hapa kuna fedha zinatengwa kwa ajili ya ulinzi hata sisi hapa tunalindwa, hakuna mtu anayeweza kuingia humu akatufanyia mambo yale mabaya lakini ulinzi wa watoto bado. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nakuomba halafu wewe unapenda sana watoto. Sijawahi kuona Mbunge yeyote au mwanaume yeyote wa Kitanzania anabeba mtoto mgongoni. Wewe unapenda watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili ulifanyie kazi. Kwenye hizo fedha unazokusanya za kodi hakikisha tunapata ulinzi wa watoto. Mpe fedha Mheshimiwa Masauni, mpe fedha Mheshimiwa Gwajima, mpe fedha Mheshimiwa Simbachawene, fanyeni kazi kwenye ulinzi wa watoto nimesema tafuteni dawa. Tafuteni dawa kwa wanaume wabakaji wote na walawiti na fedha hizo unaweza ukazipata. Tukifanya hivyo nakwambia mambo haya yatapungua tu. Nimeshasema mara nyingi hapa hivi mnaona tabu gani kuwa hasi hao? Na wao hawawezi kuwa hasi mpaka wewe utoe fedha ili hao Mawaziri wengine wenye hizi sekta waweze kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema jambo la ndoa za utotoni. Yaani mpaka wakati mwingine nashindwa kuelewa. Tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Katiba alimhakikishia Mheshimiwa Spika ndani ya Bunge hili kwamba ataleta muswada hapa tukapitisha sheria. Sasa nasikia pembeni pembeni vinakuja vikundi mbalimbali eti ndoa za utotoni ziendelee. Nimesema mara nyingi jamani mtoto wa miaka 12 anaolewa anakwenda kufanya nini huko? Mbona hatuna uchungu na mabinti na haya mambo yote yanayohusu watoto wa kike, yanayohusu wanawake hayafanyiwi kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wangekuwa wanakeketwa wanaume ukeketaji ungeisha, wangekuwa wanaolewa wanaume wadogo, ndoa za utotoni zingeisha lakini mambo yanayohusu wanawake kwa nini Serikali hamtaki kuifanyia kazi? Watoto wana keketwa kila siku, Serikali mpo, vyombo vya dola vipo eti mnasema hamuwezi kujua wanafanya kwa siri, nchi hii tunashindwa kulikomesha hilo? Mbona la ualbino tulilikomesha kwa sababu gani la ualibino lilikwisha? Kwa sababu waliokuwa wanaathirika ni watu wenye ualbino wanaume na watu wenye ualbino wanawake na ndiyo maana lilipungua na likaisha. Leo hii kwa sababu wanaokeketwa ni wanawake Serikali mko wapi? Mheshimiwa Waziri wa Fedha toa fedha zikafanye kazi kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaki hiyo ya ukeketaji wala hatutaki hiyo ya ndoa za utotoni. Mnatuletea hapa taratibu za ajabu eti watu wanasema sheria, sijui utamaduni. Mbunge gani hapa atatoa mtoto wake wa miaka 12 akaolewe? Nani atatoa mtoto wake wa miaka 10 akaolewe? Wanasema tu pembeni huko, wawalete watoto wao hapa ili wakaolewe kwa miaka hiyo 12. That is uncouth, inasikitisha. Wanawake tusimame ndani ya Bunge hili tukatae. Leta Muswada hapa tujadili msiufiche fiche huko kwa kusikiliza vikundi vya watu wachache. Tamaduni zilizopitwa na wakati ziondoke ili mwanamke huyu akombolewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nimekupa kazi na sisi tunasimamia Serikali kwa hiyo mimi nakusimamia leo Mheshimiwa Mwigulu toa fedha, utoe fedha za kuwatunza watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nikushukuru sana. (Makofi)