Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia pumzi pamoja na uzima wa afya, kuja kujadili bajeti hii ambayo tunapanga maendeleo kwa ajili ya Watanzania na cha pili, nashukuru kwako wewe kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapokuwa ameudhiwa au amepata jambo ambalo linampa maudhi, basi wale wenzake wanaompenda huwa wanamliwaza. Sasa kwa kuwa, mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunajua alipata maudhi na watu kwa kumsema vibaya hasa kwa kumbagua, kwa hiyo, nataka kumpa kijishairi kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shairi hili linasema, “Sharti uusafi moyo ukitaka kuwa mwema, uwafanyie wenzio kwa kubembeleza wema, watakuendea mbio upate kurudi nyuma. Wema uutekeleze bila ya kuweka tamaa, watu uwasikilize shida zao kusimama, kisha wema ukuponze ubaki unalalama.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunaelewa kwamba Mheshimiwa Rais alifanya wema kumtoa mtu gerezani na akafanya mengine makubwa tu, kumwachia baadhi ya rasilimali zake ambazo zilikuwa pengine zimeshafutwa, lakini bado ule wema umemponza mama, lakini hizi ni kama tasnia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 21 na 22 wa hotuba yake, katika Paragraph ya 146, alieleza pale mabadiliko ya Sheria ya SDL ambapo hii sheria inaitwa Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Sura ya 82. Mheshimiwa pale amefanya mabadiliko kwa kuweka 1/3 ya fedha zitakazopatikana na Skills Development Levy kwenda katika Wizara inayohusiana na kazi na ajira. Kwa hiyo, katika Wizara hii, kwa sababu kule kuna program ya kukuza ujuzi, program hii ya kukuza ujuzi ilikuwa iko chini, kwa maana hiyo tulikuwa tunashindwa kupata wataalamu. Kutokana na hiyo 1/3 itakuwa kubwa kwa zaidi ya mara 10. Kwa maana hiyo sasa, Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inashughulika na ajira na walemavu itapata hilo fungu kwa ajili ya kukuza ujuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali. Nampongeza na ninamshukuru Mheshimiwa Rais, amekwenda kukuza ajira kwa vijana wetu, anakwenda kukuza ujuzi kwa vijana wetu. Kwa nini? Tumetoka Shilingi bilioni tisa, kama tutaangalia katika Volume IV, kitabu kile page ya nne ya Skills Development Levy kutoka Shilingi bilioni tisa na kwenda kukaribia Shilingi bilioni 100 na kitu. Kwa hiyo, hii maana yake ni kwamba tunakwenda kujenga uwezo kwa vijana waweze kujiajiri. Pamoja na mama ametoa ajira, lakini pia vijana wanajengewa uwezo waende wakajiajiri. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali, tunakushukuru sana mama kwa kuwajali vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu. Fedha hizi, kama tunakwenda kukuza ujuzi tutengeneze skilled labors wa kiwango cha juu ili kuweza kumudu sasa kuingia katika Tanzania ya viwanda. Kwa sababu, mwanzo tulinadi Tanzania ya viwanda, lakini hatukuwa na watu waliokuwa na ujuzi katika sekta hizo. Kwa hiyo, tukajaribu kuangalia upande wa kukuza ujuzi ambapo tutavutia viwanda. Duniani hapa watu wote ambao ni wawekezaji wa viwanda wanatazama vitu kama mfano wa availability of raw materials na skilled labor. Sasa tukiwa na skilled labor ina maana tutaweza kutekeleza ile Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niishauri Serikali, kwa sababu kila sehemu wanakuza ujuzi, kila Wizara; ukitazama Wizara ya Kilimo wanayo hii program ya kukuza ujuzi, lakini pia Wizara ya Mambo ya Ustawi wa Jamii nao wanakuza ujuzi. Sasa tutazame katika instrument, ni nani ataratibu hili? Maana tukitapanya resources tutakuwa hatuna mratibu na tutakuwa hatuna namba ambayo tunataka kuijua kwamba hii sasa tumekua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ambayo ina kipato cha kati ilitakiwa iwe na at least asilimia 12 ya watu ambao wana ujuzi katika kazi, lakini sasa hivi tuko katika asilimia 3.6. Kwa hiyo, tunamshukuru sana mama, amewajali vijana wake. Vijana ajira zinakuja, mama ameweka Shilingi bilioni 112 katika kukuza ujuzi. Tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka niliongelee, Mheshimiwa Waziri amezungumza katika paragraph ya 151 ambayo ipo katika ukurasa wa 154 wa hotuba yake. Pale alizungumzia Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004. Mheshimiwa amependekeza katika 151 LN, kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye nyuzi za pamba (cotton) zinazotambulika kwa HS Code 52.05, 52.06, 52.07, anasema lengo ni hatua ya kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo kwa kuongeza thamani ya zao la pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Waziri hapa, lakini viwanda ambavyo tunavyo hapa Tanzania vinavyotengeneza hizi nyuzi za aina hii tuliyoitaja, wanatengeneza kwa ajili ya matumizi yao wenyewe na hakuna kiwanda kinachotengeneza kwa ajili ya mwenzie. Kwa maana hiyo, wanaonunua kutoka nje, huwa wananunua kwa sababu ndani hizi nyuzi hazipatikani, na viwanda vinavyotengeneza ukiwaambia labda walete quotation, bei yake inakuwa ni kubwa zaidi kuliko ile ya nje. Pia uwezo wa kutengeneza kibiashara, hakuna kiwanda hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ililisikia hili ikajipanga kuwaalika wawekezaji na wawekezaji walikuja, lakini Serikali yenyewe ilishindwa kwa sababu, imeshindwa kutoa incentives. Walitaka incentives, imeshindikana. Kwa hiyo, viwanda hivi vilipokuja, vikakimbilia Uganda. Kule Uganda wananunua umeme kwa senti nne. Sisi senti 10 ya Dola. Sasa ukienda Zimbabwe wananunua kwa senti nne. Hapa ni senti kumi. Uganda wamehakikisha wanawanunulia pamba wanawawekea kwenye maghala. Kwa maana hiyo, availability of raw materials imehakikishwa. Sasa sisi hapa kwetu haiko hivyo. Isitoshe, tukisema kwamba tumekipandishia hiki kiwanda asilimia 25 tunaenda kuua biashara yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Maendeleo na Ustawi wa Jamii tulitembelea kuangalia wafanyakazi. Pana wafanyakazi 8,700, ukisema hiki kiwanda kinashindwa kufanya kazi, umeondoa ajira za watu 8,700. Isitoshe Afrika Mashariki ushuru ni asilimia 10, Kenya Halimi pamba, lakini anatumia hiyo asilimia 10, Uganda asilimia 10. Sasa sisi tunashindwa kuingia katika ushindani. Soko letu tunalotumia, tunauza AGOA, tunauza South Africa na katika nchi nyingine. Wenzetu zinapatikana bidhaa zao kwa bei rahisi na sisi kwetu zinafeli kupatikana hizi bidhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, tujaribu kuangalia kwa sababu siyo kosa la kiwanda, ni kosa la Serikali kuweka incentives, kiwanda kimeshindwa. Tuweke incentives katika umeme, pia tujaribu kuangalia mazingira yote ya hivi viwanda ili vitusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii mia kwa mia. Naomba Mheshimiwa Waziri aje atupe majibu. (Makofi)