Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mchango wangu katika eneo hili la Bajeti Kuu ya nchi na leo kidogo niko kizalendo zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ni majemedari wa kupiga kelele na kuzungumza sana maneno makali katika mitandao na kila maeneo mengi sana. Maneno haya yangekuwa yanatoboa mwili wa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, leo angekuwa amejaa bandage mwili mzima. Kwa hiyo anachotakiwa hapa sasa hivi ni kuwa na ngozi ngumu tu na kujenga imani halafu baadaye anatoboa. Nchi inatukanwa kila kona na sababu ya nchi kutukanwa kila kona ujue watu wamechoka, hawana pesa mifukoni. Kwa hiyo, mtu akikaa akafikiri hana cha kufikiri anaingia kwenye mtandao anaanza kutukana, sasa hili lazima Waziri alijue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uandaaji wa bajeti huu ni kwamba wakati wanaandaa bajeti, hawa watalam wetu wawe wanaita na sisi tuliyochomwa jua sana huku mtaani tuje tuwashauri namna ya kuandaa bajeti. Kuna vitu ambavyo sisi tutawaeleza hiki weka, hiki punguza, hiki toa, lakini wakijifungia ndani wenyewe waliokaa kivulini wanakaa kwenye AC, magari yapo yapo kwenye AC na kila kitu, wakimpelekea Waziri huku, huku Waziri anaendelea kutukanwa sana. Sasa naye ana wataalam wanaomzunguka hali siyo nzuri, huku chini Mheshimiwa Waziri wa Fedha miradi mingi sana inafanyika, tembea nchi nzima mabarabara yanatengenezwa, majengo yanajengwa na kila kitu kinakwenda katika nchi hii, maendeleo yanazunguka kama tairi la gari. Nchi inakuwa kama imepata uhuru sasa hivi, kila kitu kinafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote kuna jambo la kujiuliza, kwa nini kelele zinakuwepo? Huku chini kuna watu wakitoka ndani saa kumi na mbili asubuhi kwenda barabarani kutafuta pesa wanachomwa jua mpaka saa kumi na mbili jioni, anarudi na elfu tatu na elfu mbili, anapitia dagaa anakwenda kula nyumbani kwake, hawa watu wapo wengi kwenye nchi hii. Sasa Waziri alete mipango ya kupata pesa, wananchi huko wapate pesa na zenyewe zizunguke sasa kama tairi la gari, kelele zitapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipi kifanyike? Lazima waangalie huku chini wananchi wanatakiwa sasa wapate miradi itakayowaendesha, yatengenezwe masoko ya gharama nafuu. Haya masoko yanayokwenda kujengwa, Mheshimiwa Waziri wa Fedha angekuwa ananisikiliza ananiangalia, unafahamu akianza tena kula story mambo yatakuwa magumu sana huku, kwa sababu kuna mambo makubwa hapa ndani anatakiwa ayasikilize…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam, unaongea na kiti…
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti na yeye awe ananiangalia na ananisikiliza…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam naomba ufuate utaratibu.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MWENYEKITI: Ongea na kiti.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Sawa, ananiangalia kwenye TV, haina neno. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza na Waziri wa Fedha ni kwamba iko miradi mingi inayokwenda na pesa nyingi zimekwama. Kuna magari mabovu, kila Halmashauri kwenye yadi zao wana magari mabovu mengi yamekaa. Haya magari yalikwenda pale kupakiwa yamesimama ni mabovu. Haya magari kwa nini yasiuzwe? Msajili wa Hazina amepita kukagua magari nchi nzima, yako kwenye ofisi zote, polisi kila mahali kwa nini hayauzwi haya magari tukapata pesa ili zirudi kwa wananchi huku chini zikafanye kazi? Kwa nini wanakuwa na vitu vibovu wamevishikilia, wanayasubili