Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kuipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiongozwa na Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, pia napenda kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na ndugu yetu Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, kwa pamoja na juhudi zao zote wanazofanya kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu na timu yake yote katika kutupambania sisi Watanzania kutatua changamoto mbalimbali zinazotukabili pamoja na bajeti nzuri hii waliotuletea, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu napenda nijielekeze kwanza kwenye sekta ya kilimo. Bajeti ya Kilimo sasa hivi imefikia bilioni 970.8. Ni safari ndefu, tumeanza mbali, napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi hiyo katika kutatua changamoto za wakulima pia kujiwekeza kwenye kilimo chenye tija kwa mwananchi mkulima lakini pia kwa faida ya Watanzania wote na Taifa letu kupata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza sana bajeti hii kwa kupunguza na kuondosha baadhi ya tozo na kodi mbalimbali kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na sekta zingine za kijamii. Napenda kuipongeza bajeti hii kuna mambo yametugusa sisi wananchi kwenye sekta zetu tunaofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu kwenye sekta hii ya kilimo. Napenda kuishauri Serikali kwanza naipongeza Serikali kwa kuongeza ruzuku kwa mbolea lakini naishauri tuendelee kujenga viwanda vingine vipya vya mbolea. Kwa zile malighafi za mbolea zinazopatikana ndani ya nchi tuendelee kujenga viwanda vyetu vya mbolea ili kukabiliana na changamoto hii, pia kukabiliana wakati itakapojitokeza majanga mengine na maafa huko duniani kwa sababu mbolea ni silaha kwenye kilimo chetu. Kwa hiyo, tukiwa na mbolea nyingi ya kutosha hapa nchini, tutaweza kutatua changamoto zetu bila kuagiza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya sukari. Bodi ya Sukari na Wizara ya kilimo imejipanga vizuri sana kuhakikisha tunakwenda kuongeza tija katika sukari lakini pia kuacha kuagiza sukari huko siku za baadae. Pamoja na hilo nia na dhamira ya Wizara ya Kilimo na Bodi ya Sukari ni kufufua Chuo cha Sukari kwa sababu sasa hivi tuna shida ya wataalam wa sukari hapa nchini, inalazimika wazalishaji kuagiza wataalam nje ya nchi. Kwa hiyo, mimi nashauri andiko lao hili lifanyiwe kazi ili kile chuo kifufuliwe na wanafunzi waanze kusoma ili tupate wataalam wetu wa sukari hapa ndani ya nchi tuepushe na tatizo la kuagiza wataalam mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu kwenye sekta ya uvuvi, nasisitiza tu uwekezaji Bahari Kuu uendelee ili tuweze kuingia kwenye sekta hii ya uvuvi wa Bahari Kuu pamoja na kulifufua shirika la TAFICO liongezewe fedha kwa haraka ili lianze kazi na mambo haya yaende sambamba kwenye sekta ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mazingira nashauri na mimi masuala ya nishati mbadala. Kutafutwe mbinu ya kupunguza gharama kwa mtumiaji mdogo wa chini ili kila mtumiaji mwananchi aweze kumudu gharama hizi za kutumia nishati mbadala ili kuepusha ukataji wa miti ambao unaharibu mazingira ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ajira Serikali inajipanga sana sekta mbalimbali kuhakikisha vijana wanapata ajira, lakini kwenye ajira kuna wanaopenda kilimo, wanaopenda uvuvi, wanaopenda na kazi nyingine. Lakini kuna na wengine kila mtu kwa kipaji hake na utashi wake anapenda kile ambacho anakipenda. Mimi nashauri bado tuling’ang’anie soko la ajira kwenye lugha ya Kiswahili. Sasa hivi vyuo vingi duniani vinaanzisha mitaala ya lugha hii ya Kiswahili, bado hili soko linaandamwa na nchi jirani. Tujipange kuhakikisha hili soko tunalikamata sisi Watanzania kwa sababu sisi ndiyo wenye chimbuko la Lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea najikita kwenye amani na utulivu wa nchi. Bila ya amani bila utulivu wa nchi haya yote tunayoyapanga hayatatekelezeka ila nia ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anaishi kwa amani na utulivu katika nchi yetu. Napenda kuwapongeza Marais wetu kwa juhudi kubwa wanayochukua kuhakikisha amani na utulivu wa nchi unakuwa sambamba na hali halisi ya maendeleo ya nchi. Wanajitoa nawapongeza kwa uvumilivu wao na ustahimilivu wao, mengi yanawakuta wanayabeba, binadamu kapewa kifua cha mbele na cha nyuma, yote wanayabeba kulingana na hali halisi inayojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba viongozi wetu na wasaidizi wake ninyi Mawaziri wetu, muendelee kumpa moyo Mheshimiwa Rais, pia nasi tunaendelea kuwapa moyo ili mambo yetu ya kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo yafanyike. Ninachotaka kusema baniani mbaya lakini kiatu chake dawa. Viongozi wetu wanahangaika kutafuta miradi, kutafuta pesa kwa ajili yetu sisi Watanzania lakini sisi tunajifanya hatuoni. Naomba sasa Watanzania tuheshimu na tuthamini juhudi zetu zinazofanywa na viongozi wetu mbalimbali kwa sababu lililopo baharini lisubiri ufukweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanayofanyika kuna siku tutayaona na tutayafaidi sote, siyo hao viongozi wanayoyaleta. Sote Watanzania kila pembe tulipo, mafanikio haya tutayafaidi na tutajivunia hapo baadaye. Ndiyo maana nikasema lililoko baharini lisubirie ufukweni, tutaona na mwenye macho haambiwi tazama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ada ya mja kunena, uungwana ni vitendo, tenda watu wataona, majisifu weka kando, viongozi wetu wanatenda hawajisifu na tutayaona. Ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)