Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kukushukuru mwenyewe binafsi kwa kuridhia na kunipa nafasi na mimi niweze kutoa maoni yangu kwenye bajeti hii ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ilivyo ada, nianze kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kuwa nzuri anayoifanya, hasa mwenyewe kwenye jimbo lango. Hivi nimeongea na Mwenyekiti wiki hii ninaambiwa tumepokea zaidi ya milioni 570 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hivyo, nilikuwa na milioni 470 kwa mwaka uliopita pia kwa ajili ya sekondari mpya ya kata isiyokuwa na sekondari. Naendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anatushika mkono sisi wananchi wa Rorya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu tumekuwa na changamoto ya maji, lakini ninavyosema sasa hivi, katika miradi ya miji 28 tumepewa zaidi ya shilingi bilioni 132 kwa ajili ya utekelezaji wa maji na sasa tunajenga tanki la lita milioni sita kwa ajili ya kuhakikisha tunasambaza maji kwenye Wilaya yetu ya Rorya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana pia kwa kutupa fedha kwa ajili ya ujenzi wa VETA. Kubwa kuliko yote, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kuingiza barabara yetu ya Mika–Utegi–Shirati–Kirongwe, kwa ujenzi wa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kukuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha ulione hili kama fursa, kwa kuwa mama tayari sisi ametukumbuka na ameliweka kwenye bajeti, sasa iende ikatengewe fedha, itangazwe kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 56 ili angalau barabara hii kwanza inakwenda kufungua uchumi wa Wilaya ya Rorya pamoja na nchi jirani, lakini pia inakwenda kufungua uchumi wa Mkoa mzima wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi kama Serikali, kwa sababu barabara inakwenda kutuunganisha kati ya nchi na nchi, naamini kabisa mnakwenda kuvuna na kupata mapato kwa asilimia kubwa sana kupitia barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna kwanza ulivyojipambanua kwa namna ulivyokuwa unawasilisha hoja. Lakini pili, kwa namna unavyoendelea kumshauri Mheshimiwa Rais kusimamia sera zinazohusiana na sekta na Wizara hii ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa mambo matatu; la kwanza, nikushukuru sana kwa namna ambavyo umeweza kumshauri Mheshimiwa Rais kuridhia na kufuta ada kwa wanafunzi ambao wanasoma vyuo vya ufundi. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri hili umewasaidia sana wananchi wanyonge, hasa sisi Wabunge wa vijijini hili lilikuwa ni kimbilio kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; ni kuridhia kwenye vyuo vya kati kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi angalau waliochaguliwa kwenda maeneo hayo. Kwenye hili Mheshimiwa Waziri ningeomba nikushauri na ulitazame na ninaamini mwishoni uweze kuliwekea majumuisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati unatoa hotuba yako hapa ulijipambanua hadharani, wazi kabisa, na wananchi wote walikujua kwamba wewe ni mtoto wa mkulima, ni mtoto wa mfugaji, na umelelewa katika mazingira magumu sana. Wapo wananchi huko chini Mheshimiwa Waziri, kwa huu huu mkopo ambao tunakwenda kuutoa, maana yake ni kwamba tukisema tunatoa kwa badhi ya wanafunzi waliochaguliwa kwa baadhi ya kozi na kozi nyingine tusiwape mkopo, tunakwenda kutengeneza mpasuko sana huku chini kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, litazame Mheshimiwa Waziri; leo mtu na jirani yake, anamtazama mtoto wa kwake anakwenda kusoma chuo fulani anapewa mikopo lakini huyu ambaye amechaguliwa na Serikali kwenda chuo fulani hapewi mkopo, lakini wote wanaishi maeneo yaleyale, wote ni wajane, wote hawana fedha na wote ni maskini kabisa wa kutupwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ulione hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimechangia hapa, na ninaamini wananchi wanakuona, na wewe umejipambanua kama role model wa aina ya jamii fulani wanaotoka huko, litazame hili, ikiwezekana wanafunzi wote wanaokwenda kwenye vyuo vya kati wapewe mikopo, haijalishi huyu anakwenda kusomea nini na anasomea nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, ukirudi nyuma, hata huyu ambaye hakupenda asome yale masomo kwa mfano ya sayansi, ukirudi nyuma kwenye historia unaweza ukakuta si sababu yake, hakuwa yeye ndiyo chanzo cha kutokusomea sayansi. Unajua shule zetu zina changamoto nyingi sana za walimu wa sayansi kwenye baadhi ya maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiwatoa wale ukasema hawa kwa sababu wamechaguliwa kwenda kozi fulani kwa hiyo hawastahili kupata mkopo wanakwenda kupata wanafunzi fulani, utatutengenezea