na yenyewe kwa ajili ya kuja pata urithi, nani aje apate urithi wakati sisi tuna shida leo? Yauzwe haya magari, watu tupate pesa huku za kuendesha ofisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pointi nyingine ninayotaka kuieleza hapa, nataka kumweleza Waziri suala la msingi sana ni suala la kilimo. Huko kwenye kilimo sasa hivi Serikali imeweza kutoa pesa kwa ajili ya ruzuku ya mbolea, ruzuku ya petroli, dizeli na kila kitu, mabilioni ya shilingi. Kama tumeweza kutoa mabilioni ya shilingi kwenye ruzuku kwa nini tusitoe pesa zikanunuliwe trekta za gharama nafuu? Massey Ferguson, zikanunuliwa Swaraj, hizi trekta wakagawiwa wananchi kule, wakakopeshwa, wakapimiwa mashamba, hapa yuko Waziri wa Ardhi, wapime mashamba kwa Hati za Kimila zitumike kama dhamana, watu wapewe matrekta kule kwa ajili ya kuboresha kilimo chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mitambo ya kuchimba visima, sasa kwa nini ile mitambo ya kuchimba visima kama wanaweza kutoa ruzuku kwa nini isingie tukaagiza mitambo mingi zaidi, ikapelekwa sasa Wizara ya Kilimo? Wizara ya Maji wanachimba visima vyao na Wizara ya Kilimo wakachimbe visima, tusitegemee kilimo hiki cha mvua, tulime zaidi ya mara tatu kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupa mfano, nina eneo tu Sengerema, Sengerema imezungukwa na Ziwa kwa asilimia 68. Tunao vijana kule sisi Sengerema wamekaa katika makundi, leo mwaka wa tatu wanakaa wanasubiri kupewa mitambo ya irrigation. Waziri Jafo alisema, Waziri nanii, Waziri nani huyu? Waziri Bashe anasema kwamba anakwenda kutengeneza irrigation Kanda ya Ziwa. Wasilete miradi mikubwa ya bilioni nane, bilioni sita wanunue mashine za dizeli, mashine za water pump umeme sasa hivi upo kila kona, tufanye irrigation, sisi tuna uwezo wa kuzalisha na kulipa ile mikopo kwa haraka. Haya ni mambo ambayo wanatakiwa wayafanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uwekaji wa stempu, uwekaji wa stempu wa ETS ni wa muhimu sana kwa manufaa ya nchi. Sasa bidhaa zinazowekwa sasa hivi yule bwana wakati anapewa kazi alikuwa na viwanda vichache. Leo viwanda vimekuwa vingi zaidi ya mia tatu, lakini kuna bidhaa nyingine bado zinatakiwa wakaweke mpaka kwenye majani ya chai, majani ya chai yanatengenezwa ya paketi wanatengeneza kila kitu, leo Mheshimiwa Waziri ameweka mpaka kwenye maji. Sisi tuna shida na kodi na hawa wanavyokuja kuweka basi kelele zipungue kwa sababu hao wenye viwanda vikubwa wanadai shilingi nane inayowekwa kule ni kubwa. Basi wakae na huyu mtu SICPA apunguze bei angalau shilingi tatu hivi viwanda sasa, hawa wawekezaji wetu wa ndani wakawalinde. Hakuna namna ya kulinda viwanda vya ndani isipokuwa kuvipunguzia mzigo uliopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekaji wa stempu uende kwenye bidhaa zetu ikiwezekana kwenye cement, sukari kila kinachozalishwa kwenye nchi hii kiwe kina nembo ya kwetu na hawa watu stempu zao, stempu wanaleta kutoka nje, kutoka Uswisi kwa nini wasiweke kiwanda hicho cha kutengeneza stempu hapa hapa? Vitu vyote vikafanyika hapa hapa Dar es Salaam, kama ni Dar es Salaam au kama ni Dodoma tutakuwa tumepunguza mzigo mkubwa kwa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi na ninachotaka kuomba kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, suala hili linalopigiwa kelele, hili la bandari. Suala la bandari, watupe fedha sisi Wabunge, huku tunavyozungumza twende Majimboni tukapige mikutano tuwaambie wananchi. Hakuna namna nyingine