deni kubwa sana sisi Wabunge ambalo tulikuwa tumelitua, kwa msaada huu tulikuwa tumelitua. Nilikuwa na wanafunzi zaidi ya 50 ambao walikuwa wanatarajia angalau kufika mwezi Septemba tuwachangie kwa ajili ya kwenda kulipia ada, na ada ya vyuo unaifahamu, ni zaidi ya milioni moja mpaka 1,400,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, sasa litazame; kama mzazi alikuwa anashindwa kulipa 70,000, mama yetu kwa huruma yake akaamua kuiondoa hiyo 70,000 ya ada, leo 1,400,000 huyu mzazi anakwenda kuitoa wapi? Kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri utakapofanya majumuisho, ulikuwa una nia njema, lakini tukiliweka katika mazingira haya tunakwenda kuwagawa Watanzania na haitakuwa imependeza zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru pia kwa namna ambavyo umeendelea kumshauri Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kuondoa VAT kwenye nyumba zinazojengwa za kibiashara zenye gharama chini ya milioni 50. Wito wangu ni nini kwenye hili; real estate developers, hasa National Housing, TBA na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayofanya kazi ya development ya ujenzi wa nyumba, waitumie hii kama fursa ya ujenzi wa nyumba hizi za gharama nafuu ili waendane na malengo na dhamira yako iliyokusababisha kumshauri Mheshimiwa Rais. Ili angalau nyumba za bei nafuu zisizozidi milioni 50 zijengwe maeneo yote ya nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani niwaone Rorya wakija wanajenga nyumba milioni 25 kwa ajili ya kuwasaidia watumishi. Waende halmashauri nyingine wajenge nyumba milioni 30, nyumba milioni 35. Kwa sababu hawa real estate developers walikuwa wanalia kuhusiana na bei ya nyumba, na wananchi wengi walishindwa kulipia hizi nyumba kwa sababu ya ongezeko la VAT, na Mheshimiwa Rais ameridhia kuiondoa. Ninatamani sana hizi taasisi ziweze kujikita kutumia fursa hii kwa uzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, lingine ni Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi. Kwa mujibu wa sheria hii ambayo tunayo hapa; The Land Use Planning Act No. 6 ya mwaka 2007 inaipa mamlaka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, hawa ndio wanapewa mamlaka makubwa ya kupanga na kuainisha matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwenye mpango wako wa Tatu wa Taifa wa mwaka 2022/2023-2025/2026, anayekwenda kutafsiri ile asilimia 50 ya kuainisha mpango wa matumizi bora ya ardhi ni hii Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi; anayekwenda kutafsiri Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ukurasa wa 120, kwamba ni lazima tutakapofika 2025 vijiji viwe vimepangwa matumizi zaidi ya 4,131 ni Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anayekwenda kutafsiri hotuba za viongozi zinazozungumzia mpango wa matumizi bora ya ardhi ni hii tume. Na ndiyo maana kwenye sheria hii hawa ni National Planning Authority ambao kimsingi wanatakiwa wasimamie haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe Mheshimiwa Waziri utakuwa shahidi, hawa watu wamefanya kazi kubwa sana Msomera, wamefanya kazi Loliondo, sasa hivi wako Bunda, wanafanya kazi Tarime. Na hawa ndiyo wanahakikisha wanapanga matumizi bora ya ardhi kwa wale wananchi waliohamishwa Ngorongoro kwenda kule Msomera; wamefanya kazi kubwa sana nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, ninachosikitika kwa mara nyingi, na nimekuwa nikilisema sana hili; ni kwa nini tume hii, moja, hatuipi meno, lakini mbili, hatuitengei fedha nyingi ili iweze kuendana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, maelekezo ya Mheshimiwa Rais, lakini iendane na Mpango wako wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa. Kwa sababu inaonekana kama ni kitu ambacho hakipo na hakina umuhimu wake. Lakini ninyi ni mashahidi Mheshimiwa Waziri; kama tunataka tuondokane na migogoro nchini ni lazima tume iongezewe fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana wengi tumekuwa tukishauri hapa, kama tatizo ni fedha na nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, mwaka jana tulichangia ukaridhia kuongeza fedha ukawapa bajeti zaidi ya bilioni 5.4. Mwaka huu naambiwa mmeishusha, mnawapa bilini 3.7, na wakati malengo ni yaleyale, na hatujafikia dhamira ya Ilani, hatujafikia dhamira ya Mpango wa Tatu wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, nikuombe, kwa sababu tuna fedha ya mkopo, ile bilioni 345 mmege zaidi ya bilioni 20, bilioni 30, muwape hawa watu ili waende wakapange watumizi bora ya ardhi nchi. Na ninaamini kabisa kwa kufanya hivyo watakuwa wanatimiza na wanaendana na malengo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante kwa kunipa nafasi.