ya kwenda kueleza wananchi kutoa huu uongo, hawa watu walikuja na hoja ya kuzuiwa kufanya mikutano. Wakafunguliwa kufanya mikutano, wakaja na hoja ya Katiba mpya, Rais yeye ndiye alikuwa Makamu Mwenyekiti anaendesha hapa kiti cha Katiba mpya wakaikataa Katiba mpya na yeye ndiye alikuwa Makamu Mwenyekiti. Mwenyekiti wake amekufa, Mheshimiwa Sitta yeye akabakia, ndiyo Mwenyekiti sasa hivi wa Katiba, hilo na lenyewe limejifuta, wamehamia kupotosha kwenye bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa twende kule sisi tukawashughulikie, tukawaeleze wananchi ukweli kuhusiana na suala la bandari. Bandari ndiyo mlango pekee utakaokuja kututoa sisi kwenye matatizo, bandari ile inaingiza trilioni 1.6. Haiwezekani ikaingiza pesa ndogo kiasi hicho halafu tukaacha ile bandari ikaendelea kukaa pale. Walio wengi wanaopotosha pale ni waliokuwa na maslahi na ile bandari, wanandugu wa ile bandari wanapotosha, wanapewa pesa kwenye mitandao, wapotoshe kwamba bandari inauzwa, bandari inauzwa kwa lipi? Kitu kipo katika mikataba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inahitaji tutoe elimu kwa wananchi waeleweshwe zaidi na sasa hivi hawana sehemu nyingine yeyote wanayotegemea kupiga kelele isipokuwa ni hiyo. Mheshimiwa Waziri awe na ngozi ngumu na ninachotaka kumwambia aendelee kusimamia, lakini awakumbuke wachomwa jua, hakuna namna nyingine ya kuweza kuwakumbuka wachomwa jua isipokuwa hilo jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la mwisho ni suala la elimu. Haiwezekani tuna misitu kuanzia kule kwako, iko misitu Mafinga, Sengerema kule sisi Buyingi tuna misitu mingi, kwa nini Serikali isitoe cubic meter elfu kumi ikachana mbao za moja kwa nane au moja kwa kumi, wakanunua square pipe, tukatengeneza madawati nchi nzima? Watoto wanakalia mawe wakati tuna misitu imejaa hapa. Inakuwaje namna hii? Mheshimiwa Waziri wa Fedha angekuwa amekali mawe, angekuja kuwa Waziri Fedha? Khee! Inakuwaje namna hii lakini na Naibu Waziri wa Fedha wangekuwa wamekalia mawe wangekuja kuwa katika hali hiyo? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusitengeneze madawati nchi nzima? Madarasa yaliyotengenezwa kwenye nchi yote ya Mama Samia yalikuja na madawati yake, haya madawati yaliyokuwa ya Marais wengine waliotangulia, watoto wanakalia mawe kwenye nchi hii. Kwa nini tuna misitu mikubwa namna hiyo? Mafinga iko pale imejaa, Sao Hill imejaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie katika jambo hili, hili jambo ni gumu. Hatuwezi kujenga madarasa mapya, yale madarasa yaliyokuwa zamani yote yana hali mbaya, hayana madawati na hatuwezi kuwa salama sisi Wabunge kama watoto wanakaa chini, tuone huruma katika jambo hilo. Najua nchi ina mambo mengi, lakini kama tumeweza kutoa ruzuku, Wizara ihakikishe watoto wanakalia madawati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo Waheshimiwa Wabunge wanatakiwa waniunge mkono kabisa, hoja ya madawati iwe ni hoja ya nchi, hoja ya madawati ni hoja ya nchi, madarasa ni mengi hatuna jinsi. Walimu namna ya kuwafundisha hawa Watoto, wanapata tabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, namshukuru sana Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa kunijengea jengo la TRA, Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho sasa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Waangalie Sheria za Kodi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, Mheshimiwa Mwigulu, ahsante sana, hali siyo nzuri huku hela hakuna. (Makofi)